KANUMBA, UNCLE JJ, KWELI KAZI YA MUNGU HAINA MAKOSA! MASIKINI LULU MATATANI

Jamii Africa

“…LAKINI Mola eeeh, kazi yake haina makosa; wala hairekebishiki na binadamu yeyote!…” Ndiyo maneno ambayo yanaweza kutumika kuhitimisha majonzi ya Watanzania wengi kuhusiana na kifo cha ghafla cha mwigizaji, mtundi, mtayarishaji na muongozaji nguli wa filamu nchini, Steven Charles Kanumba.

Marehemu Kanumba

Taarifa kwamba Kanumba amefariki dunia zimepokelewa kwa mshtuko mkubwa na Watanzania, hususan wapenzi wa filamu za Tanzania, na mshtuko huo umewapata Jumamosi alfajiri wakati wakijiandaa na matayarisho ya Sikukuu ya Pasaka.

Marehemu Steven Kanumba alifariki Usiku wa kuamkia Jumamosi, Aprili 6, 2012, baada ya kuanguka. Sababu za kifo chake hazijaelezwa wazi pamoja na kuwapo taarifa za kuwapo ugomvi kati yake na msichana Elizabeth Michael maarufu kwa jina la Lulu, ambaye pia ni msanii kijana. Lulu ambaye naye amekutwa na majeraha madogo, anashikiliwa na polisi kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo.

Tanzania nzima iligubikwa na simanzi ya ghafla alfajiri hiyo huku mashabiki na wapenzi wa filamu, hata wale wasio na mapenzi ya filamu za Bongo, wakipiga simu huku na huko kutaka kuthibitisha kama kweli Kanumba, ambaye alipenda kujiita ‘The Great’, alikuwa amefariki dunia.

Kanumba, ambaye alikuwa amejizolea sifa na kupachikwa jina la Uncle JJ kufuatia filamu aliyoigiza kwa jina hilo, amewaacha Watanzania wengi midomo wazi kutokana na kifo hicho ambacho chanzo chake, kwa mujibu wa taarifa za awali, kilitokana na kujigonga kichwa wakati wakinyang’anyana simu na mpenzi wake.

Kwa kifupi, hakuna msima usio na sababu, na hiyo inaweza kuwa sababu tu ya ‘kuhalalisha’ kifo chake ingawa ukweli ni kwamba, anayeijua siri ya binadamu ni Mwenyezi Mungu pekee. Itoshe tu kusema kwamba, huenda siku yake ilikuwa imetimia, kwa sababu hakuna mtu ambaye ameweza kuiona kesho.

Wasanii wengi wamemwelezea Kanumba kama mtu aliyekuwa mpole, mcheshi na aliyependa kushirikiana na yeyote bila kubagua, hali iliyomfanya ajijengee jina kiasi cha kuvuka mipaka ya Tanzania na kuigiza na wasanii nyota wa kimataifa, akiwemo Ramsey Noah wa Nigeria.

Aliwapenda watoto, na hili linadhihirika katika filamu zake kadhaa ambapo anaonekana siyo tu vile anavyoigiza nao, lakini kitendo cha kuwachukua kutoka kusikojulikana na kuwaibua kwenye tasnia ya filamu na kuwa nyota kama alivyofanya kwa Jeniffer kinaonyesha ni kwa jinsi gani hakuwa mwigizaji katika mapenzi ya watoto.

Filamu kama Uncle JJ, This Is It, na Big Dad, zinathibitisha haya, kwani amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwasilisha ujumbe kwa hadhira yake kutokana na mambo yanayotokea ndani ya familia.

Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu

Steven Kanumba alizaliwa Januari 8, 1984 mkoani Shinyanga na alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Bugoyi na baadaye kujiunga na shule ya sekondari Mwadui, kabla ya kupata uhamisho kuja Dar es Salaam alikojiunga na shule ya Dar Christian Seminary. Alifanikiwa kufaulu na kujiunga na shule ya sekondari Jitegemee kwa masomo ya kidato cha tano na sita.

Akiwa Jitegemee ndipo alipoanza shughuli za uigizaji katika kikundi cha shule, lakini alikuja kufahamika zaidi kuanzia mwaka 2002 baada ya kujiunga na kundi la maigizo la Kaole Sanaa Group la Magomeni, jijini Dar es Salaam alikowakuta akina Vincent Kigosi ‘Ray’, Mzee Kipara, Rajab Hatia ‘Mzee Pwagu’, na wengineo wengi.

Tamthiliya ambazo amewahi kuigiza akiwa na kundi la Kaole ni pamoja na Jahazi, Dira, Tufani, Gharika na Baragumu, ambamo alifanya vizuri na kutengeneza ushirikiano wa ‘mapacha watatu’ yeye, Tay na Frank.

Baada ya kudumu na kundi hilo kwa muda akiigiza tamthiliya zilizokuwa zikirushwa kwenye kituo cha televisheni cha ITV, hatimaye akawa miongoni mwa wasanii wa kwanza kabisa kuanza kuigiza filamu na kuisimamisha mpaka ilipo sasa.

Filamu ya kwanza ambayo alishiriki kuiandaa na kuigiza ni ya Johari, ambayo iliwapatia umaarufu mkubwa yeye, Ray na mwanadada Blandina Chagula ‘Johari’ ambaye walikuwa wote Kaole.

Kanumba, ambaye alikuwa akijiandaa kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2005, ameigiza filamu nyingine nyingi miongoni mwazo zikiwemo Sikitiko Langu, Johari 2, Dangerous Desire, Dar 2 Lagos, Riziki, Cross my Sin, Uncle JJ, This Is It, Big Dad, Village Pastor, pamoja na Devils Kingdom ambayo amemshirikisha Ramsey Noah.

Miongoni mwa filamu hizo pia ameshiriki kutunga, kutayarisha na kuziongoza, na kazi zake zimeonekana kuwa bora kimataifa kiasi ambacho ameweza kuitangaza vyema Tanzania.

Mbali ya kutunga na kuigiza filamu, lakini Kanumba alikuwa na kipaji cha kutunga na kuimba muziki, ingawa kazi zake zilikuwa bado hazijarekodiwa katika kiwango stahiki.

Walinena waliosema, ‘Wema hawana maisha’, na kwa kweli wema wa Kanumba utabakia kuwa simulizi daima kwani amekwishaikamilisha kazi yake.

BWANA AMETOA, BWANA AMETWAA, JINA LA BWANA NA LIHIMIDIWE! AMINA.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania –TAFF- kuomboleza kifo cha msanii maarufu nchini Steven Charles Kanumba, aliyeaga dunia usiku wa kuamkia leo, Jumamosi, Aprili 7, 2012.

Katika salamu hizo, Rais Kikwete amemwomba kiongozi huyo wa TAFF kufikisha salamu za rambirambi za dhati ya moyo wake kwa wana-familia ya Kanumba na kwa wasaani wote nchini ambao wamepotelewa na mdau na mwenzi wao.

Rais Kikwete amesema kuwa ameshtushwa na kuzunishwa na kifo cha msanii huyo ambaye amemwelezea kuwa msanii mahiri na mwenye kipaji kikubwa ambaye katika uhai wa maisha yake mafupi na akiwa bado kijana sana amechangia kwa kiwango kikubwa maendeleo ya sanaa ya filamu nchini na kupitia sanaa hiyo kuitangaza Tanzania kimataifa.

Amesema Rais: ”Nimepokea kwa mshtuko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Ndugu Steven Charles Kanumba. Kupitia filamu zake, ameburudisha na kuelimisha jamii yetu kwa namna ambayo haiwezi kupimika. Alikuwa msanii mahiri na mwenye kipaji kikubwa ambaye mchango wake mkubwa katika kuanzisha, kukuza na kuimarisha sanaa ya filamu nchini hautasahaulika.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Ndugu Kanumba pia ametoa mchango mkubwa katika kuitangaza nchi yetu ya Tanzania mbele ya mataifa mengine kupitia sanaa ya filamu na uwezo mkubwa wa kisanii. Tutaendelea kumkumbuka kwa mchango wake huo kwa nchi yetu.”

Nakutumia wewe Rais wa TAFF salamu zangu za rambirambi na kupitia kwako kwa wasanii wote wa filamu na sanaa nyingine kufuatia msiba huu mkubwa kwa fani yetu ya sanaa. Aidha, naomba unifikishie salamu za dhati ya moyo wangu kwa wanafamilia wote. Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa. Waambie naelewa machungu yao katika kipindi hiki kigumu cha msiba,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

Namwomba Mwenyezi Mungu awape subira na nguvu za kuweza kuhimili kipindi hiki kigumu kwa sababu yote mapenzi yake. Aidha, naungana na wana-familia na wasanii wote nchini kuwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema peponi roho ya Marehemu Steven Charles Kanumba. Amen.”

……………………………

 

7 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *