Jinsi Richmond Na Dowans Walivyoizunguka TANESCO

Jamii Africa

Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development wa tarehe 23 Juni, 2006 wa kuingiza majenereta ya umeme kufuatia upungufu wa nishati hiyo mwaka uliokuwa umekithiri nchini mwaka 2006 ulihamishiwa kwa kampuni ya Dowans Holdings S.A tarehe 14 Oktoba, 2006 mwezi mmoja kabla bila ya kuihusisha TANESCO kama ilivyotakiwa kwa mujibu wa kifungu 15.12 cha mkataba huo.

Kifungu hicho cha Mkataba kilikuwa kinaruhusu mkataba huo uliokuwa na thamani ya dola milioni 172.5 kuahulishwa kwenda kwenye kampuni nyingine baada ya makubaliano ya pande hizo mbili tena kwa maandishi.

Sehemu ya kifungu hicho cha mkataba huo ambao FP inao kinasema wazi kuwa “Neither party may assign this agreement or grant any security interest, charge, lien, or other encumbrance in this Agreement other than by mutual agreement between the parties in writing”. Kwa maneno mengine, mkataba ulikataza pande zote mbili (TANESCO na RDC) kuhaulisha jukumu lolote au jambo lolote linalohusiana na mkataba huo kwenda kwa kampuni au chombo kingine pasipo makubaliano ya maandishi kati ya pande hizo mbili.

Hivyo kitendo chochote kwa upande wa TANESCO au Richmond kuhamisha mkataba au majukumu yake kwenda kwa chombo kingine bila ridhaa ya kimaandishi ya mwenzake ilikuwa ni uvunjaji wa mkataba huo. Hata hivyo, katika taarifa ambazo Kamati Teule iliyoundwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchunguza Richmond ilipatiwa chini ya kiapo kampuni ya Richmond ilihamisha mkataba wake kwa Dowans Holding S.A tarehe 23 Disemba, 2006.

Mlolongo wa matukio kwa mujibu wa ripoti ya Kamati teule hadi kufikia RDC kuhamisha unaonesha kuwa Shirika la Ugavi wa Umeme la Tanzania lilifichwa ukweli wa kilichokuwa kinaendelea kwani haikujua kuwa wakati wote inafikiria ugumu wa kuhamisha mkataba huo kwenda Dowans kampuni ya Richmond tayari ilikuwa imeshauhamisha mkataba huo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyosomwa kwa kile kilichodaiwa na aliyekuwa Waziri Mkuu Bw. Edward Lowassa kuwa ni “kwa mbwembe” inaonesha kuwa TANESCO waliandikia RDC barua tarehe 27 Oktoba, 2006 ya tahadhari kuwa RDC ilikuwa inaonesha kushindwa kutekeleza masharti ya mkataba (default notice) iliyotaka majibu kufuatia mapungufu kadhaa ambayo TANESCO waliyaona. Ripoti hiyo inasema kuwa kwa mujibu wa TANESCO mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na “kushindwa kwa kampuni hiyo kusafirisha angalau mtambo wa kwanza wa wastani wa unit 22 kW kuja Tanzania; kushindwa kwa kampuni hiyo kutoa taarifa za mara kwa mara za maendeleo ya utekelezaji wa mradi; uwepo wa kampuni hiyo Marekani kihalali; uwezo wa kampuni hiyo kitaalamu na kifedha kuweza kutekeleza Mkataba huo wa umeme wa dharura katika muda muafaka.”

Lengo la taarifa hiyo ilikuwa ni kutaka majibu kutoka RDC ya kwanini TANESCO isione kuwa Richmond wameshindwa kazi na hivyo kuvunja mkataba. Barua hiyo ya tahadhari haikujibiwa. Kwa mujibu wa Ripoti ya Mwakyembe shirika la TANESCO likaandika barua nyingine za tarehe 17 na 23 Novemba, 2006 “kuikumbusha (Richmond) kuhusu hoja zake za awali (za barua ya Oktoba 27, 2006) ambazo hazikujibiwa na kudai maelezo kuhusu taarifa za kwamba kampuni hiyo haikuwa na mahusiano na Pratt & Whitney iliyotegemewa sana kubeba sehemu kubwa ya majukumu ya mradi.”

Hata hivyo barua zote hizo tatu hazikujibiwa wala hoja zilizoibuliwa na TANESCO kupewa majibu yenye ushawishi wa ukweli na mvuto wa kiakili. Na siku hiyo ya Novemba 23, 2006 Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO alijieleza kwa Waziri juu ya tatizo lililokuwa linaonekana kuhusu uwezo wa Richmond. Tarehe 28 Novemba, 2006 yaani siku tano baada ya barua ya Mkurugenzi wa TANESCO Waziri wa Nishati Bw. Nazir Karamagi alimpigia simu aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO Balozi Fulgence Kazaura kumtaarifu kuwa kampuni ya Richmond ilikuwa inakusudia kuhaulisha mkataba wake kwenda kampuni “nyingine” na hivyo alitaka kujua kama mkataba uliruhusu uwezekano huo.

Ripoti ya Mwakyembe inasema kuwa “Tarehe hiyo hiyo 28 Novemba 2006 uongozi wa TANESCO ulimshauri Mwenyekiti wa Bodi kama ifuatavyo:- (i) Mkataba kati ya Richmond Development Company LLC na TANESCO hauruhusu kukabidhi majukumu ya Mkataba kwa Kampuni nyingine isipokuwa kwa maafikiano ya pande mbili za
Mkataba (Kifungu 15.12).” Tarehe 4 Disemba, 2006 (chini ya siku kumi tangu Karamagi adokeze nia ya Richmond kuhamisha mkataba) TANESCO walipokea barua kutoka Richmond ambayo ilionesha kuwa kampuni hiyo ilitaka “kutumia haki yake chini ya Kifungu 15.12 cha Mkataba ili kuhamisha majukumu yake yote ndani ya Mkataba huo kwenda kwa DOWANS Holdings, S.A. Aidha, Richmond Development Company LLC ilieleza kwamba tarehe ambayo TANESCO itaridhia mapendekezo hayo iwe ndiyo tarehe rasmi ya kuhamisha mafao na majukumu yote kwa DOWANS Holdings, S.A na kwamba DOWANS Holdings, S.A itawasilisha vielelezo vya utambulisho wake kwa TANESCO”

Hata hivyo, barua hiyo ambayo TANESCO waliipokea Disemba 4, inaonesha kuwa iliandikwa Novemba 9, karibu mwezi mmoja kabla. Siku moja kabla ya kupokea barua ya Dowans kutaka kuhamishia mkataba wake kwa Dowans yaani tarehe 8 Disemba, 2009 TANESCO ilikuwa imeiandikia Benki ya Citibank isaidie kufanya uchunguzi wa kujua kampuni ambayo Richmond ilikuwa inataka kuhamishia mkataba wake ilikuwa ni kampuni gani na yenye uwezo gani kwani “la “kwani japokuwa masharti ya Mkataba yanaruhusu Mkataba kuhamishwa, TANESCO ingependa kufahamu hasa ni nani anayehamishiwa Mkataba huo”.

Kamati Teule haikufanikiwa kupata majibu ya Citibank ila iliambiwa kulikuwa na shinikizo toka Wizarani “kuwa viongozi wa Wizara kama kawaida yao waliishinikiza TANESCO kukubaliana na ombi la Richmond Development Company LLC la kuhamisha mkataba.” Ni kutokana na hilo tarehe 21 Disemba, 2006 TANESCO ikaiandikia kampuni ya Richmond kukubali uhaulishaji wa mkataba huo kwenda kwa Dowans kwa barua yenye SEC. 388/12/206 ambapo pamoja na mambo mengine ilitaka “ipate hati ya uthibitisho kutoka Dowans Holdings, S.A ya kuridhia uwajibikaji kamilifu katika kutekeleza Mkataba wa tarehe 23 Juni, 2006, kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC.”

Hivyo tarehe 23 Disemba 2006 Mkataba ukaingiwa kati ya TANESCO na Dowans S.A ambao ulikuwa ni kuhamishia mkataba kati ya TANESCO na Richmond kwenda kwa Dowans Holdings S.A.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kamati Teule kusainiwa kwa mkataba huo kati ya TANESCO na Dowans Holding S.A kulileta mambo matatu muhimu ; kwanza, “Tarehe 23 Disemba 2006 ndiyo siku rasmi ambayo Richmond Development Company LLC imekabidhi rasmi majukumu yake ya utekelezaji wa Mkataba kati yake na TANESCO kwa Dowans Holdings S.A”; Pili, “Dowans Holdings, S.A itatekeleza majukumu ya Mkataba uliotiwa saini kati ya TANESCO na Richmond Development Company tarehe 23 Juni, 2006 kwa masharti yote kama yalivyo katika Mkataba”; na tatu, “Malipo halisi na madeni ndani ya Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC, sasa yatakwenda kwa Dowans Holdings, S.A kuanzia tarehe 23 Disemba, 2006.”

Hata hivyo kulikuwa na tatizo; Richmond Development Corporation LTD ilikuwa tayari imeshahamisha mkataba wake na TANESCO kwenda kwa Dowans miezi karibu miwili nyuma. Yaani, RDC iliingia mkataba na Dowans Holdings S.A tarehe 14 Oktoba, 2006 bila ya kushirikisha, kutaarifu au kwa namna yoyote ile kupata maridhiano ya kimaandishi toka kwa TANESCO kinyume cha kipengele cha 15.12 tulichokiona hapo juu.

Hii ina maana kuwa mazungumzo yote yaliyofuatia hadi TANESCO kukubali kuwa Richmond ihamishe mkataba kwenda kwa Dowans SA katika barua ya Disemba 21, 2006 yalikuwa ni kanyaboya, au danganya toto kwani wakati TANESCO inaingia ikiamini (in good faith) kuwa Richmond ilikuwa bado haijahaulisha mkataba kwa Dowans, Dowans iliingia ikijua kuwa tayari imekwisha fanya hivyo.

Kampuni ya Richmond ilihamisha mkataba wake kwenda Dowans tarehe 14 Oktoba, 2006 ikikabidhi majukumu yake yote iliyokuwa imekubaliana na TANESCO kwenda kwenye kampuni hiyo inayodaiwa kuwa ni ya Costa Rica. Mkataba huo uliingiwa kabla tu ya mitambo ya kwanza kusafirishwa kwa ndege kupelekwa Tanzania. Siku hiyo hiyo wakati Richmond inahamisha mkataba wake wa Juni 23, 2006 na TANESCO kwenda Dowans Holdings S.A ilihamisha vile vile mkataba wake wa Septemba 25, 2006 kati yake na Vulcan (Vulcan Advanced Mobile Powers Systems, LLC na Vulcan Power Group, LLC) wa ununuzi wa mitambo toka kampuni hiyo kwenda kampuni ya Dowans Holdings S.A.

Ni muhimu kutaja kuhamishwa kwa mkataba wa Richmond na Vulcan kwenda Dowans S.A kwa sababu mara baada ya mkataba huo kuhamishwa kwa Dowans S.A kampuni hiyo ililipa Vulcan dola milioni 7.5 na ikanunua mtambo wa kwanza wa gesi ambao uliingizwa nchini mwishoni mwa 2006 na kupokelewa kwa shangwe. Wakati baadhi ya magazeti yaliripoti kuwa “mitamo ya Richmond yawasili” ukweli ni kuwa mitambo hiyo ilikuwa ni ya kampuni ya Dowans Holdings S.A ambayo ndiyo ilinunua na kugharimia kuingizwa kwake nchini.

Hili hata hivyo linaleta matatizo makubwa mawili ya kisheria ambayo yote yanahusiana na malipo ya shilingi bilioni 94 ambayo kampuni ya Dowans S.A inatarajiwa kulipwa siku chache zijazo kufuatia hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (International Court of Arbitration). Tatizo la kwanza ni kuwa wakati aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Bw. Nazir Karamagi alipozungumza na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO Balozi Fulgence Kazaura Novemba 28, 2006 kuulizia kama mkataba wa Richmond unaruhusu kuhamishwa kwenda kampuni nyingine, kampuni ya Richmond ilikuwa tayari imekwisha hamisha mkataba huo kisheria kwenda Dowans Holdings S.A.

Hii ina maana kuwa yote yaliyofuatia hapo hadi baadaye TANESCO kukubali kuhamisha mkataba kwenda Dowans kwa barua yake ya Disemba 21, 2006 yalikuwa ni mazingaombwe tu ya kujaribu kutimiza matakwa ya kifungu cha 15.12 cha mkataba wa Richmond na TANESCO kama tulivyoona hapo juu. Ilikuwa ni muhimu kwa Richmond kutimiza kifungu hicho kwa sababu vinginevyo mkataba kati yake ya Dowans usingekuwa halali kwani ungekuwa umehaulishwa kinyume cha makubaliano.

Hili linatuleta kwenye kuelewa kwanini jitihada zote za TANESCO kuitaarifu Richmond kuwa ilikuwa inaelekewa kushindwa kutekeleza mkataba hazikuzaa matunda. Inafafanua kuwa kwanini barua za Oktoba 27, Novemba 17, 23 na 29 kwenda kwa Richmond hazikujibiwa na badala yake maelekezo ya Waziri Karamagi (Novemba 28, 2006) kwa Kazaura kuwa “Richmond Development Company LLC walikuwa wanataka kuhamisha majukumu yao yaliyobaki katika Mkataba wa uletaji mitambo na uzalishaji umeme wa dharura kwa kampuni nyingine.” Majibu yaliyotolewa siku ile ile kwenda kwa Waziri kuwa “ Kifungu cha 15.12 cha Mkataba huo hakiruhusu kukabidhi majukumu ya Mkataba kwa Kampuni nyingine isipokuwa kwa maafikiano ya pande mbili za Mkataba.” Hili lilithibitisha tatizo ambalo Richmond waliligundua baada ya kuingia mkataba na Dowans Oktoba 14, 2006 bila kuwashirikisha TANESCO. Hivyo, mpango wa “kuwashirikisha TANESCO” ukaingizwa na hatimaye TANESCO wakakubali na “mkataba” ukahamishwa “rasmi” kwenda Dowans Disemba 23, 2006 kama Ripoti ya Mwakyembe ilivyoonesha. Hii ina maana Richmond ilivunja mkataba na TANESCO pale ilipoamua kuhamisha mkataba wake huo kwenda kwa Dowans Oktoba 14, 2006 bila ya ridhaa, ushauri, makubaliano ya kimaandishi kati yake na TANESCO kama kipengele cha 15.12 cha Mkataba kilivyotaka.

Richmond ilijua kuwa imefungwa na kipengele kingine ambacho kiliweka wazi kuwa endapo ingehamisha mkataba huo bila ya kuihusisha TANESCO basi itakuwa imejiingiza matatani. Kipengele hicho ni cha 12.1e ambacho ni sehemu ya mambo ambayo yatafanya Richmond kuwa imeelekea kushindwa kutekeleza mkataba. Hivyo, Richmond ilikuwa haina jinsi nyingine kwa sababu isingeweza kuiambia TANESCO kuwa tayari imeingia mkataba na Dowans kwani itakuwa ni sababu tosha kwa TANESCO kuvunja na isingeweza kuvunja tena na mkataba na Dowans S.A kwani tayari Dowans walishaingia gharama za kununua majenereta toka Vulcan. Njia rahisi ilikuwa kuanzisha mazingaombwe ya “kuhaulisha mkataba kwenda kampuni nyingine”.

Hili hata hivyo linatuingiza kwenye tatizo kubwa la pili ambalo linahusiana moja kwa moja na malipo ya Bilioni 94 kwenda Dowans S.A siku chache zijazo. Kesi iliyoamuriwa na ICC-ICA ilizingatia kati ya mambo mengi uhalisia na uhalali wa mkataba wa Dowans. Sehemu kubwa ya hukumu hiyo ilishughulikia ukweli kuwa mkataba uliokuwa umeingiwa na TANESCO na Dowans wa Disemba 23, 2006 ulikuwa ni halali. Katika hukumu hiyo kilichoangaliwa ni makubaliano ya kuhamisha mkataba kutoka kwa Richmond kwenda Dowans Holdings S.A kama yalivyoanzishwa na mawasiliano ya simu kati ya Waziri Nazir Karamagi (akiwa Calgary, Canada) kwenda kwa aliyekuwa mwenyekiti wa bodi Balozi Kazaura Novemba 28, 2006.

Kuna mambo ambayo tuna uhakika nayo na ambayo ni msingi wa hatimaye kukataa kuwalipa Dowans S.A na Dowans Tanzania Limited tuzo iliyotolewa na Mahakama ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICC). Mambo yafuatayo ni ya kuzingatia.

  1. Wakati Karamagi anawasiliana na Kazaura kuulizia kama mkataba wa Richmond/TANESCO unaruhusu kuhamishika alikuwa tayari na taarifa kuwa Richmond walikuwa tayari wameshahamisha mkataba kwenda Dowans, SA Oktoba 14,2006 (mwezi mmoja na nusu kabla)
  2. Majibu ya TANESCO siku ile ile kwenda kwa Kazaura ikitaja uwepo wa kifungu cha 15.12 kwenye mkataba kinachozuia kuhaulisha mkataba bila ya ridhaa ya maandishi toka kwa TANESCO inatuonesha kuwa TANESCO walikuwa hawajui kuwa Richmond walikuwa tayari wamehamisha mkataba wao kwenda Dowans Holdings S.A Oktoba 14, 2006
  3. TANESCO wakiwa wamepewa jina la kampuni iliyokusudiwa kuhamishiwa mkataba ya Dowans S.A wanawasiliana na wawakilishi wa kampuni hiyo ili kupata taarifa za uwezo na uhalisia wa kampuni hiyo kuweza kuchukua mkataba. Na wanawaandikia barua Citibank ili iwasadie kufanya uchunguzi wa uhalisia na uwezo wa kampuni hiyo. Barua hiyo inaandikwa Novemba 8, 2006. Barua hiyo aidha haijibiwi au hakuna ushahidi wa kuwepo kwa majibu yake.
  4. Novemba 9, 2006 kampuni ya Richmond wanawaandikia barua rasmi TANESCO kuwajulisha nia yao ya kutaka kuhamisha mkataba kwenda kampuni nyingine wakitumia haki yao ya kifungu cha 15.12 cha Mkataba. Hii ndiyo barua ambayo inawafikia TANESCO Disemba 4, 2006. Hapa kuna jambo la kutafakari kidogo. Kwanini barua iliyoandikwa Novemba 9, 2006 iwafikie TANESCO Disemba 4, 2006? Yawezekana iliandikwa baada ya kugundua kuwa mkataba umeshahamishwa kwa Dowans S.A Oktoba 14, 2006 lakini TANESCO hawakuwa na taarifa hivyo walihitaji kutengeneza mazingira ya taarifa?
  5. Pendekezo la nne hapo juu linaonekana lina ukweli kwa sababu ni tarehe 28 Novemba, 2006 ndipo Karamagi anaulizia kama mkataba unaruhusu kuhamishika; na anapoambiwa kuwa haiwezekani isipokuwa kwa ridhaa ya pande zote mbili chini ya kifungu 15.12 ndipo siku sita baadaye (Disemba 4, 2006) barua iliyoandikwa Novemba 9, 2006 inafika TANESCO ikiwa na nia ya ya kuhamisha mkataba chini ya haki za 15.12. Barua hiyo ya Richmond ilisema kuwa kampuni iliyokusudiwa ilikuwa ni Dowans S.A na kuwa kampuni hiyo mpya itajitambulisha yenyewe kwa TANESCO.
  6. Novemba 14, 2006 Dowans S.A inawaandikia TANESCO ikijitambulisha kuwa ndiyo kampuni ambayo imekusudiwa kurithi mkataba wa Richmond na TANESCO. Wakati Dowans S.A inaandika barua hii tayari ilikuwa imeshaingia mkataba na Richmond Oktoba 14, 2006. Lilikuwa jukumu la Richmond na Dowans S.A kuitaarifu TANESCO kuwa mkataba umekwishachukuliwa. Hilo hata hivyo lingekuwa kinyume na kifungu cha 15.12. Dowans iliandika barua kana kwamba ilikuwa haijachukua mkataba huo bado na hivyo kudanganya ili kupata faida ya aina fulani kinyume na sheria yetu ya Mikataba ya 2002. Kuna mambo ambayo TANESCO ingeweza kujua kuhusu kampuni ya Dowans lakini suala la kuwa ilikuwa tayari imekwishaingia mkataba lilikuwa ni suala la kujulishwa na Richmond au Dowans wenyewe. Ni sawasawa na mtu ambaye kwa muda wote wa uchumba na hatimaye siku ya harusi anafunga ndoa akiamini kuwa anayefunga naye ndoa hakuwa tayari amefunga ndoa na mtu mwingine ambayo ilikuwa bado halali kisheria. Ndoa inaweza kufungwa lakini endapo ikaja kujulikana kuwa yule mwingine alificha ukweli kuwa tayari alikuwa katika ndoa halali basi ile ndoa ya pili inafutiliwa mbali (annulled) kwani haikuwahi kuwepo.
  7. Barua ya Dowans ya Disemba 8, 2006 inaondoa shaka kabisa kuwa Dowans waliwaficha TANESCO ukweli kuwa tayari kampuni ya Costa Rica ilikuwa tayari imekwisha funga “ndoa” na Richmond kuchukua mkataba wake na TANESCO bila ridhaa ya kimaandishi na TANESCO. Barua hii kwa mujibu wa hukumu ya ICC (kifungu cha 517) iliomba kibali cha kuhamisha mkataba na kutoa taarifa mbalimbali kuhusu kampuni hiyo na kampuni ya Portek Group.

Ni kutokana na mabo hayo hapo juu ndipo tunaona makosa makubwa ya hukumu ya ICC. Hukumu hiyo kifungu cha 518 ambacho kinatupilia hoja ya “kutokuwa wa kweli” iliyotolewa na TANESCO dhidi ya Dowans inadai kuwa yote yaliyosemwa kwenye barua hayo yalikuwa ni kweli (factual). Hukumu hiyo inasema kuwa “based on the evidenced presented before the Tribunal, all these (yale yaliyodaiwa kwenye barua ya Disemba 8, 2006) representations were proven to be factual – what the letter of 8 December purpoted to present was actually in the dossier accompanying the letter. This is substantiated by the fact that the Tribunal was presented with evidence that DHSA and RDVECO requested the consent of TANESCO to the assignment (of the contract)”

Hukumu hiyo ikadai katika kifungu cha 519 kuwa “based on the evidence adduced before the Tribunal these representations presented in the dossier of 8 December 2006 were statements of fact, were true”. Yaani, “ kulingana na ushahidi uliotolewa katika mahakama yaliyosemwa katika barua ya Disemba 8, 2006 yalikuwa ni madai ya uhakika, yalikuwa kweli”.

Ni kutokana na msimamo huo wa mahakama hiyo hoja kuwa Dowans haikuwa mkweli wakati inataka kuchukua mkataba wa Richmond ilitupiliwa mbali katika kifungu cha 524. Baada ya kutupilia mbali hoja hiyo kwa makosa mahakama hiyo ikaangalia kile ilichoamininishwa kuwa ndio makubaliano ya kuhamisha mkataba toka Richmond kwenda Dowans.

Katika kifungu cha 533 cha hukumu hiyo inaoneshwa kuwa kulikuwa na makubaliano ya kuhamishia mkataba kati ya TANESCO na Richmond kwenda Dowans kwa barua iliyoandikwa Disemba 21, 2006 (kama tulivyoona hapo juu). Na hili lilikuwa kweli kwani ni tarehe 23 Disemba, 2006 mkataba huo ukapelekwa kwa Dowans. Na hata uamuzi wa baadaye wa TANESCO kukubali mkataba uhamishiwe toka Dowans S.A kwenda Dowans Tanzania Limited ulitegemea uhalali wa kitendo cha Disemba 21 na 23, 2006.

Hili linaturudisha kwenye hoja ya msingi kabisa ambayo inatufanya tuulize maswali yafuatayo:

a. Kama Richmond ilikuwa tayari imeshahamisha mkataba wake na TANESCO kwenda Dowans S.A Oktoba 14, 2006 ni kitu gani kilikuwa kinafanyika kwa majadiliano ya kuanzia Novemba 9 hadi TANESCO kukubali kuhamishwa mkataba Disemba 21, 2006?
b. Richmond ilipowasiliana na TANESCO kueleza nia yake ya kutaka kuhamisha mkataba kwenda Dowans wakati tayari ilikuwa tayari imeshauhamisha mkataba huo kisheria kwanini haikuweka wazi jambo hilo kwa TANESCO kama kifungu cha 15.12 kinavyotaka?
c. Kampuni ya Dowans S.A ililipia na kuingiza mitambo ya kuzalishia umeme mwishoni mwa Oktoba 2006 baada ya kufanya hivyo ikiamini inatekeleza makubaliano yake na Richmond ya Oktoba 14, 2006 yaliyohusisha kurithi mkataba wa TANESCO na ule wa Vulcan. Kwa maneno mengine, Dowans ilianza kutekeleza mkataba wake na Richmond ikiamini ilikuwa inatekeleza mkataba wa TANESCO. Kwanini, Dowans haikuiambia TANESCO kuwa imechukua mkataba kutoka Richmond na badala yake kutenda kana kwamba ilikuwa haijapata mkataba huo bado?
d. TANESCO isingeweza kujua kwa namna yoyote ile kuwa Richmond imeshaingia mkataba na Dowans Oktoba 14, 2006 isipokuwa kwa kuambiwa na Richmond yenyewe na Dowans S.A. Ni kwa sababu hiyo uongozi wa TANESCO ulijitahidi kuzuia mkataba kuhamishwa lakini wakajikuta “wanasukumizwa” na Wizara na hatimaye kukubali. Ukweli ni kuwa TANESCO hawakuwa na njia nje ya hapo kwani mkataba tayari ulikuwa umeshahamishwa.

Kutokana na haya yote ambayo tunayo sasa hivi na tunayajua kwa uhakika ni kitu gani kinahalalisha kuwalipa kampuni ya Dowans S.A? Kwa vile tayari wamekwishalipwa zaidi ya bilioni 100 hadi hivi sasa na bado majenereta ni yao na kuna dalili kuwa wanapanga kuyakodisha tena kwetu kupitia kampuni nyingine ni wazi kuwa ni viongozi gani wenye dhamira safi katika Tanzania wanaoweza kuhalalisha malipo ya bilioni 94 zaidi? Mkataba wenyewe wa miaka miwili ulikuwa ni wa bilioni 172.5 (japo majenereta yenyewe kuyanunua moja kwa moja ilikuwa chini ya bilioni 60) na tukilipa bilioni 94 kama ilivyoamuriwa na serikali ni wazi kuwa kampuni ya Dowans S.A na washirika wake watakuwa wamekomba zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa majenereta ya bilioni 60! Hiki ni kilele cha ufisadi, ni kutamalaki kwa uzembe na kutukuzwa kwa kutokuwajibika.

Kutokana na uzito wa ushahidi ambao tumeupendekeza mbele ya wasomaji na Watanzania wenzetu tunajikuta tunabakia na mapendekezo yafuatayo tu:

a. Serikali isilipe hata senti moja na iamue kujitoa kwenye Mahakama ya Usuluhishi na badala yake Bunge letu liimarishe sheria zetu za usuluhishi wa kibiashara ili mikataba yote inayohusiana na umma inapotokea matatizo iamuliwe kwa sheria zetu wenyewe.
b. Mitambo ya Dowans ambayo tayari tumeshalipia zaidi ya gharama yake kuiingiza nchini ikamatwe na kutaifishwa kwa kutumia madaraka ya Rais (Executive Order) au kwa sheria nyingine yoyote ile.
c. Watendaji wote wa Dowans S.A na Dowans Tanzania Limited ambao walikuwepo wakati Dowans S.A inarithi mkataba wa TANESCO kutoka Richmond kwenye makubaliano ya Disemba 23, 2006 watimuliwe nchini, watangazwe kuwa ni “watu wasiotakiwa” personae non grata. Wapewe si zaidi ya masaa 24.
d. Rostam Aziz ambaye ndiye amekuwa kinara wa kuitetea Dowans na ambaye mapema mwaka huu (Januari 5, 2011) alikiri kuwa yeye ndiye aliyewashawishi Dowans kuja nchini na ambaye ndiye aliyepewa nguvu ya kisheria (Power of Attorney) kutumika kwa niaba ya Dowans Holdings S.A alikuwa anajua na alipaswa kuwa anajua kuwa Dowans S.A walikuwa tayari wamechukua mkataba wa Richmond na TANESCO. Akiwa ni Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye aliapa kulinda na kutetea sheria na Katiba ya nchi yetu alipaswa kuonesha uzalendo kwa kuitaarifu TANESCO (shirika la umma) juu ya jambo hilo. Akiwa ni mtu ambaye angenufaika kwa namna moja au nyingine na uwepo wa Dowans nchini (akiwa ni mshirika na rafiki wa mmoja ya wamilikiwa wa Dowans S.A) Rostam hakuliweka na hadi hivi sasa hajaweka Tanzania mbele katika suala hili. CCM inatakiwa imvue uanachama na serikali imshtaki kwa makosa mengi ambayo tungeweza kuyafafanua kutokana na kushiriki kwake.
e. Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Bw. Nazir Karamagi naye ahojiwe na ikibidi ashtakiwe kwa kushiriki kwake kuificha TANESCO ukweli kuwa mkataba wa TANESCO kuhamishiwa kwa Dowans S.A na Richmond. Bw. Karamagi alijua alipaswa kujua kuwa mkataba ulikuwa umekwishahamishiwa kwenda Dowans kutokana makubaliano ya Oktoba 14, 2006. Kwani, ni yeye aliyetoa taarifa kwa TANESCO juu ya nia ya Richmond kuhaulisha mkataba wake kwenda Dowans S.A na alisisitiza kuwa iwe hivyo licha ya mapingamizi ya Shirika hilo la Ugavi.
f. Mwanasheria Mkuu wa Tanzania awajibishwe kwa kutetea malipo haya ambayo ni wazi ni kinyume cha sheria.
g. Huduma yote iliyotolewa na majenereta ya Dowans S.A ichukuliwe kuwa ni huduma ya bure kwani Mkataba uliosainiwa Disemba 23, 2006 haukuwa na maana yoyote kisheria kwani Dowans S.A ilikuwa imekwishajifunga kinyume na kifungu cha 15.12 na Mkataba wake na Richmond wa Oktoba 14, 2006. Ukweli huu uko wazi kwani katika kesi yake dhidi ya Richmond huko Houstona Marekani, Kampuni ya Dowans haitaji kabisa mkataba wa Disemba 23, 2006 bali inatambua kuwa iliingia makubaliano na Richmond ya kuchukua mkataba wa TANESCO tarehe 14, Oktoba 2006.
h. Watanzania wote wenye dhamiri njema wapinge kwa nguvu na namna zote malipo haya ya kidhalimu na kutaka wale wote waliojitokeza kuyatetea wawajibike wao wenyewe au wawajibishwe na vyombo halali. Malipo haya ni kinyume na maadili, ni ya kimabavu na yanadhalilisha utu wa Mtanzania.

Niandikie: [email protected]

21 Comments
  • MM kuna hoja hapo tatizo ni taratibu na mfumo wa kuwasilisha haki ikatendeka. Mshikamano wa wenzetu CCM ndio unazaa matatizo yote. Napendekeza mawakili binafsi wakujitolea wafuatilie hili jambo kwa sababu serikali kupitia mwanasheria mkuu is party to the conspiracy

  • uchambuzi na ulinganifu mzuri, tatizo hamna uthibitisho wa mkataba wa tarehe 14.Oktoba 2006 kati ya RDEVCO na DHSA. mkataba huo ndo msingi wa hoja hii hapa, kama hatuoni huo uthibitisho tutaaminije kwamba hiyo siyo random date iliyochaguliwa na mtoa hoja?

    • Huduma yote iliyotolewa na majenereta ya Dowans S.A ichukuliwe kuwa ni huduma ya bure kwani Mkataba uliosainiwa Disemba 23, 2006 haukuwa na maana yoyote kisheria kwani Dowans S.A ilikuwa imekwishajifunga kinyume na kifungu cha 15.12 na Mkataba wake na Richmond wa Oktoba 14, 2006. Ukweli huu uko wazi kwani katika kesi yake dhidi ya Richmond huko Houstona Marekani, Kampuni ya Dowans haitaji kabisa mkataba wa Disemba 23, 2006 bali inatambua kuwa iliingia makubaliano na Richmond ya kuchukua mkataba wa TANESCO tarehe 14, Oktoba 2006.

      • nashangaa watu wa Tanesco kushindwa kujenga hoja nzito na makin za utetezi, kupishana kwa tarehe za kusaini mikataba hiyo, ni misrepresantation of facts, ni kosa kisheria

  • Honestly ukisoma uchambuzi hapo juu kuna vitu vingi ambavyo vilikuwa siri. Na hii inatokana na mikataba yetu kufichwa ndiyo maana kunakuwa na madudu.
    Kitu kingine ni pale Tanesco wakijua kabisa kuwa wanashinikizwa kufanya kitu ambacho ni against their will ilitakiwa either wajiuzuru au wakatae ili maamuzi yatoke juu si kwao.
    Napendekeza katika watu wa kuchukuliwa hatua hata watendaji wa Tanesco wanatakiwa wapewe quinin yao.
    Huyu RA ni mbunge kivuri yuko pale ili kuficha makucha yake. Lakini jamaa kwa kweli anatisha sana. Maana haya mambo ni mazito ulifanyia taifa, then ka% unawapelekea IGUNGA kule wagombanie ili waimbe kuwa anawajali.
    Kalamagi, EL, Richmond, RA, TANESCO wachukuliwe hatua maana wao ndiyo walituingiza kwenye MKATABA WA KIMAFIA. HATUA KALI ZICHUKULIWE.

  • Haya yote yanafanywa na viongozi wetu makusudically wakijua kuwa wa-Tz ni watu wakupelekwapelekwa tu, tofauti na nchi zingine. Na, hiyo inatokana na kupanda bei kwa kila hitaji la msingi la mwanadamu kila siku hapa Tanzania.

    Tumeona nchi za wenzetu jinsi ambavyo ongezeko la bei kidogo tu linavyoweza kuwatoa madarakani watawala wa nchi husika, kwa kutumia nguvu ya umma (maandamano) lakini siyo hapa kwetu Tz.

    Hii maana yake nini? maana yake ni kuwa baada ya viongozi wetu kuona tunakubali kupelekwa pelekwa sasa wameamua kupiga DEAL ya kikwelikweli (DOWANS) kuona je, tutafanyaje.

    Wito kwangu watz tuamshe MAANDAMANO nchi nzima, ili tupinge jambo hili pamoja na mengine yooote, likiwemo hata lile la jamaa zetu POLISI kuondolewa baadhi ya posho zao, nahata kupanda kwa gharama za UMEME.

    shime watz tuamke sasa mbona EGYPT na TUNISIA wameweza je, ninani aliyeturoga sisi?

  • KATIKA HILI SWALA MWENYE RUNGU LA KUWASHTAKI AU KUTAIFISHA MASHINE ZA DOWANS NI KIKWETE. ILA SASA KAMA MNAVYOMJUA KIKWETE NA ROSTAM NI PETE NA KIDOLE NI SHEMEJI YAKE NA UENDA HATA NAE KWENYE IO KAMPUNI YUMO INGAWA HAWEZI KUJITAJA KWA SASA. IVYO SIO RAHISI RAIS KIKWETE AU CHAMA CHAKE CHA MAFISADI KUCHUKUA HATUA YOYOTE ILE. KIKWETE HAWEZI KUMGUSA ROSTAM WALA LOWASA. HIVYO NI JUKUMU LETU SISI WENYE NCHI HII, TUNAONEWA NA KUONEKANA WAJINGA KUAMKA BILA KUOGOPA CHOCHOTE KILE WAWE POLISI AU KIKWETE NA MAFISADI WENZI. TUSIOGOPE KUPIGWA MABOMU AU KUULIWA KUMBUKA UNAPOPIGANA KUNA MAWILI KUFA AU KUPONA LAKINI TUSIWE WAOGA TUAMKE SASA,TUNARASILIMALI NYINGI SANA LAKINI TIZAMA KILA SIKU NI SERIKALI WANAIBA NA KUJENGA MAHEKALU NA KAMA HAITOSHI BADO WANATUONGEZEA KAMA HAYA YA DOWANS YANI WACHUKUE CHOCHOTE KILE ULICHONACHO. NILIKWISHA SEMA HUKO NYUMA. TUKIMNGOA ROSTAM TANZANIA ITAKUWA NA AMANI. ANA MAKAMPUNI ZAIDI YA MIA ZA MIFUKONI HALAFU BADO YUKO KWENYE BUNGE NA UNAKUTA WANACCM WANAMSIFU NA KUMWIMBA. TUAMKE KAMA TUNISIA,MISRI BILA HIVI WATANZANIA TUTATESEKA NA MAFISADI WATAONDOKA. HILI SUALA LIKIWA MBAYA KWA ROSTAM UTAMWONA ANAPANDA NDENGE NA KUONDOKA SIO MTANZANIA. WATANZANIA TUANDAMANE KUIKATAA SERIKALI YA MAFISADI TUSINGOJE KESHO TUANZE LEO KUDAI HAKI KWA WOTE. ANGALIA WATOTO WA WALALAHOI WALIVYOFELI. UKOMBOZI NI SASA TIZAMENI KWA WAAFRIKA WENZETU WA TUNISIA,MISRI. TUSILALE MPAKA KIELEWEKE

  • Hapa inaonyesha kuwa serikali imeshikwa na matajiri, wanajisikia kulifanya ndilo huwa. Nguvu ya umma tu ndio itakuwa dawa, lakini inabidi watanzania waelewe maana yake, maana wengi ni waoga halafu wanaridhika upesi wakipewa katishirt, kofia , kanga n.k hawasikii wala hawaoni.Nani alijuwa kuwa leo Misri, Tunisia, Yemen wataandamana kushinikiza utawala uondoke madarakani? tena nchi hizo maisha yao huwezi kulinganisha na umaskini tulio nao sisi.

    Faulo iliyochezwa tarehe 31.12.2010 kuwaresha madarakani tena jamaa lazima tuitafakari, maana hawa jamaa wana mtandao mkubwa, dawa ni kung’oa woote, leo dowans kesho waliochomewa ofisi zao za miwa, keshokutwa ataibuka mwingine tutamlipa, nasema tutamlipa kwani ni sisi walala hoi tunaumia, mabilioni yaliyoweza kujenga barabara ngapi, au kungelipa wadai wangapi leo zinashurutishwa tena haraka kulipwa kwa mijitu michache isiyotosheka.

    Jamani sasa kila mtu kwa aombe Mwenyezi Mungu kwa imani yake kwa DHATI ili aingilie kati, yeye anaweza yeye ni mwenye haki hata kama hao waliofanya ni wana ibada PIA lakini haki ya Mungu inasimama PALEPALE haijalishi wanatoa sadaka kubwa kwenye sehemu zao za ibada, sauti ya wengi itavuta HURUMA ZA MUNGU atatutokea kwa namna yake.

  • umeandika kwa kirefu sana maelezo yako. kwa mtazamo wangu masuala ( issues ) hapa ni zifuatazo:-
    1. je tulikuwa na shida ya umeme 2006 iliyolazimisha kutafuta ufumbuzi wa dharula?

    2. kama mkataba ulikuwa na kifungu kinachoruhusu kuhaulishwa kwa mkataba dhambi iko wapi hasa ukizingatia kuwa upande mpya katika mkataba ulikuwa na uwezo mkubwa kuliko ule wa zamani na uliweza kuleta mitambo tuliyo kuwa tunaihitaji.

    3. kama mkataba usingehaulishwa tungerudi katika mstari wa huanzia na kuanza kutangaza zabuni upya jambo ambalo si kwa masilahi ya watumiaji wa umeme.

    4. shida yetu ilikuwa ni kupata umeme megawati 100 na hao “mashetani” dowans waliweza kutupa umeme huo na wateja wa tanesco nina hakika walilipia. sasa kwanini dowans wasilipwe haki yao. mtoto wa baba ambaye si wa ndoa atabaki kuwa baba halali wa mtoto hata kama atapigwa mawe hadi kufa kwa kumzalisha mke wa mtu

    5.kama azizi anakubali kuhusika na mwenye mali anajitaja dhambi iko wapi?

  • Nimeisoma vizuri sana ripoti ya jinsi richmond na dowans zilivyoizunguka ila sijaelewa kiundani ni vipi Mh.aliyejiuzulu kutajwa kama ndiye mhusika na sakata zima na kutakiwa kuachia ngazi?

    Kwahiyo Mh.Sana aliyejiuzulu ili kunusuru taifa hana kosa lolote? mahana hata kesi za wahusika wanaoitwa mahakamani sijasikia Bwana Mkubwa akiitwa hata kama mshahidi tu! Naomba niweke sawa hapo maana hata watanzania wapo gizani sana kuhusu hili.

    “An Idle Mind is the Workshop of Devil”

  • Swala hapa ni Waziri Ngereja aji hudhuru kwa sababu hili swala lilitoke wakati yeye ni Waziri wa nishati hiyo, ili iundwe kamati mpya labda tutapona na mgao wa umeme, na akiji hudhuru wachukuliwe hatua sio watu ibie halafu wanajiudhuru ndo utakua mchezo, TANZANIA BILA MGAO WA UMEME INAWEZEKANA.

  • napenda kuona watazania wanahuwezo wa kuchukua hatua embu serikari hilipe hilo deni tujuwe nn kinafwata tusiwe mabingwa wa kusema tu

  • MBONA WAHUSIKA HAWASHTAKIWI ACHENI USANIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIII TUMECHOKA

  • NI Vizuri kusema sasa basi sasa basiiiii!!! Lakini (TANZANIA-
    Mungu katujaalia shida hata kama nasema mtaumia sifa hii ilianza zamani mimi nilikuwa nalaani sana utumwa kwamba watu waliteswa na kuuzwa ughaibuni lakini kumbe sio kweli walikwenda kwa hiyari yao tena na amini ilikuwa sifa kubwa mtu kwenda utumwani unaombewa kwa mungu na baba yako pia mama yako mzazi anakuabiaa mwanangu nenda salaama hii ilikuwa enzi hizo mungu ibariki TANGANYIKA
    Sasa ukoloni ukasema biashara hii basi watu wengi walichukia hawakuwa nalakufanya bali kuukubali ukoloni yani utumwa wa hapa hapa NKURUMA, NYERERE, LUMUMBA,
    NASSAR ,KENYATTA , Wakakataa ukoloni watu wengi pia wakachukia lakini hawana lakufanya uhuru wakapewa hao wote niliyo watajaa na wengine wakaiga nao wakapewa lakini tuliyo wengi baado tunasononeka kwanini tusirudi kwenye utumwa kwanza tutakula bure ,nguo bure, treni bure, pesa bure halaafu matibabu bure sisi kazi yetu sikubeba mizigo kwani hiyo kazi ngumu bona kazi poa
    sasa Serikali Karibu Zote Africa wamekubali kurudi kwenye utumwa ili waweze kula na kustarehe wao n watoto zao kama vile zamani mikataba hii ni uthibitisho tosha kwamba safari ya kurudi utumwani haipingikii wachache ndiyo baado mnaleta kelelee za hovyo kwani RICHMOND,DOWANS,
    Wakipewa billion 200 wewe utakosa nini haya mambo
    wewe unahoji hoji nini
    MUNGU IBARIKI AFRICA,
    MUNGU IBARIKI TANZANIA

  • Kweli hii nchi tumebaki kuzulumiwa resourse zetu halafu tuko kimya tu watanzania!! Dowans hatakiwi kulipwa kabisaa!!!!

  • Sasa kama haya yote yapo wazi na tuanao wanasheria makini wa kupresent haya kwa nini hayashughulikiwi? Nchi ipo katika hali mbaya kiuchumi halafu tunawalipa watu pesa za bure wakati wao ndio walitakiwa watulipe.

  • Na aamini hatujachelewa ipo siku tutalia na kusaga meno.

    Yatupas tunguke tuilinde nchi yetu. Tumsaidie mweshimiwa Rais katika haya yanayotokea na tutoe ushauri wa busara namna ya kuyatekeleza na kuyasimamia yote haya yatakwisha.

    Kumbukeni nchi yetu tu ndio iliyobaki tukvurugika na sisi basi tumeliwa na hatutkaa tusahau. Ole wenu mnaotia aibu taifa, ole wenu siku zenu zinahesabika na njama zenu zimegundulika. Tamaa kubwaaa zote za nini wewe mtu wa kufa na vyote mtaviacha. Ebu imarisheni upendo.

    Mambo yote Richomod yalipangwa na wajanaja wachache njia nzuri nikuwafirisi sheria itafuata baadaye wakati walishakufa.

  • Wananchi hasa wanyonge wajue kuwa nchi hii ni yetu sote masikini kwa matjiri lakini wachache wandhani wana hatimiliki yake umoja wetu bila uoga ndiyo mwokozi wetu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *