FAMILIA ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, imekitabiria Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ushindi wa kishindo wa kuongoza nchi mwaka 2015.
Familia hiyo ya muasisi wa taifa imesema ukomo wa serikali ya CCM umefika ambapo inaamini Uchaguzi Mkuu wa urais ujao, CHADEMA itaibuka kidedea.
Kauli hiyo ya familia ya Mwalimu Nyerere, ilitolewa jana na mtoto wa tatu wa Baba wa Taifa, Magige Nyerere, akiwa mbele ya kaburi la Baba wa Taifa wakati viongozi wa CHADEMA Taifa walipozuru nyumbani kwa mwasisi huyo Butiama, Musoma, mkoani Mara, ambapo waliweka mashada katika kaburi hilo na Mama Maria kuongoza sala.
Alisema anaamini wapigakura mwaka 2015 watakuwa milioni 12 na kati ya hao, CHADEMA itapata kura milioni sita na CCM itaambulia kura milioni nne.
Kwa mujibu wa mwanafamilia huyo wa Baba wa Taifa kwa sasa nchi iko katika joto kubwa la kisiasa.
“Lazima tuseme ule ukweli uchaguzi mkuu uliopita CHADEMA haikuweza kuongoza dola, lakini mwaka 2015 wapigakura watakuwa milioni 12 na milioni sita zitaenda CHADEMA na milioni nne CCM.
“Hali ilivyo sasa, joto la kisiasa hapa nchini liko juu na wananchi wameonekana kufanya mageuzi ya kiuongozi,” alisema Magige Nyerere mbele ya mke wa Baba wa Taifa, Maria Nyerere.
Huku akimfananisha Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, na mdogo wake, Makongoro Nyerere, ambaye naye alikuwapo alisema, “Nakiri kuwa mimi ni CCM, lakini nafurahia kazi na siasa yenu…naomba uendelee hivyo na hata ukiwa bungeni kama kiongozi wa upinzani.”
Viongozi hao wa CHADEMA na msafara wao walizuru nyumbani kwa Nyerere majira ya saa 5:55 asubuhi kwa lengo la kumsalimia mjane wa Baba wa Taifa.
Kiongozi wa msafara huo, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, alimuomba Mama Maria kukiunga mkono chama hicho na kukiombea mema.
“Mama tumekuja kukusalimia na familia yako…CHADEMA tunaomba mtuombee na mtuunge mkono,” alisema Mbowe kisha Mama Maria kutikisa kichwa kuashiria kukubaliana na maelezo hayo.
Akitoa nasaha zake mbele ya kaburi la Nyerere, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema mchakato wa Nyerere kuwa Mtakatifu mwenye kheri bado haujakamilika, hivyo raia wawe na uvumilivu.
Alisema nchi ya Uganda imepiga hatua juu ya mchakato huo, hivyo hatuna budi kuwa wavumilivu.
Kuhusu maandamano ya CHADEMA nchi nzima, Magige Nyerere alisema,” Awali nilipatwa na wasiwasi mkubwa, lakini nimebaini kumbe ni maandamano mazuri; yaendelee.”
Hata hivyo, mtoto huyo wa Baba wa Taifa alisema maandamano hayo ni vema yakaendelea kwa amani, ili kufikisha ujumbe husika katika mamlaka husika.
Wakiwa wilayani Tarime jana Mbowe alimtaka Rais Kikwete kuacha mara moja kuwajaza hofu Watanzania juu ya kuwepo mipasuko ya kidini. Mbowe ambaye aliongoza maandamano makubwa kabla ya mkutano, alihoji sababu ya Rais Kikwete kushindwa kuwakamata na kuwasweka ndani wanaoleta chokochoko za kidini.
Viongozi hao wa CHADEMA kesho wataendelea na ziara yao katika mkoa wa Shinyanga kwa kufanya maandamano makubwa ya kuwashukuru wananchi kwa kuwapa kura na kuwataka wananchi wapinge hatua ya serikali ya kutaka kuilipa kampuni ya Dowans.
Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma na Janeth Josiah, Musoma – FUATILIA LINK HII
nashukuru nimejifunza kitu kupita makala hii.pia napenda kuwaunga mkono wanzilishi na wandaaji makala hii wananchi wengi wanajifunza mambo mengi ya siasa yetu ya tanzania inavyokwenda.
kwa upande wangu nashukuru sana chama cha demokirasia na maendeleo CHADEMA NAWAPA MOYO KWAMBA WASIKATE TAMAA WAENDELEE NA MAPAMBANO WATASHINDA 2NA WAOMBEA MUNGU SANA.