Digiti sawa, zi wapi chaneli tano muhimu?

Michael Dalali

Wahenga walinena; “Ahadi ni deni”. Katika mchakato wa kuingia kwenye mfumo wa kurusha matangazo kwa njia ya digiti toka mfumo wa analojia, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano iliwaahidi watanzania; wataendelea kupata fursa ya kutizama chaneli za ndani. Iliahidi ving’amuzi vingalirusha bure chaneli tano muhimu za ndani zisizo za kulipia ambazo ni; ITV, Channel Ten, TBC1, EATV na StarTv.

Miezi miwili mpaka sasa toka kuingia katika mfumo wa digiti ambapo siyo ving’amuzi vyote vinarusha chaneli tano muhimu kama ahadi na uthibitisho uliotolewa.

digital-tanzania

Ifahamike kuwa, hakukuwa na muongozo wa king’amuzi gani mwananchi anapaswa anunue ambao ulitolewa hapo awali ili kumhakikishia mlaji kupata huduma bora na hasa kupata kuona chaneli muhimu za ndani. Ila tu kila mwananchi wenye kuhitaji wa kupata matangazo ya luninga alihamasishwa kununua king’amuzi ili aweze kupokea matangazo yaliyoanza kurushwa kwa mfumo wa digiti tofauti na mfumo wa analojia ambapo haikuwalazimu kuwa na king’amuzi.

Ni kweli, makampuni binafsi ndiyo yamekuwa vinara kwa muda mrefu hata kabla ya kuingia katika mfumo wa digiti yamekuwa yakiendesha biashara ya kurusha matangazo kwa njia hiyo kwa kutumia ving’amuzi. Asilimia kubwa ni makampuni ya kigeni.

Hata nchi ilipoingia katika mfumo wa digiti, na hivyo hitaji la kutumia ving’amuzi kukua bado tegemezi la huduma ya kupokea matangazo kutumia ving’amuzi imekuwa chini ya makampuni binafsi.

Ni kampuni moja tu ambayo serikali ina hisa. Kampuni ya Star Times International Communication yenye king’amuzi chao cha StarTimes ambapo serikali kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) lina hisa asilimia 35 huku wawekezaji toka China wakiwa na asilimia 65.

Suala la mkataba baina ya kampuni ya Star International Communication na Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) na hasa afya na ustawi wa Shirika la TBC ni suala pana ambalo linastahili makala ya kujitegemea tofauti na hii.

Tukiachilia mbali ubora duni wa baadhi ya ving’amuzi katika kurusha matangazo yake ambao wateja wengi wameshaonyesha kutorishishwa, suala la kupata matangazo toka chaneli za ndani limekuwa ndoto kwa ving’amuzi vingi nchini.

Ni makampuni yasiyozidi matatu yenye kutoa huduma kupitia ving’amuzi ambao angalau kidogo wamemudu kutoa huduma ya chaneli za ndani hususan zile tano muhimu.

Licha ya kumudu kurusha matangazo ya chaneli muhimu tano za ndani makampuni hayo pia yameungana na makampuni mengine kuenenda kinyume na ahadi ya mamlaka ya TCRA kuwa huduma ya chaneli tano muhimu zinapaswa kutolewa bure hivyo hata kama mteja hatomudu kulipia gharama ya kupokea matangazo kwa mwezi husika aweze kuendelea kutizama chaneli tano muhimu. Hili nalo linakiukwa.

Katika mazingira hayo, wananchi ambao wamekuwa wakipambana kuhakikisha wanapata huduma ya taarifa za ndani wamekuwa wakilazimika kununua na kuvigharamia ving’amuzi zaidi kimoja. Hili halikubaliki!

Suluhu kama hii ni suluhu ya mtu mmoja mmoja, si suluhu ya kijumuiya kwa manufaa ya wengi. Si kila mwananchi ambaye anaweza kumudu kununua na kugharamia ving’amuzi zaidi ya kimoja. Hivyo ni muhimu sana kuhakikisha kila raia analindwa.

Hatupaswi kuruhusu taifa kuendelea kuacha raia watafute suluhu ya mtu mmoja mmoja kwani ndiyo inayoligawa na kuligharimu Taifa mpaka sasa.

 Tumeshuhudia pale ambapo baadhi ya wananchi walianza kuwa na mashaka na ubora wa elimu inayotolewa na shule za umma wamekuwa wakiwapeleka vijana wao katika shule binafsi huku shule za umma zikizidi kudidimia katika uduni na hali mbaya ya kimazingira ya kielimu. Zao la hali hiyo ni pamoja na ufaulu duni hasa katika shule nyingi za umma!

Suluhu binafsi inaweza kuonekana pia katika nyanja nyingine nyingi kama vile mazingira mabaya ya huduma za usafiri hususan katika miji na kila mwananchi mwenye uwezo kukimbilia kutatua kwa kuwa na usafiri binafsi huku ule usafiri wa umma kuzidi kuwa katika mazingira duni mathalani kubeba abiria wengi sana kuliko inavyopaswa..

Mifano katika sekta ipo mingi sana, iwe afya, nishati ya umeme, maji nk kote kuna uduni na mfumo umeacha wananchi watafute suluhu yao binafsi na si suluhu ya kimfumo mzima.

Miongoni mwa majukumu ya mamlaka mbalimbali kama ilivyo kwa TCRA ni kusimamia na kuratibu shughuli nzima za sekta husika. Hivyo, kwa TCRA kusimamia suala la kurusha na kupokea matangazo kutoka kwa kampuni kwenda kwa wananchi ni miongoni mwao.

Ni kama vile mamlaka ya EWURA inavyosimamia na kuratibu masuala mazima ya nishati na maji. Hivyo kuweza kusimamia mathalani bei za nishati ya mafuta na kuwasimamia ipasavyo wafanyabiashara.

Wananchi wengi kwa nyakati tofauti wamekuwa wakihoji, iwapi haki yao ya kupata taarifa inazingatiwa? Ni kwanini mamlaka na taasisi za kiserikali husika zinashindwa kuhakikisha kila mtanzania anamudu kuona hasa chaneli tano muhimu kama vile ahadi ilivyotolewa?.

Licha ya mchakato mzima wa kuingia katika mfumo wa digiti kuwanyima haki wananchi kupata taarifa lakini pia kutokuweza kusimamia wafanyabiashara na makampuni husika ambayo yanatoa huduma za kurusha matangazo kwa wananchi imeshtusha wengi.

Ikumbukwe, suala la kupata habari na kusambaza habari ni haki ya kila raia kikatiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa mujibu wa ibara ya 18 (b); “kila mtu anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila kujali mipaka ya nchi” lakini vile vile kipengele 18 (d) “kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii”.

Lakini jukumu hili pana la kuhakikisha haki kwa wananchi linawakumba pia wadau wengine mathalani baraza la walaji la sekta husika. Mabaraza ya walaji yanapaswa kuhakikisha walaji (wananchi) wanapata huduma stahiki na kwa ubora.

Mpaka sasa hakuna mikutano ya mara kwa mara kusikiliza wananchi “public hearings” ambayo ni moja ya njia za ufanyaji kazi wa mabaraza haya kupata mrejesho wa wananchi katika upatikanajihuduma.

Katika kipindi hiki cha nguvu ya soko huria ambapo mikono ya serikali inaondoka katika uchumi wa soko suluhu na matumaini ya wananchi daima imewekwa katika mabaraza. Mabaraza yanapaswa kuwa watetezi wakuu wa walaji. Ndiyo mantiki kuu hasa ya wito wa aliyekuwa rais wa awamu ya tatu wa Tanzania yaani; “tunaondoa mikono ya serikali kwenye uchumi wa soko lakini hatuondoi macho ya serikali”.

Na ndiyo hata hofu ya baadhi ya wananchi juu hasa ya hatari ya mazingira ambapo mabaraza ya walaji yakiwa yana hisiwa kuenenda kama vile yapo katika ndoa na watoa huduma na wadhibiti, daima walaji ndiyo wanaoumia kutokana na hali hiyo.

Katika hali ya mabadiliko ya kasi ya sayansi na teknolojia hususan upashanaji wa habari kwa njia ya TEHAMA, bado pia mabaraza hayajachukua fursa hiyo kukusanya maoni na mrejesho wa kutosha wa wananchi juu ya maoni yao katika utolewaji wa huduma mathalani hii ya digiti kwa kupitia ving’amuzi. Wananchi wengi wamekuwa wakionyesha kutokuridhishwa kwao huku madai hayo yakielea hewani bila hatua madhubuti kuonekana zinachukuliwa.

Katika nchi nyingi zilizopiga hatua hasa katika kusimamia na kupigania haki za raia wao, mabaraza na watendaji wakuu wa mabaraza mathalani wenyeviti wananguvu sana katika jamii zaidi au sawa hata na wanasiasa.

Lazima wananchi waamke kudai haki yao ya msingi ya kupata taarifa, kwani kutokupata taarifa kunarudisha nyuma kwa kiasi kikubwa juhudi zote za kimaendeleo. Na ndiyo maana hata kuna usemi wa; “information is power”! (yaani; taarifa ni nguvu).

Na ndiyo maana hata katika mapinduzi ya serikali za nchi, vituo vya habari ni miongoni mwa sehemu muhimu sana ambazo wahusika wa mapinduzi huvilenga!

Kwa hivyo basi, endapo kwa makusudi au kwa bahati mbaya na kuendelea kuachwa kwa hali ya kutokuwa na fursa kwa wananchi wengi kutokupata taarifa kwa wananchi ni kudhibiti nguvu ya wananchi. Ni  njia na mbinu moja wapo ya kuwadhibiti.

Tumefikia kuwa na Taifa ambalo wananchi wake wamegawanyika. Wapo wananchi ambao hawamudu kabisa kupata habari kutokana na kutokumudu gharama za manunuzi na uendeshaji wa ving’amuzi. Lakini pia wapo wananchi ambao kutokana na udhaifu wa kimfumo wakosa kuona chaneli za ndani muhimu si kwamba hawana king’amuzi au wameshindwa kuvilipia bali huduma ya chaneli tano muhimu hazimo katika ving’amuzi ambavyo wanatumia. Wamekuwa watanzania ambao wanalazimika kutizama chaneli za nje zenye habari za mataifa mengine ndani ya nchi yao kuliko kutizama chaneli za ndani ili kupata habari za ndani ya nchi.

Ni wakati sasa wa kuchukua hatua. Ni wakati sasa kwa kila raia mmoja mmoja na kwa kuungana kuhakikisha tunawasilisha kutoridhika kwetu na namna ya mifumo ya upashanaji habari inaendeshwa nchini katika mamlaka husika kama vile Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), katika baraza la walaji la sayansi na teknolojia na katika wizara husika. Ni jukumu na wajibu wa kila raia kuhakikisha anaiwajibisha serikali pale haienendi katika misingi ya haki.

Kwa hatua na matendo yetu ndipo tutamudu kuonyesha utofauti kati ya “watawaliwa” (subjects) na “raia” (citizens) katika Taifa letu. Hayati Bob Marley alipata kuimba; “how long shall we stand a side and look…while injustice prevails” (Ni mpaka lini tunaendelea kusimama kando na kutizama….vitendo vya uvunjifu wa haki vikimea).

Wakati ni sasa!

10 Comments
  • Ki ukweli, wananchi wamebweteka na ni waoga hata kudai haki zao, nahisi ni ujinga uliokomaa na umasikini uliokithiri. Mimi toka huu uanze sijaangalia Television za kwetu nacheki Mpira tena kwakulipia ktk Dstv.

    Maisha yamekua si maisha kutokana na habari hakuna kabisa na nchi imekua dolo. Ni muda wa kuamka na kudai vilivyo haki yetu mana haki haipatikani kwa kukaa tu na kumuomba Mungu, lazima ufaiti na Mungu atakuongoza.

  • Ni kweli kabisa kaka serikali yetu imekuwa gumuzo kubwa la matatizo mengi yanayotukumba sisi wananchi,hivyo serikali yetu ni vyema ikasikiliza maoni na kuweza kutatua matatizo ya wananchi pale inapowezekana na kutekelezeka.

    Pia ni vyema serikali yetu ikatekeleza ahadi zake kwa wananchi kwani ahadi ni deni.Ni yangu matumaini kuwa serikali yetu itayasikiliza maoni na maombi ya wananchi na kuyafanyia kazi.

  • hivi ving’amuzi serikali imevileta ili kulirudisha taifa nyuma kimaendeleo kwani ingekuwa na nia thabiti ingewekeza hisa za kutosha ili kumiliki % kubwa ya kimamlaka na kuonyesha chanel zote muhimu za ndani ili kumwezesha kila mtz kupata habari kwa wakati anaotaka yeye.

  • haya mambo yamekuwa siasa tupu hakuna lolote na serikal inajua taifa changa wakat linaelekea umri wa kustaafu aibu

  • Tatizo kubwa tulilo nalo watanzania ni ubinafsi sisi kwa sisi wenyewe hatupendani. Na ni sababu kubwa inayofanya mpaka sasa usione chochote sbb wachache wanavyo turio wengi hatuna

  • tupo pamoja marafiki nchi ishauzwa wanao miliki hizo chanel ni wakubwa wa nchi watanzania tuamke kuburuzwa sasa basi

  • Kwakweli inaumiza sana zaidi pale umenunua kisha chanel zinakata kata.ususan arusha.

  • Thanks Michael kwa kuvunja ukimya! Kuna tatizo gani watanzania? tulivyoambiwa na TCRA haikuwa hivyo na tumekaa tu tupoje?.Hata hivyo vin'gamuzi vya star times (ambapo TBC wanashare) havina ubora.Hivi tutachoka lini kupata huduma mbovu kutoka kwa watoa huduma wa nchi hii? mbona tunaburuzwa na tunaangalia tu? Kiwango chetu cha mwisho cha uvumilivu ni kipi?

  • Hakika nawashukuru sana nyote kwa pamoja kwa kutoa maoni yenu. Maneno yenu ni msukumo na tija chanya katika kuendeleza mapambano ya kuhakikisha sauti za wanyonge zinasikika kupitia kalamu na fikra za kiuandishi kusanifu maisha halisi ya mtanzania ambaye yu katika mapambano ya kupata maisha yenye ustawi na neema.

     

    Tusiache kuandika na kusoma! Tutashinda hakika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *