Je, ni wakati sahihi kufuta mitihani ya kitaifa katika shule za msingi?

Jamii Africa

Serikali imeshauriwa kuupitia upya mfumo wa utoaji mitihani ya kitaifa katika shule za msingi ili kuokoa idadi ya wanafunzi wanaokariri madarasa na kuacha shule.

Kulingana na mfumo wa elimu ya msingi nchini Tanzania, mwanafunzi anatakiwa kufanya mitihani miwili ya kitaifa ili asonge mbele kwa madarasa yanayofuata. Wanafunzi hufanya mtihani wa darasa la nne ambapo wanaofaulu huingia darasa la tano lakini wanaofeli hukariri darasa hilo mpaka wafaulu.

Hivyo hivyo, mwanafunzi akififanikiwa kuvuka darasa la nne atakabiliwa na mtihani wa darasa la saba ambapo akifanya vizuri ataruhusiwa kuandikishwa elimu ya sekondari lakini kama akifeli atabaki nyumbani labda ajiunge na elimu ya ufundi.

Benki ya Dunia kupitia wataalamu wake wa elimu Afrika, wameshauri serikali kutathmini faida na hasara za mitihani ya kitaifa kwa mstakabali wa elimu nchini ikizingatiwa kuwa baadhi ya wanafunzi kutokana na mazingira ya yasiyoridhisha ya kusomea hukosa maarifa ya msingi kuweza kujibu mitihani.

Maneja wa Benki ya Dunia anayesimamia Elimu katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika, Dkt. Sajitha Bashir amesema mitihani ya kitaifa inawazuia wanafunzi kuendelea mbele kimasomo hasa wakifeli na wengine huacha shule.

“Mitihani ya kitaifa inawazuia wanafunzi kuendelea kimasomo kutoka msingi hadi sekondari katika nchi nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara”, amesema Dkt Sajitha.

Amebainisha kuwa katika nchi 28 kati ya 43 za Afrika ambazo zina takwimu za elimu imebainika kuwa nchi hizo wanafunzi wa elimumsingi wanafanya mitihani ya kitaifa ambapo kwa sehemu ni kikwazo kwa wanafunzi wasiojiweza kuendelea na masomo ya sekondari.

“Hii mitihani inasababisha shule kuwakaririsha madarasa wanafunzi wenye uwezo mdogo”, amesema Dkt. Sajitha na kuongeza kuwa hali hiyo husababishwa na changamoto za elimu ikiwemo uhaba wa walimu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwenye shule.

 Utafiti uliofanyika katika nchi za Afrika zinazozungumza Kifaransa unakadiria kuwa kuchelewa kwa elimu ya msingi kuwa ya lazima ni matokeo ya kiwango kikubwa cha wanafunzi kukariri madarasa katika nchi hizo.   

Nchi ambazo zimeimarisha mfumo wa elimu ya msingi na sekondari zimejumuisha na kuzifanya kuwa za lazima ambapo hutolewa kwa miaka 8 hadi 9 ambapo wameondoa mitihani ya kumaliza elimu ya msingi ambapo mwanafunzi hujiunga moja kwa moja na sekondari bila ulazima wa kufanya mtihani.

 Dkt. Sajitha anafafanua kuwa kufuta mitihani ya kumaliza elimu ya msingi kunaweza kutengeneza mabadiliko kadhaa ambayo yanaweza kuwa na umuhimu mkubwa wa kuimarisha mfumo wa elimu na hamu ya wanafunzi kupata maarifa yatakayowasaidia katika maisha kuliko kusoma ili wafanye mitihani.

“Kufuta mitihani kunatengeneza mabadiliko  ya kupunguza kukariri katika madarasa ambayo mtihani unaofanyika na madarasa ya nyuma; na inaongeza viwango vya mpito kuelekea elimu ya sekondari. Botswana imepitia kivitendo mabadiliko haya: Mwaka 1987 nchi hii ilifuta mitihani ya mwisho katika shule za msingi, ambayo mwanzoni ilitumika kuchagua wanafunzi kwenda sekondari”, amesema Dkt. Sajitha.

Ameongeza kuwa baada ya Botswana kupitia mabadiliko hayo ya kisera, kiwango cha mpito kati ya elimu ya msingi na sekondari kiliongezeka haraka, kutoka asilimia 50 kabla ya 1987 hadi kufikia asilimia 90 mwaka 1994

 

Wadau wa Elimu nchini watofautiana

Mwalimu Joseph Mmbando, Mmiliki wa shule ya sekondari amesema haoni sababu ya kufuta mitihani shuleni kwasababu mitihani inatumika kupima uelewa wa wanafunzi kitaaluma na kuwafanya wawe na bidii ya kusoma wakijua wanakutana mtihani mbele.

Ameongeza kuwa  ikiwa wanafunzi watajifunza vizuri na kusimamiwa na walimu wao hawawezi kufeli. Ameitaka serikali kuboresha miundombinu ya kujifunzia ili wanafunzi wawe na moyo wa kujifunza kufanya vizuri katika mitihani iliyo mbele yao.

“Shule binafsi  zinafanya vizuri kwa sababu ya uangalizi wa karibu wa wamiliki. Shule za Serikali nyingi uangalizi hauko vema hivyo si rahisi kufanya vizuri kitaaluma”, amesema Mwalimu Mmbando.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Shule Kuu ya Elimu ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dkt. Luka Mkonongwa amesema hatua hiyo itawezekana ikiwa utaratibu mzuri utaandaliwa juu ya mfumo sahihi ambao kama nchi tunapaswa kuufuata kuinua kiwango cha elimu nchini.

“Tuwe na msimamo wa kitaifa katika sekta ya Elimu Tanzania. Hatuna utaratibu wa kuilinda sera ya Elimu, tunayumbishwa na matamko, ni lazima tuwe na utaratibu maalumu utakaofuatwa na kuheshimiwa na kila mtu”

Naye Mchambuzi wa masuala ya Kisiasa, Prof. Mwesiga Baregu amesema nchi inahitaji mjadara mpana wa kitaifa juu ya masuala muhimu ya elimu ikiwemo mfumo wa mitihani kwa wanafunzi. “Tanzania inahitaji mjadala mkubwa wa elimu. Je, ni wapi tunaelekea?”.

Hivi karibuni serikali ilitoa waraka ambao unazikataza shule zinazomilikiwa na watu binafsi kuwakaririsha wanafunzi madarasa isipokuwa kwa mitihani ya kitaifa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *