Elimu ni haki ya msingi kwa kila mtoto, lakini kutokana na changamoto mbalimbali wapo watoto ambao hawakupata fursa ya kupata elimu ya msingi katika umri unaostahili.
Kwa kuzingatia kuwa elimu ni silaha muhimu kumkomboa mtoto kifikra, serikali ilianzisha programu ya Mpango wa Elimu ya Msingi Kwa Watoto Walioikosa (MEMKWA) ili kuwawezesha watoto kupata elimu nje ya mfumo rasmi.
Programu ya MEMKWA ilianzishwa kwa majaribio kati ya mwaka 1999 hadi 2002 katika wilaya za Musoma Vijijini, Kisarawe, Ngara, Masasi na Songea Vijijini. Programu hiyo ilipoonyesha mafanikio, mwaka 2003 serikali ilianzisha madarasa ya MEMKWA katika shule za msingi nchi nzima.
Elimu ya MEMKWA imegawanyika katika makundi rika mawili, ambapo kundi rika la kwanza hujumuisha watoto walio na umri kati ya miaka 10-13. Watoto hao husoma kwa miaka 2 hadi 4 kisha huruhusiwa kufanya mtihani wa darasa la nne (IV). Kundi rika la pili hujumuisha vijana walio na umri kati ya miaka 14 hadi 18.
Wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo yao huruhusiwa kujiunga katika elimu ya mfumo rasmi na kufanya mtihani wa darasa la saba, wakifaulu huendelea na elimu ya sekondari.
Dhima ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 inajikita kuinua ubora wa elimu na mafunzo na kuweka mifumo na taratibu zitakazowezesha kupata idadi kubwa ya Watanzania walioelimika na wanaopenda kujielimisha zaidi ili waweze kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa letu.
Licha ya ongezeko kubwa la watoto wanaoandikishwa darasa la kwanza, bado idadi ya watoto walio katika elimu ya mfumo huu usio rasmi yaani MEMKWA ni kubwa ikilinganishwa na msisitizo wa serikali wa kuifanya elimu ya msingi kuwa bure na ya lazima.
Takwimu za Kituo Huru cha Serikali za mwaka 2016 zinaonyesha kuwa kulikuwa na wanafunzi 69,492 wa MEMKWA kundi rika la kwanza nchi nzima.
Fikra Pevu imebaini mikoa 10 ambayo ilikuwa na wanafunzi wengi wa MEMKWA kwa mwaka 2016. Mikoa hiyo ni Geita, Kagera, Kigoma, Morogoro, Dar es salaam, Mwanza, Tabora, Rukwa, Tanga na Singida. Mikoa hiyo ina wanafunzi kati ya 2,927 na 8,732.
Mikoa hiyo 10 iliyotajwa kuwa na wanafunzi wengi bado ina tofauti kubwa ya idadi ya wanafunzi kutoka mkoa mmoja hadi mwingine. Pia kanda ya Ziwa inaonekana kuwa na wanafunzi wengi zaidi ikilinganishwa na kanda nyingine za Kusini na Mashariki.
Mathalani mikoa ya Geita, Kagera na Mwanza ilikuwa na wanafunzi 18,163. Tofauti ya wanafunzi kati ya mkoa ya Geita na Kagera ni wanafunzi 2,784 huku mkoa wa Geita ukiwa unaongoza kwa kuwa na wanafunzi wengi wa MEMKWA ambao ni wanafunzi 8,732 ukifuatiwa na Kagera ambao una wanafunzi 5,948.
Tofauti hiyo ya wanafunzi 2,784 ni pungufu kidogo ya idadi ya wanafunzi 2,927 waliopo mkoa wa Tanga ambao ni miongoni mwa mikoa 10 yenye wanafunzi wengi wa MEMKWA. Lakini idadi ya wanafunzi waliopo mikoa ya Tabora na Kigoma haitofautiani sana ikilinganishwa na mikoa mingine kama inavyoonyeshwa hapo juu kwenye kielelezo cha picha.
Pia tofauti hiyo inajitokeza kwa mkoa wa Iringa wenye wanafunzi wachache kabisa na Geita yenye wanafunzi wengi Tanzania Bara. Mkoa wa Iringa ulikuwa na wanafunzi 252 tu ikilinganishwa na Geita yenye wanafunzi 8,732.
Iringa inajumuishwa katika mikoa 10 kati ya 26 ambayo ilikuwa na wanafunzi wachache kabisa wa MEMKWA. Mikoa mingine ni Kilimanjaro, Simiyu, Songwe, Dodoma,Lindi, Mbeya, Manyara, Katavi na Njombe.
Mikoa hiyo 10 yenye wanafunzi wachache ilikuwa na jumla ya wanafunzi 10,907, ambapo ni juu kidogo ya mkoa mmoja wa Geita wenye wanafunzi 8,732. Licha ya Simiyu kuwa katika kanda moja na mazingira yanayofanana na Geita bado mkoa huo uko miongoni mwa mikoa yenye idadi ndogo ya wanafunzi.
Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ina wanafunzi wachache ambapo haitofautiani sana na mikoa ya Kanda ya Kaskazini hasa mikoa ya Kilimanjaro na Manyara. Ukitazama kwa makini kwa kila kanda kuna mikoa yenye idadi kubwa na ndogo ya wanafunzi wa MEMKWA.
Hali hii inaweza kuashiria utofauti uliopo katika uandikishaji wa watoto kwa darasa la kwanza na idadi ya wanafunzi ambao wanachelewa kuanza shule. Pia wapo wanafunzi wanaodondoka njiani na kushindwa kuendelea na masomo.
Changamoto Zilizopo
Wadau wa elimu wanasema maeneo ambayo yanaongoza kuwa na wanafunzi wengi wa MEMKWA, sababu ni kuwa baadhi ya wazazi wanakataa kuwaandikisha watoto wao shule wakiwa katika umri mdogo.
Wanatumia kigezo hicho kwa kudai kuwa baadhi ya shule ziko mbali na makazi wanayoishi, hivyo huwalazimu wanafunzi kutembea umbali mrefu kuzifuata shule na watoto wadogo hawawezi kufika huko shuleni kwa kuhofia usalama wao.
“Wazazi wengi wanakataa kuwapeleka watoto wao shule kwasababu shule ziko mbali, hivyo wanasubiri wakue na kufikia umri wa kujitegemea ndipo waanze kwenda shule” anasema Faustin Clement mkazi wa Geita.
Kauli hiyo inathibitishwa na Mwanachama wa shirika la HakiElimu, Profesa Suleman Sumra katika utafiti wake alioutoa katika Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) ambapo anasema;
“Ni wazi kwamba agizo la kuandikisha watoto kuanza shule wakiwa na umri wa miaka saba limepuuzwa. Kama ilivyokuwa siku za nyuma, wazazi wengi huwaona watoto hao bado wadogo na hivyo kuweka kipaumbele katika kuwaandikisha shule wenye umri mkubwa kwanza”, anafafanua zaidi,
“ Wazazi wengi wanashauri suala la umri liwe wazi kwa kuangalia mazingira na utamaduni wa watu. Baadhi ya sehemu, umbali wa ilipo shule kulinganisha na makazi ni mkubwa mno kuliko uwezo wa kutembea wa mtoto wa miaka saba”.
Kutokana na changamoto mbalimbali, hivyo zinawazuia watoto kuanza darasa la kwanza kwa wakati, elimu ya MEMKWA huwa njia pekee ya mtoto kuipata elimu ya msingi lakini sio wote wanaofanikiwa kuingia katika elimu hiyo.
Rafiki wa Elimu kutoka mkoa wa Mara, Juma Richard anasema elimu ya MEMKWA ni njia mojawapo ya kufuta ujinga kwa wanafunzi walioshindwa kuingia katika elimu ya mfumo rasmi. Anashauri kuwekwa kwa mipango endelevu ambayo itawawezesha watoto kupata elimu bila kikwazo chochote.
“Watanzania tunaiona elimu ya MEMKWA kama haina msaada kabisa kwetu lakini ifike mahali tukumbuke kwamba Mwalimu Nyerere alipigana kufa na kupona kuhakikisha tunafuta ujinga nchini na mbinu kubwa aliyotumia ni kuhakikisha waliokosa elimu wanapata elimu bila kujali umri wao na alifanikiwa kwa kiwango kikubwa sana”. Anasema Richard.
Matamko na Ripoti Mbalimbali
Ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ya mwaka 2015 inaonyesha kuwa takribani watoto Milioni 58 wameshindwa kujiunga na shule na milioni 100 kati yao wameshindwa kuhitimu elimu ya msingi duniani kote.
Tanzania bado ina idadi kubwa ya watoto ambao hawako shuleni na wanatakiwa kupatiwa elimu ili kujenga taifa la watu walioelimika.
Kwa mujibu wa takwimu za Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) za mwaka 2012 zinaonyesha kuwa Tanzania ina jumla ya vijana wa umri wa miaka 7-17 Milioni 3.5 waliopo nje ya shule, ambapo kati yao Milioni 2.5 wanahitaji elimu ya Sekondari na Milioni 1 wanahitaji Elimu ya msingi.
Mafanikio Ya MEMKWA
Kwa mwaka 2013 wanafunzi 4,170 wa MEMKWA walichaguliwa kujiunga darasa la tano huku wengine 1,576 waliofanya mtihani wa darasa la saba walijiunga na elimu ya sekondari mwaka 2012. Pia Serikali imeimarisha mafunzo kwa walimu wanaofundisha wanafunzi wa MEMKWA ili kupunguza idadi ya watoto wasiojua kusoma na kuandika.
"Vilevile wizara imeandaa Mwongozo wa Ufundishaji wa KKK (Kusoma, Kuandika na Kuhesabu) kwa watoto wanaosoma nje ya mfumo rasmi kwa lengo la kuwasaidia walimu watakaofundisha madarasa ya Elimu Nje ya Mfumo Rasmi". anasema Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Njalichako akiwa bungeni hivi karibuni.
Programu ya MEMKWA inapaswa kuimarishwa kwa kuongeza rasilimali watu na miundombinu ili kuhakikisha wanafunzi waliokosa elimu ya msingi wanapata fursa ya kusoma kama watoto wengine katika shule za msingi na sekondari.
Dira Maendeleo ya Taifa, 2025 (The Tanzania Development Vision) inalenga kuwa na taifa la watu wenye elimu ya kati na ya juu ili kuwa na watendaji kazi wenye uwezo wa kushughulikia kikamilifu changamoto za kimaendeleo.