DAR: Magufuli ampongeza Makonda kwa ziara za kuwafikia wananchi na kutatua kero

Jamii Africa
Rais Magufuli leo amepongeza ziara anazofanya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda za kuwafuata wananchi na kusikiliza kero zinazowakabili wananchi hao 'wanyonge' na kutoa suluhisho papo hapo.
 
Amempongeza kwa njia ya simu baada ya kupigiwa na Makonda akiwa katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi wa Ubungo eneo la Mbezi.
 
makonda_ziarani
 
Katika simu hiyo, Rais Magufuli amedai kuwa viongozi wengi wanajifungia kwenye ofisi zao na hawafanyi ziara za kusikiliza kero zinazowakabili wananchi wanaowaongoza. Amesema wananchi wana kero nyingi zinazohitaji viongozi kuwafikia na kuzitambua kero hizo ili waweze kuzitatua.
 
Amewataka Wakuu wengine wa Mikoa nchini kuiga mfano wa Paul Makonda kwa kuwatembelea wananchi na kusikiliza kero zao. Amemhakikishia Makonda kuwa anamuunga mkono kwa asilimia 100.
 
Aidha, Rais alifafanua kuhusu wananchi waliovunjiwa makazi yao eneo la Ubungo ili kupisha barabara, na kuwambia hawatolipwa fidia kwa sababu walijenga kwenye hifadhi ya barabara. Amewataka wananchi hao kufuata sheria; wasijenge kwenye hifadhi ya barabara.
 
Amesema kuwa bomoabomoa itaendelea Ubungo kwa wale waliojenga kwenye hifadhi ya barabara kwa sababu Serikali imeshapata kiasi cha shilingi Bilioni 67 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya juu yenye ghorofa tatu. Amesisitiza kuwa wananchi wanaoona kuwa wameonewa na ubomoaji waende Mahakamani wakadai haki yao.
 
https://youtu.be/PyulmnW7Q-Q
 
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amegusia pia kuhusu jengo la TANESCO lililopo kwenye hifadhi ya barabara kuwa na lenyewe muda ukifika litabomolewa ili kupisha ujenzi na upanuzi wa barabara.
 
Mjadala kuhusiana na simu iliyopigwa na Rais Magufuli kwa Mkuu huyo wa mkoa unaendelea katika JamiiForums kupitia mnakasha huu.
Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *