Hoja za kitaifa zitawaunganisha au kuwatenganisha wabunge 2018?

Jamii Africa

Kabla ya kuingia katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, Tanzania ilikuwa na mfumo wa Bunge la chama kimoja yaani wabunge wote walitoka chama tawala. Majadiliano ya wabunge yaliwapa fursa wabunge kutofautiana katika hoja mbalimbali na mwishowe kufikia uamuzi wa pamoja wa kupitisha maazimio.

Wabunge walikosa uhuru wa kujadili hoja za serikali kwa mapana kwasababu walikuwa ndani ya mfumo wa chama kimoja na hivyo kulazimika kukubaliana na mapendekezo yaliyotolewa na serikali hata kama wabunge hawakubaliana nayo.

 Mipango ilitegemea fikra za watu wachache na hata wabunge waliojaribu kupinga mipango ya serikali ambayo haina tija kwa wananchi walipata upinzani mkubwa kutoka kwa viongozi wengine na kuonekana kama ni maadui wa maendeleo.

Mathalani, kundi la wabunge lililojulikana kama G55 ambao walileta hoja ya kuwa na serikali ya Muungano yenye serikali tatu na wakaanzisha harakati za kushawishi ambapo kungekuwa na serikali ya moja ya Muungano, serikali ya Mapinguzi Zanzibar na ile ya Tanganyika. Lakini jitihada hizi zilipingwa vikali na watawala wa wakati huo na wabunge hao walinyamazishwa kwa kuhusishwa na tuhuma mbalimbali za kuuhujumu muungano.
 
Mageuzi makubwa ya kisiasa yaliyotokea barani Afrika kutoka mfumo wa kijamaa na kuingia katika  mfumo wa Kibepari ambao ulileta mabadiliko ya mfumo wa kuongoza na wananchi kuongezewa uhuru wa kutoa maoni na kusikilizwa, watu kujiamulia mambo yao bila kuingiliwa na mtu lakini sio kwa kiwango cha kuvunja sheria za nchi.

Bunge nalo likabadilika kutoka katika mfumo wa chama kimoja na kuhusisha vyama vingi vyenye itikadi  na  mitazamo tofauti, wabunge walikuwa huru zaidi kuikosoa serikali na watendaji wake ili kuboresha uwajibikaji na kutimiza majukumu yao kwa viwango sahihi.

Dhana ya vyama vya upinzani ilitokana na mtazamo wa demokrasia ambao wanafalsafa wake wanaamini kuwa huwezi kutatua matatizo na watu wenye uwezo sawa wa mawazo bali watu wenye mawazo yanayokinzana/tofautiana lakini yakiwa na lengo la kuleta mabadiliko katika jamii.

Uchaguzi wa kwanza  wa vyama vingi ulifanyika mwaka 1995 ambapo ulitoa fursa kwa vyama vilivyosajiliwa kusimamisha wagombea wao ili kushindana na wagombea wa chama tawala CCM. Wabunge kadhaa wa upinzani kutoka chama cha NCCR- Mageuzi na vyama vingine waliingia  bungeni. Uwepo wao bungeni ulikuwa   ni changamoto kubwa kwa serikali kwa sababu walitumia uhuru wa kujieleza na kuikosoa serikali ili itimize majukumu yake ipasavyo.

Wabunge hawa bila kujali itikadi za vyama vyao, walitumia uhuru wao vizuri na kuzingatia nidhamu na sheria za bunge. Hurka hii ilikuwa ni ya kihistoria kwa Bunge la Tanzania kwa kuwa wabunge walijadili hoja mbalimbali kwa kutofautiana lakini mwisho walifikia muafaka kuhusu maendeleo ya taifa.

Nidhamu ya bunge iliimarika zaidi  baada ya kuchaguliwa  Spika Samuel Sitta mwaka 2006 ambaye anatajwa kuwa spika wa viwango kwa sababu ya umahili wake wa kuongoza bunge bila kuegemea upande wowote na kutoa fursa sawa kwa wabunge kujadili masuala ya kitaifa kwa upana kuongeza uwazi na uwajibikaji wa watendaji serikalini. 

                                                              Muonekano wa ndani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wananchi walikuwa na imani kubwa na wabunge. Bunge ilikuwa sehemu muhimu ya kuwakilisha matatizo yao kwa sababu wabunge waliungana na kuonyesha nia ya kuwatoa wananchi katika umaskini.

Hali ilibadilika baada ya uchaguzi wa mwaka 2010 bunge likapunguza nguvu yake, nguvu ya wabunge kusimama pamoja katika masuala muhimu ya taifa imeendelea kupungua huku maslai binafsi na makundi ya vyama yakipata nafasi kubwa na kuacha hoja za msingi za kuibua ufisadi na kuisimamia serikali kuwajibika mbele ya wananchi.   

Mbunge wa Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa akichangia katika kikao cha Bunge Juni 20 mwaka 2012 aliwakumbusha wabunge wajibu wao na kujikita kwenye hoja za kitaifa, “Watu ambao tuko 350 taifa limetuamini tunatakiwa kuhoji na tumeumbwa kutatua matatizo na sio kutengeneza matatizo kwa hiyo tukija hapa tujadili masuala yanayoligusa taifa”,

“Tunapofika katika karne hii katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunapojadili bajeti maana yake tuna changamoto zinazotukabili kama taifa lakini tunaanza kuongea ngonjera, maneno ya uswahili yenye unafiki, woga, kujipendekeza na kutojadili mambo ya msingi”.


Siku chache zijazo bunge litaanza vikao vyake mjini Dodoma chini ya Spika Job Ndugai na wananchi wanatarajia mambo ya msingi yatajadiriwa na kutafutiwa ufumbuzi ikizingatiwa kuwa taifa linakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiuchumi ambazo zimezidisha kiwango cha umaskini miongoni mwa wananchi.

Miongoni mwa miswada itakayojadiliwa ni ongezeko la umri wa kustaafu kwa lazima kutoka miaka 60 hadi 65. Ongezeko hilo litawahusu Maprofesa, Wahadhiri Waandamizi na Madaktari Bingwa wa taasisi za umma. Pia kuiboresha sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii.

 Wabunge hawana budi kutanguliza maslai ya wananchi hasa kipindi hiki ambacho vikao vya kamati za bunge zimeanza ili kujadili na kutoa mapendekezo juu ya mipango na matumizi ya rasilimali za nchi.

Ni matarajio ya wananchi kuona wabunge wakisimama pamoja kutetea maslahi mapana ya wananchi wanyonge na kuishauri serikali njia sahihi za kuboresha huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu, maji, umeme. Vikao vya bunge la 2018 vikawe chachu ya kuleta maendeleo na kuwapunguzia wananchi mzigo wa umaskini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *