Ni ukweli usiopingika kuwa wengi wetu hatujui ni jinsi gani tujieleze kwa daktari ili tuweze kupata tiba sahii na kwa wakati. Pia, kuna wakati tunashangazwa na baadhi ya maswali tunayoulizwa na daktari ambayo kuna muda yanaonekana kuwa hayana uhusiano na tatizo linalotusumbua.
Nimeona ni vyema nikaelezea ni taarifa zipi muhimu za kumuelezea daktari ili aweze kufikia hitimisho la kubashiri tatizo lako.
1: Tatizo Kuu (Main complaint)
Hapa unatakiwa kumueleza daktari ni kipi kinakusumbua mpaka ukaamua kumuona. Ni muhimu sana kueleza tatizo hili limechukua muda gani. Mfano miaka kadhaa, miezi kadhaa, wiki kadhaa au siku kadhaa au limekuwa likijirudia mara kwa mara kwa muda flani.
Kwa mfano: Kukohoa kwa zaidi ya wiki mbili kunaweza kusababishwa na Kifua Kikuu, Kansa au ugonjwa wa Moyo; Kukohoa kwa wiki moja yaweza kuashiria ni homa ya mapafu; Kukohoa kwa masaa kadhaa yaweza kuwa umepaliwa na chakula; Kukohoa mara kwa mara yaweza kuwa ni pumu n.k
2: Historia ya tatizo
Hapa unatakiwa kueleza tatizo lako limeanza vipi, linatokea wakati gani (usiku, mchana au muda wote) linahusiana na nini mfano kukohoa na kutapika au tumbo kuuma na kuharisha. Pia, eleza kama tatizo lako linaongezeka au kupunguzwa na kitu flani mfano unakohoa sana unapolala chali au moyo unakwenda mbio unaposimama lakini unapata afadhali unapochuchumaa au kiungulia kinapungua unapomeza vidonge vya magnesium n.k
Kwa lugha fupi ya kitabibu, maelezo ya ugonjwa wako yatafuata acronym ya DOPARA (Duration, Onset, Periodicity, Associating factors, Relieving or Aggreviating factors).
3: Historia ya afya yako kwa ujumla
Hapa unatakiwa kujieleza kwa ujumla kuhusu afya yako toka uzaliwe. Je, umewahi kutibiwa kwa tatizo hilo hilo? Umewahi kulazwa hospitali kwa tatizo lolote? Umewahi kufanyiwa upasuaji? Usiogope kutaja hata kama ulitibiwa kwa dawa za kienyeji!
Pia, ni muhimu kueleza dawa au tiba zozote ulizowahi kupata miaka kadhaa nyuma au siku chache kabla ya kufika kwa daktari anayekuona muda huo. Mfano, tatizo lako kwa sasa ni mimba kutoka na hapo hapo ukawa na historia ya kutoa mimba kadhaa hapo ulipokuwa kigoli yaweza kuelezea kuwa shingo ya uzazi imelegea n.k!
Aidha, ni muhimu kumueleza daktari kuwa kuna baadhi ya dawa zinakuletea mzio (allergy).
4: Historia ya kifamilia
Kuna baadhi ya magonjwa yanasababishwa na mifumo ya maisha (lifestyle) yetu na pia kuna baadhi ya magonjwa ni ya kurithi hivyo ni muhimu kueleza masuala ya kifamilia kwa ujumla.
Mfano babu, baba, mama au bibi walikuwa na tatizo flani kuna uwezekano na wewe ukawa nalo.
Mtoto anaweza kuwa na tatizo la utapiamlo kisa mama ni mfanyakazi wa TBC na hivyo hapati muda wa kumnyonyesha au mume ni dereva wa magari ya mizigo ya kwenda Zambia na hivyo kamuambukiza mke wake magonjwa ya gono n.k
Haya ni baadhi ya maelezo muhimu yanayotakiwa kutolewa kwa daktari ili kufanikisha ugunduzi wa ugonjwa wa mteja aliyefika kupata huduma. Yanaweza kubadilika kidogo kulingana na mazingira ya mgonjwa au tatizo lakini huu ndio msingi wa kujieleza kwa daktari.
Baada ya kutoa maelezo haya, daktari anatakiwa kukufanyia uchunguzi wa mwili (physical examination) ili aweze kulinganisha na maelezo yako na baada ya hapo atakuandikia vipimo (investigations) ili kupata ugonjwa halisi unaokusumbua.
Kwa leo niishie hapa, tukutane wakati mwingine! Aksanteni.
Nimenufaika sana na maelezo yako Dr.
Asante sana.