Elimu yetu Tanzania: Suala la kujifunza na changamoto za utandawazi

Ramadhani Msoma

Poleni watanzania wenzangu kwa habari ya kusikitisha ya wahitimu wa Kidato cha Nne 2012 kuwa na ufaulu wa kusikitisha (zaidi ya 90% wamefeli kwa kupata div 4 au ziro). Kwa mzalendo yeyote lazima atajihoji ni wapi tunaelekea kama Taifa!? Kuna sehemu tumekosea, fuatana nami katika uchambuzi huu na nayakaribisha maoni yako…

Tafiti nyingi zimeonyesha kuwa hali si shwari katika mfumo rasmi wa kupata elimu hasa kwenye suala muhimu la ubora. Ingawa nafasi za kusoma katika shule zetu za msingi, sekondari na vyuoni zimeongezeka jambo ambalo limetoa wigo mpana wa kuongezeka kwa uandikishwaji wa vijana wengi zaidi, lakini bado utata upo katika ubora wa elimu inayotolewa. Hii ni kwa elimu itolewayo na taasisi za umma na zile za binafsi. Ndiyo, hata katika taasisi za elimu za binafsi ambazo hivi karibuni zimekuwa zikipapatikiwa sana hususan na baadhi ya watanzania wenye uwezo bado viwango vya ufaulu na ubora wake ni duni!

Tafiti iliyoendeshwa na shirika lisilo la kiserikali la UWEZO mnamo mwaka 2012 ilionyesha kuna tofauti ndogo sana ya ufaulu kati ya shule binafsi za Tanzania na zile za umma za nchini Kenya, ikiwa kiwango cha ufaulu wa asilimia 71 na 75! Hii inamaanisha, shule binafsi za nchini Tanzania zinautofauti ndogo sana kwa kiwango cha ufaulu (na ubora) kulinganisha na zile shule za umma kwa nchini Kenya licha ya kuwa kwa upande wa Tanzania, wazazi na walezi wanawajibika kulipa gharama kubwa sana wakati nchini Kenya katika shule za umma gharama ni nafuu. Hivyo kumbe inawezekana kabisa kuwa na shule za umma za gharama nafuu zenye elimu bora.

Kazi kubwa bado inatakiwa kufanyika ili watoto walio kwenye shule na taasisi mbalimbali za elimu nchini wajifunze na kuelimika kweli. Katika hili, serikali inapaswa kulipa suala la ubora wa elimu umuhimu mkubwa. Ukiacha hiyo ngazi ya kielimu, kuna elimu inayotolewa na vyuo vya ufundi kama VETA ambayo nayo inabidi iwekewe mkazo na isionekane ni elimu ya  wanaoshindwa kuingia kidato cha kwanza au kuendelea na kidato cha tano.

Pia na kuna elimu inayotolewa na vyuo vyetu vya elimu ya juu na vyuo vingine ambayo vinaanzishwa siku hizi kwa kasi na wingi ikiwa ni jitihada njema za kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu ya juu lakini  tunahitaji usimamizi wa hali ya juu katika ubora.

Kimsingi elimu ninayoieelezea ni iliyo katika mfumo rasmi na inategemea mitaala. Kufanya vizuri katika hatua moja kunakuwezesha kwenda kwenye hatua nyingine angalau kuna viwango na vigezo vimewekwa ili kufuzu. Licha ya matatizo yaliyopo kwenye mfumo rasmi wa elimu yetu nchini ambapo tunaweza kutupia mzigo wa lawama serikali na taasisi zinazotoa au kusimamia utoaji wa elimu hiyo lakini je tumeshajihoji na kujitathmini kuhusu tabia ya kusoma na kujielimisha sisi wenyewe? Kupeana msukumo katika kuelimika au elimu tunayoipata kuhakikisha inatukomboa?

Kwenye mazingira haya ya utandawazi  na kama pia tumekubali kuwa sekta binafsi na soko huria ndo itakayosukuma maendeleo ya nchi, hatuna budi kubadilika watanzania na hasa vijana kujielimisha wenyewe kwenye mambo mbalimbali iwe kwenye teknolojia, siasa (watu wengi hufikiri siasa ni ya wanasiasa lakini wakumbuke wote tunaathirika na maamuzi ya kisiasa. Rais wa zamani wa Ufaransa Charles de Gaulle alisema; “I have come to the conclusion that politics are too serious  matter to be left to the politicians” Tafsiri yangu ikiwa; nimefikia hitimisho kwamba siasa ni jambo la msingi mno kuachiwa wanasiasa ) pia kwenye uchumi, michezo na nyanja mbalimbali.

Kwa mfumo wa uchumi wa dunia ya sasa milango imefunguka kiasi kwamba muingiliano baina ya watu wa mataifa umekuwa mkubwa na maisha ya mwanadamu yamekuwa ya ushindani mkubwa wa rasilimali ambazo hata kama zipo kwenye mipaka yetu lakini watu wengine duniani wanazitamani. Ili tuwe  washindani duniani hatuna budi kuuelewa ulimwengu wa sasa na mifumo yake nje ndani hatuna jinsi.

Ni muhimu kuwa na serikali na taasisi zenye nguvu sio tu nguvu ya serikali dhidi ya raia wake kwa maana ya kubinya haki za raia wake, au kutawanya maandamo, bali inayoongozwa na watu wanaoelewa mazingira ya sasa ya dunia hii ya ushindani ya jinsi kama taifa linavyoweza kushiriki na kupata faida kwenye utandawazi. Tuna jukumu la kuhakikisha tunakuwa na serikali ya aina hiyo. Serikali kama hiyo inaweza kupatikana tu kutokana na aina ya jamii tuliyo nayo, ndiyo maana ni muhimu sana kuwa na jamii iliyopata elimu bora katika mazingira rasmi na kwa jitihada binafsi za kujielimisha. Tukumbuke wengi tunaowalalamikia kwa utendaji mbovu kwenye serikali zetu na sekta binafsi wanatoka miongoni mwetu!

Udadisi binafsi wa kujifunza ni mdogo sana miongozi mwa watanzania, achilia mbali ongezeko la fursa za  kusoma kutoendana na kuongezeka kwa ubora watanzania walioelimika inashabiri ukweli kuwa wengi wa watanzania wanaopitia mifumo ya kielimu hukosa muda wa kujifunza kwa mfano wa kujisomea wenyewe hasa baada ya kutoka kwenye mfumo rasmi wa elimu. Kwa hiyo kuna mchanganyiko wa hatari yaani; utolewaji wa elimu isiyo na ubora  sambamba na uvivu wa kujifunza miongoni mwa wanajamii.

Waajiri wengi hususan kwenye zama hizi za ushindani wamekuwa wanalalamikia viwango duni vya watu wanaozalishwa kwenye shule na vyuo vyetu. Kwenye ripoti ya chama cha waajiri Tanzania (Association of Tanzania Employers) na wadau wengine kama shirika la kazi duniani (ILO) inayoitwa Business Agenda-Tanzania  ya mwaka 2011 inasema; kuna upungufu mkubwa wa ujuzi kwenye sekta binafsi kwenye ngazi zote .Ufanisi umekuwa mdogo kulinganisha na jirani zetu kama  Kenya na nchi nyingine zinazoendelea kama China na India. Ripoti hiyo pia inabainisha kwamba ili tutoke hapo tulipokwama ni lazima tuongeze ubora kwenye elimu inayotolewa kwenye shule za msingi, sekondari, vyuo vya ufundi na elimu ya juu.

Shida kubwa ya elimu yetu rasmi ni kwamba haitufundishi kujifunza. Hata waliopo kwenye vyuo vikuu hawana ari ya kujifunza zaidi ya kusoma kwa ajili ya kufaulu mitihani na majaribio. Mtu anaweza kumaliza elimu ya juu bila kugusa kitabu! Ni jambo la hatari sana hili. Tumepunguza na kuhalalisha suala zito la kujielimisha mpaka kwenye kupata vyeti tu. Huo ndio umekuwa msukumo wa wengi, kupata vyeti kumekuwa  motisha mashuleni na vyuoni kunakowafanya watu wakariri chochote.

Tumefikia uthubutu hata wa kununua au kulipa fedha kuandikiwa tasnifu (dissertation) alimradi tuweze kupata shahada badala ya kufanya utafiti kwa tija ya kuibadili, kuifahamisha na kuikomboa jamii yetu!

Uchumi wa kisasa unahitaji watu walioelimika vyema na walio tayari kuendelea kujielimisha hata baada ya kutoka shuleni na vyuoni.  Mwandishi Ruchir Sharma kwenye kitabu chake kinachoitwa;  Breakout Nations in pursuit of the next economic miracles  anatoa mfano wa kampuni ya vifaa vya kompyuta ya intel mwaka 2010 ilivyokwama.Kampuni hiyo ilitaka kuwekeza kwa kufungua kiwanda cha kutengeneza vifaa vya kompyuta nchini Vietnam kwa kiasi cha dola za marekani bilioni moja, na walihitaji wafanyakazi 4,000 wenye ujuzi wa kawaida wa ufundi  na wenye kujua kiingereza kidogo lakini walipowasaili watu 1,200 wa kwanza walipata watu wenye sifa hizo wanne tu! Mpaka sasa wameshindwa kufikia lengo la kupata wafanyakazi wenye ujuzi wanaoutaka kwa idadi hiyo ya 4,000, na labda mpaka mwaka 2016 ndio watafikia hiyo idadi na hiyo ni baada ya kuanza kuwafunza watu wao wenyewe. Hapa kuna funzo muhimu sana hasa nyakati hizi ambapo neema za rasilimali kama gesi, mafuta na madini zinaendelea kugunduliwa nchini mwetu.

Tuwekeze vizuri kwenye elimu rasmi. Watu wafundishwe kujifunza. Elimu iwakomboe, tujue kujifunza ni zoezi la kudumu. Lakini kama tunataka tu kukimbia ovyo ovyo na tusijue tuendapo basi njia yoyote itatufaa.

3 Comments
  • HAYA NI MATOKEO YA KILE TULICHOKIPANDA BAADA YA KUFUTA ULE MTIHANI WA MCHUJO WA KIDATO CHA PILI.

  • Kwa  kweli  kuna  sababu  nyingi  sana  zinazohusiana  na  matokeo  mabaya  ya  kidato  cha  nne.  Baadhi  ya  sababu  hizo  kwa  ufupi  ni;

    1.kukosekana  kwa  motisha  kwa  walimu.

    2.upungufu  wa  vitabu  na  vifaa  vya  maabara.

    3.utandawazi  ambao  umechukua  sehemu  kubwa  ya  ubongo  wa  wanafunzi  na  hivyo  kupuuza  masomo.

    4.wazazi  kutoshirikiana  kwa  ukaribu  na  walimu katika usimamizi  wa  wanafunzi.

    5.uwezo  binafsi  wa  wanafunzi  kuwa  mdogo  kwani  wengine  huchukuliwa  wakiwa  na  alama  za  chini sana  katika  kuingia  kidato  cha  kwanza.

    6.uwezo  mdogo  kwa  baadhi  ya walimu.

    7.ualimu kuwa  ni kimbilio  la  baadhi ya wakosa  ajira  ambao  hawapo tayari  kufundisha ila  wapo  tayari  kwa  mshahara.

    8.baadhi  ya  viongozi wa nchi kuona suala la elimu si muhimu ila siasa ndiyo  muhimu kwao hivyo  nguvu  huelekezwa katika siasa na hivyo  elimu kutokuendeshwa kitaalamu bali  kuongonzwa kisiasa.   

  • Kwa nini katika kujadili hili watu wengi wanaangalia nini sababu ya tatizo pasipo kutoa jibu sahihi ya nini kifanyike, nimefuatilia comment nyingi za viongozi, wanasiasa na baadhi ya wananchi wanatoa sababu tu, nini sasa tunatakiwa kufanya kama taifa,tuanzie wapi na tuishie wapi?.

    Vilevile tuangalie maeneo haya je tuko na ufanisi kiasi gani? 1. Je tunamuandaaje mwalimu aliye bora? 2. Je wazazi katika familia wanamuandaa mtoto kisayansi kuanzia utotoni mpaka anapofikisha umri wa miaka 18? 3. je vipi mazingira ya kufundishia na kujifunzia yanaendana na mwanafunzi pamoja na mwalimu wake na mtaala husika pia? 4. Vipi vyomba vinavyohusika na uboreshaji wa elimu vinawezeshwa ipasavyo na vinawajibika ipasavyo mfano idara ya Ukaguzi wa shule nk. Mbali na kukosa motisha lakini pia walimu siku hizi hawataki kuwajibika madarasani na ukizingatia walimu wenyewe ndiyo hivyo tena wameenda kusomea ualimu kama plan B baada ya Plan A kushindikana au ndiyo wale waliopata Daraja la IV na pointi 26-30.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *