MATUMIZI ya huduma za uzazi wa mpango nchini yameendelea kuwa chini kwa asilimia 27 huku serikali ikihadi yatafika asilimia 60 ifikapo mwaka 2015.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Mara, Dk Irag Ngerageza alisema moja ya sababu ya mimba zisizotarajiwa ni ukosefu wa huduma za uzazi wa mpango hasa katika maeneo ya vijijini yasio na vituo vya huduma.
Alisema huduma hiyo ni muhumu kwa mwanamke na mwanaume kwani husaidia kupanga idadi ya watoto katika familia na tofauti ya muda wa uzazi mmoja na mwingine.
Utafiti wa Hali ya Maisha na Afya wa mwaka 2010 unaonesha asilimia 34 ya wanawake walioolewa wenye miaka 15 na 49 wanatumia njia za uzazi wa mpango, kati yao asilimia 27 wanatumia njia za kisasa.
Alisema huduma za uzazi wa mpango zina mchango mkubwa katika kupunguza vifo vya wajawazito na watoto kwa asilimia 30.
Takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii za mwaka 2010 zinaonesha wanawake 454 katika vizazi hai 100,000 walikuwa wanapoteza maisha wakati wa ujauzito au wanapojifungua.
Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), Dk. Albina Chuwa anasema taarifa ya sensa ya mwaka jana itatumiwa kutathmini mpango wa malengo ya Milenia wa mwaka 2015 ambao lengo lake namba 4 na 5 linataka kupunguza kwa asilimia 75 vifo vya wajawazito na watoto.
Dk Ngerageza alisema ili afya ya mama iimarike, inafaa kuwepo kipindi cha angalau miezi 36 (miaka mitatu) kati ya mtoto mmoja na mwingine. Hii pia inapunguza hatari ya vifo vya watoto wanaozaliwa.
Alisema watoto wanaozaliwa kabla ya miaka mitatu ya uzazi uliotangulia wana uwezekano mkubwa wa kufa kabla ya kutimiza miaka mitano.
Alisema vifo hivyo ni vya watoto 136 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai, ikilinganishwa na vifo vya watoto 74 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa miaka mitatu baada ya uzazi uliotangulia.
Alisema baadhi ya wanawake walioolewa na kuzaa bila mpangilio wamekiri kufanya hivyo kwasababu ya kukosa huduma ya uzazi wa mpango.
“Wako pia wanaosema wangependa kusubiri angalau miaka miwili kabla ya kuzaa tena lakini wanakosa huduma hiyo,” alisema.
Akihutubia Mkutano wa kimataifa wa uzazi wa mpango uliofanyika Juni mwaka jana London, Uingereza kwa uratibu wa asasi ya Bill and Melinda Gates Foundation na serikali ya uingereza, Rais Jakaya Kikwete alisema kwasasa tiba zilizopo zinawafikiwa wanawake milioni 2.4 nchini Tanzania.
Alisema Tanzania inahitaji Sh bilioni 140 kusaidia kutekeleza mipango ya huduma ya uzazi wa mpango kwa wanawake milioni 3.2 ifikapo mwaka 2015.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema mpango huo unakabiliwa na changamoto alizozitaja kuwa ni ukosefu wa rasilimali ili kukidhi mahitaji, ukomo katika masuala ya kijamii kama vile utamaduni na imani za kidini na ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi kwa wasichana na wavulana.
Cell 0784991020, 0655991020