Choo cha serikali ya kijiji kinavyotisha!

Kulwa Magwa

CHOO cha ofisi ya serikali ya kijiji cha Magalata, wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, kiko katika hali mbaya kiasi kwamba mtu kukitumia lazima uvae ‘miwani ya mbao’.

Choo hicho kilichojengwa nyuma ya ofisi hiyo, hakina paa huku matofauli yaliyotumika kukijenga yakiwa yamemomonyolewa na mvua.

Kutokana na hali hiyo, mtu anapojisaidia ndani ya choo hicho ni rahisi kuonekana akifanya ‘vitu vyake’.

chooni-ukuta

Choo cha ofisi ya kijiji cha Magalata, wilaya ya Kishapu

Ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Jiyenze Ng’wandu, anasema choo hicho ambacho kilijengwa siku nyingi, kimeharibika sana lakini kinaendelea kutumiwa na wananchi.

Ingawa Ng’wandu anasema hakumbuki kilijengwa lini, ila matofali ya kuchoma yaliyotumiwa kujengea yanaonyesha kwamba kimekuwepo miaka mingi na kwamba, kumomonyoka kwa matofali hayo ni ishara kwamba kimedumu muda mrefu.

shimo-lilivyo

Hivi ndivyo kilivyo ndani

“Sikumbuki hasa lini tulikijenga, lakini cha siku nyingi ila kama umeingia ndani umeona mwenyewe, “anasema mtendaji huyo.

Hata hivyo, Ng’wandu anasema kwa sasa wanaendelea kukitumia licha ya kwamba kinahatarisha maisha ya watumiaji kwa kuwa hata ndani kuna matundu mengi yaliyoko kando ya shimo lenyewe.

Ujenzi wa choo hicho unasubiri msimu wa mvua umalizike, ambapo kwa Mwenyekiti wa kijiji hicho, Bulugu Mipawa, anasema kitajengwa sambamba na jengo la ofisi ya serikali ya kijiji.

Kaimu Ofisa Afya wa wilaya ya Kishapu, Daniel Madaha, anasema ofisi yake haina taarifa za ubovu wa choo hicho, lakini kwa nyakati tofauti mwaka jana, walizifungia zahanati tatu wilayani humo kutokana na kutokuwa na vyoo.

Madaha anasema kati ya Julai na Septemba, walizifunga zahanati za vijiji vya Ilebelebe, Kinampanda na Beledi ambazo zilifungwa kwa kutokuwa na vyoo na uchafu wa mazingira.

“Tutafuatilia kujua kwa nini choo chao kibovu na tutachukua hatua wakati muafaka,” anasema Madaha.  

2 Comments
  • Mh. Hapo mbona sioni matofali ya kuchoma? Hayo ni matofali ya kuchoma au matofali ya tope?

    Halafu huyo mtendaji anasema hakumbuki tulikijenga lini, alikuwepo au hakuwepo.

    Nice work.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *