Katika “Uchochezi” Sheria iko wazi. Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) inafanya nini?

Jamii Africa

Mapema Januari 2018 vituo vitano vya runinga vilipigwa faini ya jumla ya shilingi milioni 60 baada ya Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kusema kwamba walitangaza matangazo yenye kuleta uchochezi kwa jamii.

Matangazo hayo yalihusu mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa na Tume ya Haki za Binadamu ili kuwasilisha ripoti ya madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na polisi pamoja na wawakilishi wa uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika Novemba 2017.

Maamuzi hayo ya TCRA yaliibua mijadala mbalimbali ya namna gani sheria zinatafsiriwa na kutekelezwa katika maeneo ambayo neno “uchochezi” linahusishwa.

 

TCRA inawezaje kuvipiga faini vituo 5 vya runinga kwa “Uchochezi” wakati neno “Uchochezi” halijatajwa kwenye sheria elekezi?

Kwa namna mbalimbali TCRA ni chombo kilicho wazi na hata tovuti yake ni mfano mzuri wa namna ya kutoa taarifa muhimu kwa jamii. Sheria zote na taratibu zinazohusu kazi zake zinapatikana kwa urahisi sana kwa kila mwenye uwezo wa kupata mtandao. Katika mkutano wake na waandishi wa habari wa kuvipiga faini vituo hivyo, mamlaka hii ilitoa sababu kuhusu uamuzi wake ambao walisema ulijikita katika sheria 5 zinazohusu utangazaji wa habari.

Tatizo ni kwamba neno 'Uchochezi' halijatamkwa mahali popote kwenye sheria hizo 5 hapo juu wala kwenye Sheria ya Utangazaji 1993 ambayo ndio msingi wa kuundwa kwa sheria hizo.  Wala kwenye Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano ya mwaka 2003 au kwenye Sheria ya Mawasiliano ya Kimtandao na Barua ya mwaka 2010 ambayo inaipa TCRA mamlaka iliyonayo.

Hii inaturudisha katika swali la msingi kwamba TCRA inawezaje kuvipiga faini vituo 5 vya runinga kwa “Uchochezi” wakati neno “Uchochezi” halijaelezwa kwenye kanuni na sheria elekezi? 

Uchochezi unafafanuliwa kwenye sheria ya huduma za habari pamoja na kanuni za adhabu ambapo umefafanulia kama nia ya kuleta chuki au dharau kwa mamlaka halali ya kiserikali au utawala uliopo ili kuonyesha hali ya kutoridhika kutoka kwa wananchi au kuibua hisia za uhasama na uadui kati ya makundi mbalimbali ya watu.

Hata hivyo, Sheria zote hizi zinatoa kinga iliyowazi kabisa kwa mashtaka yanayochukuliwa kwamba ni ya kichochezi. Sheria zinasema jambo lolote halichukuliwi kuwa la kichochezi kama lilikuwa na nia ya kuonyesha namna ambavyo serikali inapotoshwa au inakosea katika utekelezaji wake au kuonyesha namna serikali inavyokosea katika Sheria, Katiba au utekelezaji wa haki kwa lengo la kurekebisha makosa hayo.

Kwa maana nyingine ni kwamba kuikosoa Serikali au Jeshi la Polisi katika makosa yao sio uchochezi. Utetezi huu unaweza kuonekana kwenye ripoti ya LHRC na habari zilizotangazwa kuhusu ripoti ile.

 

“Maslahi ya taifa” ni yapi?
Neno “Uchochezi” halijitokezi kwenye kanuni za TCRA lakini linajitokeza kama dhana muhimu inayotamkwa kuwa “maslahi ya taifa”. Vyombo vya habari vinatakiwa kuhakikisha kwamba matangazo yao hayaleti athari za kiwango cha dhana hii.

Kuripoti ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanya na polisi pamoja na wawakilishi wa vyama vya siasa unaweza kuiaibisha Serikali. Na matangazo kama haya yanaweza kuondoa uaminifu wa wananchi juu ya Jeshi la Polisi au Serikali. Ni vyema kuruhusu vyombo ya habari kutangaza mambo haya kwa “maslahi ya taifa” maana kuwakataza wasitangaze ni kama vile kuruhusu mambo haya yaendelee kutendeka.

Hii iliibua swali lingine muhimu sana kwamba “Maslahi ya taifa ni yapi”?

Kwa muktadha huu maslahi ya taifa yanaweza kusemwa kuwa ni kutotajwa kwa matendo maovu ya polisi, wananchi kuendelea kunyanyaswa kwa vitendo viovu ya kisiasa na ukiukaji wa utawala wa sheria. Imeonekana uamuzi wa TCRA uliafiki kwamba utangaza wa ripoti ya LHRC ilikuwa ni kinyume na maslahi ya taifa na hivyo kuvipiga faini vituo hivyo.

 

Kanuni mbili zipo hatarini
Kanuni mbili zipo hatarini katika swala hili ambapo ya kwanza ni endapo mamlaka inatakiwa kufanya kazi ndani ya sheria. Ya pili ni kama maslahi ya taifa yanaweza kutenganishwa kutoka kwenye maslahi ya serikali tawala. Hatma ya jambo hili italetwa na kile ambacho vituo vya runinga vitaamua kufanya kwa siku zijazo kwasababu faini zinatakiwa kulipwa mwanzoni mwa mwezi februari 2018. 

Vituo hivi vya runinga vinaweza kupinga uamuzi wa TCRA na kugoma kulipa faini hizo kwa kujitetea kwa misingi ya kisheria na kimaadili au wanaweza kukubali kulipa faini hizo.

 

Mwandishi wa makala hii ni Aidan Eyakuze (Twaweza), Makala ilitoka kwa mara ya kwanza katika Gazeti la The Citizen la tarehe 22 Januari 2018. 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *