Kasi ya wapinzani kuhamia CCM yawaibua wasomi nchini

Jamii Africa

Kutokana na kasi ya wanachama wa vyama vya upinzani kuhama vyama vyao na kukimbilia Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa lengo la kuunga mkono juhudi za rais John Magufuli za kupambana na ufisadi, wachambuzi wa siasa wameitafsiri hali hiyo kuwa ni kutafuta maslahi ya kisiasa.

Hamahama ya wanachama ilishika kasi baada ya Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu kujiuzuru nafasi yake ya ubunge kutoka CCM kwenda Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).  Kuondoka kwake kulifungua milango kwa viongozi wa vyama vingine vya upinzania kuwa na ujasiri wa kujiuzuru nafasi zao za uongozi na kukimbilia katika chama tawala.

Siku chache zilizofuata wanachama kutoka vyama vya upinzani walianza kuingia CCM ambapo mwishoni mwa wiki iliyopita Mbunge wa Kinondoni (CUF), Maulid Said Mtulya alitangaza kujivua uanachama na kuomba ridhaa ya kuingia CCM kwa hoja zinazofanana na wanachama wanaoingia katika chama hicho tawala.

Wachambuzi wa Siasa za Afrika Mashariki wamejitokeza na kusema kasi hiyo inatafsiri nyingi ikiwemo ya ubinafsi na kutafuta maslahi ya kujinufaisha kisiasa ambayo yanatokana na kukosekana kwa utashi wa kisiasa na mfumo wa kisheria unaosimamia haki za vyama vya siasa kuendesha shughuli zao kwa uhuru na uwazi.

Akizungumzia suala hilo, aliyewahi kuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Mwesiga Baregu amesema  ubinafsi wa wanasiasa ambao hauzingatii maslahi mapana ya wananchi ndio sababu inayowafanya wabadilike kila mara na kukimbilia katika vyama vingine ili kutafuta ahueni ya maisha.

“Wanasiasa wengi kubadilika badilika ni ubinafsi wao na kutafuta maslahi ya matumbo yao”, amesema Prof. Baregu wakati akihojiwa katika kipindi cha Meza ya Duara kinachorushwa na redio moja ya kimataifa na kuongeza kuwa siasa za Afrika hazitabiliki kwasababu ya kukosekana kwa umakini wa wanasiasa.

Prof. Baregu ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya CHADEMA, amesema sababu ya pili ni kukosekana kwa ajenda ya kitaifa inayowaunganisha wanasiasa wote katika kutimiza matakwa ya wananchi wanaowatumikia.

Ameongeza kuwa katika awamu ya nne ya uongozi wa rais Jakaya Kikwete, Tanzania iliongozwa zaidi na ajenda ya ufisadi ambapo wanasiasa bila kujali itikadi zao waliungana na kukemea vitendo vya ufisadi. Lakini katika awamu ya tano ajenda ya ufisadi imebebwa na rais Magufuli na kutafsiriwa kuwa wapinzania hawana tena ajenda wanayoisimamia.

Aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni (CUF) kabla ya kuhamia CCM

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, John Shibuda amesema  wanachama kuhama vyama ni sehemu ya demokrasia lakini hali hiyo ni matokeo ya wanachama kutokuelewa vizuri misingi na itikadi za vyama vyao na jinsi ya kuzitetea mbele ya wananchi ili wapate ridhaa ya kuongoza dola.

Shibuda ambaye pia  ni mwanachama wa Chama Tanzania Democratic Alliance (TADEA) ameongeza na kusema kuwa  wanasiasa wengi wa Afrika wanasumbukia maslahi yao binafsi ambapo vyama vyenye nguvu ya fedha hutumia fursa hiyo kuwarubuni baadhi ya wanachama ili watumike katika shughuli za kushawishi wananchi kuwaunga mkono.

“Ugonjwa mkubwa wa watanzania ni njaa, wanasiasa wanasumbukia matumbo yao na kuacha maslahi ya taifa”, amesema Shibuda katika Mdahalo wa Demokrasia Yetu uliondaliwa na taasisi ya Twaweza.

 

Madhara ya Siasa zisizotabilika

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Vicensia Shule amesema kubadilika kwa wanasiasa kunaathiri ajenda za maendeleo ya wananchi hasa kama wanaohama ni viongozi wakubwa katika chama. Na hali hiyo ikiendelea inaweza kusababisha ukatili wa kisiasa ambao utawafanya wananchi kuchukua maamuzi magumu kuwatoa viongozi wabinafsi madarakani na kuwaweka wengine.

“Sisi watanzania tuna unafiki wa ndani kwa hata viongozi tunaowapata wanawasilisha tabia zetu za ndani za kunyimana uhuru wa kujieleza. Mfumo wetu wa vyama unaundwa na tabia za ndani na zinaakisi aina ya kiongozi tunaowapata.  Hili taifa litaenda kwenye ukatili wa ajabu wa kisiasa”, amesema Dkt. Shule.

Madhara mengine  ni kudhoofisha mfumo wa kisiasa ambapo watu wachache kuwa na maamuzi na sauti juu ya rasilimali za nchi na kuharibu mfumo wa ushindani baina ya vyama vya siasa.

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye (kushoto) akiwa na aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu (katikati) na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana

 

Suluhisho

Hata Hivyo, Shibuda amesema ili tuwe na Demokrasia imara ya vyama vingi, wananchi wanapaswa kuchagua aina ya siasa wanayoitaka ambayo itatoa mwelekeo wa taifa na matumizi ya rasilimali zilizopo. Pia wananchi wapewe zaidi elimu ya uraia itakayowajengea uwezo wa kuhoji na kusimamia itikadi za vyama vyao.

“Wanasiasa wa Tanzania tunahitaji haki elimu ya uraia ndio itakayotufanya tuwe na makutano ya fikra katika mawazo ya dira na ndoto ya Tanzania”, ameshauri Shibuda.

Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini amesema wananchi wanapaswa kutambua kwamba wanasiasa wanabadilika kutokana na maslahi na amewataka kuunda mfumo rasmi ambao utawaunganisha na kujenga mahusiano yenye tija nje ya mfumo wa kisiasa.

Baadhi ya wananchi waliohojiwa wanasema mahusiano yenye tija yanaweza kujenga kwa kupatikana kwa Katiba Bora inayozingatia maslahi mapana ya wananchi ambayo yatawafanya wanasiasa kuwajibika katika maslahi ya taifa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *