Kwa muda mrefu sasa intaneti imekuwa ni jukwaa muhimu la kuwaunganisha watumiaji wa mitandao ya kijamii duniani kote; kupashana habari na kupadilishana uzoefu wa kijamii, kiuchumi, kisiasa na hata kiutamaduni.
Lakini habari sio njema kwa watanzania wanaotumia majukwaa ya mtandaoni kwasababu serikali imeweka baadhi ya vikwazo kwa watu kuwa huru kutoa maoni na kupata habari kupitia blogu (blog) ambapo waanzilishi watatakiwa kulipa kiasi kisichopungua milioni 1 Ili wapate leseni ya kuendesha shughuli zao.
Malipo hayo ni sehemu ya masharti ya Kanuni mpya za maudhui ya mtandaoni ambazo zimepitishwa hivi karibuni na serikali. Waanzilishi wote wa blogu watatakiwa kupata kibali toka serikalini na kulipa ada ya mwaka kabla ya kuanza shughuli za mtandaoni.
Kanuni hizo mpya pia zitawahusu wamiliki wa redio na runinga za mtandaoni (online TV’s) ambapo hatua hiyo inatajwa kuwa itawaathiri kwa kiasi kikubwa watumiaji wa majukwaa na mitandao ya kijamii.
Athari mojawapo ni kukosa uhuru wa kujumuika na kupata taarifa kutokana na ada itakayotozwa na serikali kila mwaka; ikizingatiwa kuwa blogu nyingi hazitengenezi faida na zimewekwa mahususi kwaajili ya kuwakutanisha watu kujadili mstakabali wa maisha yao.
Kwa mujibu wa Kanuni hizo ili mtu akubalike kutoa huduma, muombaji atalazimika kujaza fomu inayoelezea gharama tarajiwa za uwekezaji, idadi ya wakurugenzi, na wana hisa wa jukwaa husika (blogu). Pia kila mwana hisa anapaswa kuainisha mtaji aliochangia kwenye huduma husika, tarehe ya kuanza kufanya kazi na mipango ya baadaye ya ukuaji wa blogu.
Licha ya mamlaka husika kutoa kibali au leseni ya kuendesha blogu, pia ina nguvu kisheria kunyang’anya kibali/leseni ikiwa tovuti au blogu itachapisha maudhui yanayodhaniwa ‘ kusababisha au kuhatarisha amani, kuchochea machafuko au uhalifu’ au ‘yanatishia usalama wa taifa au afya na usalama wa umma’.
Waliopewa mamlaka ya kusimamia maudhui ya mtandaoni ambao ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) watakuwa na uwezo wa kuwalazimisha wamiliki wa blogu au tovuti kuondoa maudhui yanayodhaniwa kuwa hayafai ndani ya saa 12 na kama hawajatimiza maagizo hayo wanaweza kulipa fidia isiyopungua milioni tano au kifungo kisichopungua mwaka mmoja jela.
Kanuni hizo ambazo zinatajwa kuwa ni tishio kwa uhuru wa kujieleza nchini, zimepewa jina la Kanuni za Maudhui ya Mtandao za mwaka 2018 (Electronic and Postal Communications (Online Content) Regulations 2018). Kimsingi zinaipa serikali nguvu zisizo na mipaka za kusimamia mitandao.
Kanuni hizo zinaongeza nguvu juu ya Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015, Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wadau wa maendeleo kuwa ni mkakati wa kudhoofisha uhuru wa kutoa maoni, uwazi na uwajibikaji nchini.
Tangu zilipopendekezwa mwaka jana, wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu ikiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiForums, Maxence Melo walijitokeza na kuhoji baadhi ya vipengele ambavyo vilionekana kukiuka faragha za watu, kuminya uhuru wa wananchi kujieleza na kutoa maoni. Pia zinaenda kinyume na utamaduni wa kuifanya intaneti kuwa huru.
Kwa muktadha huo wamiliki wa vibanda vya intaneti (intaneti cafes) watalazimika kufunga kamera za CCTV ili kurekodi matukio yote kwenye maeneo ya biashara zao ili kuhakikisha kunakuwa na kumbukumbu sahihi.
Gharama za kuanzisha blogu zinatajumuisha, ada ya maombi (100,000), ada ya leseni (milioni 1), ada ya mwaka (100,000) ambapo leseni itatumika kwa miaka 3 na baada ya hapo muhusika anaweza kulipia sh. Milioni 1 ili aendelee kutoa huduma.
Kwa upande wa runinga za mtandaoni watalipa zaidi ya milioni 2, huku redio za mtandaoni nazo zitalazimika kulipa laki nne na elfu sababini ili kuendelea kutoa huduma hizo.
Hatua hizo zinadaiwa kuwa ni muendelezo wa serikali kudhibiti uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza ambapo kwa kutumia sheria ‘tata’ baadhi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii wamefikishwa kwenye vyombo vya dola kwa makosa ya ‘uchochezi’.
Kulingana na taasisi ya Freedom House (2018) inaeleza kuwa misingi ya demokrasia ikiwemo uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kukusanyika imeendelea kudhoofika nchini Tanzania na hali hiyo isiporekebishwa itaingia kwenye kundi la nchi zisizo na uhuru kabisa duniani.
Tahadhari hiyo inatokana na mwenendo wa viongozi wa serikali kufungia vyombo vya habari, kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, kushtakiwa kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii kwa tuhuma za uchochezi na kukamatwa kwa wapinzani wa kisiasa ambao wanakosoa na kutoa mawazo yanayotofautiana na serikali.
Tumeshuhudia magazeti yakifungiwa kwa kile kinachodaiwa kuwa yanaandika habari za uongo ambazo zinalenga kupotosha na kuchochea ubaya ndani ya umma. Mpaka sasa magazeti yamewahi kufungiwa katika awamu ya tano ya uongozi ni Tanzania Daima, MwanaHalisi, Mawio, Raia Mwema na Mseto.
Baadhi ya runinga na radio nazo zimekuwa zikipewa maonyo ya mara kwa mara ili kuziweka katika mstari unaotakiwa. Hali hiyo imeelezwa kuwa inahatarisha uhuru wa vyombo vya habari na haki ya wananchi kupata taarifa.
Haya yote yanatokea Tanzania, ambako juhudi mbalimbali za kuinua sekta ya teknolojia ya mawasiliano na habari zinaendelea ili kushindana na nchi jirani za Afrika Mashariki kama Kenya. “Masharti ya usajili na ada yanaonekana kuwa mzigo mkubwa kwa waanzilishi wa blogu na runinga za mtandaoni, hatimaye kukamwamisha mchakato wa kuinua uhuru wa habari nchini”, amesema, Angela Quintal, Mkurugenzi wa Kamati ya Afrika ya Kuwalinda wanahabari.
Je kwa YouTube channel ambazo haziposti masuala ya habari nazo zinatakiwa Kulipiwa