Hali bado tete upatikanaji wa maji katika vijiji vya Misungwi

Jamii Africa

Inawezekana wakazi wa  wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wakaendelea kusubiri kwa muda mrefu kabla ya kupata maji safi na yenye uhakika, kutokana na  miradi ya usambazaji maji kufika maeneo machache ya wilaya hiyo.

Wilaya ya Misungwi inavyokabiliwa na kero kubwa ya maji ya muda mrefu licha ya ukweli kwamba wilaya hiyo iko kilometa chache tu kutoka Ziwa Victoria.

Maeneo mengi ya vijiji vya wilaya hiyo yamekuwa yakitegemea maji ya visima ambavyo kipindi cha kiangazi hukauka na kusababisha watu kutumia maji yaliyotuwama kwenye madimbwi, jambo ambalo ni hatari kwa afya za wananchi.

Licha ya wilaya hiyo kuwa jirani na Ziwa Victoria, lakini Mradi Mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria ambao uligharimu mabilioni ya fedha kutoka Shirika la WaterAid umepita katika baadhi ya vijiji vya wilaya hiyo ingawa hakuna utaratibu wowote wa kuviwekea miundombinu ili kusambaza maji hayo.

Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria unalenga kusambaza maji katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Tabora, hivyo Misungwi ilipaswa kuwa miongoni mwa maeneo ya wanufaika, lakini badala yake bomba hilo kuu limekuwa kama pambo kwa wakazi wa vijiji vya wilaya hiyo linakopitia.

Ingawa vipo vijiji katika Wilaya ya Misungwi ambavyo viko pembezoni mwa Ziwa Victoria, lakini ni vigumu kutumia maji hayo moja kwa moja kwani si salama kutokana na uchafu unaomwagwa kuelekea ziwani, ambao umeyafanya maji hayo kuwa na kemikali hatari.

Mpaka kufikia mwaka 2018 hali ya upatikanaji wa maji wilayani Misungwi imeendelea kuwa si ya kuridhisha kwa vijiji vingi vilivyopitiwa na bomba hilo, hili linathibitishwa na taarifa za nyakati tofauti za baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo kutaka kuvamia miundombinu ya bomba hilo kwa kile kinachoonekana kutokuwa na faida nalo.

Akichangia mjadala bungeni April 2018,  Mbunge wa Jimbo la Misungwi, Charles Kitwanga alitishia tena kuwahamasisha wananchi wa jimbo lake kuvamia mradi huo na kuzima mitambo inayosukuma maji kuelekea vijiji vya wilaya zingine.

Kauli hiyo ya Kitwanga ni muendelezo wa kilio cha wakazi wa Misungwi ambao bado wanataabika kwa kukosa maji ya uhakika na salama katika maeneo yao.

Taarifa ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji inasema kufikia mwaka 2025 bomba hilo linatarajiwa kuhudumia watu milioni 1.

         Maeneo mengi ya vijiji vya wilaya ya Misungwi yamekuwa yakitegemea maji ya visima ambavyo kipindi cha kiangazi hukauka

Lakini miaka 7 kabla ya kufikia mwaka huo bomba hilo limeshindwa kuwa msaada kwa watu 351,607 wa Misungwi huku wilaya hiyo ikiwa na ongezeko dogo la watu la asilimia 2.8.

 

Mkakati wa serikali

Ili kuwaondolea hadha ya maji wakazi wa Misungwi, serikali imesema inashirikiana na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya kutekeleza miradi ya uboreshaji huduma ya maji kwa kutandaza mtandao wa mabomba na kujenga vituo vya maji katika vijiji vilivyo karibu na bomba kubwa la maji kutoka ziwa Victoria.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwele, akisoma makadirio ya bajeti ya wizara yake ya 2018/2019 alisema, “Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank-EIB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (French Development Agency-AFD) inaendelea kutekeleza miradi ya uboreshaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira katika Jiji la Mwanza na Miji ya Magu, Misungwi na Lamadi kwa gharama ya Euro milioni 104.5.”

Kupitia mradi huo wa kuboresha huduma ya maji katika mji wa Misungwi,  kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kujenga mifumo mipya ya kusafisha na kutibu maji; ulazaji wa bomba kuu na mabomba ya kusambaza maji; ujenzi wa matanki; ujenzi wa vituo vya kuchotea maji na ununuzi wa vitendea kazi (magari na pikipiki).

“Hadi mwezi Machi 2018, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 10 na unatarajiwa kukamilika mwezi Mei, 2019. Kukamilika kwa mradi huo kutawanufaisha wakazi 23,315 waishio Misungwi Mjini na Kijiji cha Nyahiti,” alisema Waziri Kamwele.

Licha ya utekelezaji wa mradi huo kwa mwaka wa fedha 2018/2019, bado hautaweza kuwafikia wakazi wengi wa vijiji vya pembezoni ambao wanakabiliwa na tatizo la maji kuliko wale waishio Misungwi mjini.

Hiyo ina maana kuwa watalazimika kusubiri kwa muda mrefu mpaka fedha zingine zitengwe au ajitokeze mfadhili atakayeguswa na hali hiyo ya uhaba wa maji wilayani humo.

Serikali inapaswa kulitazama suala hilo kwa jicho lingine ikizingatiwa kuwa maji ni uhai, na ili binadamu aishi anahitaji maji. Je serikali iko tayari kuona wananchi wake wanapoteza maisha kwa kukosa maji?

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *