Kombe la CHAN: Taifa Stars ni kufa au kupona Kigali, Uganda ngoma bado mbichi

Daniel Mbega

TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars, inatakiwa kucheza kufa au kupona katika mechi dhidi ya Rwanda Jumamosi, Julai 22, 2017, na ushindi tu ndio utakaoivusha katika hatua ya pili ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Afrika kwa wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN).

Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, matokeo ya mechi ya Julai 15, 2017 jijini Mwanza ya sare ya bao 1-1 yameiweka pabaya huku wapinzani wao, Rwanda, wakiwa wanahitaji suluhu tu ili wasonge mbele kwani wana faida ya bao la ugenini.

Stars imeondoka leo Jumatano alasiri kuelekea Kigali, kwa mechi hiyo ambayo ushindi wake utaipa fursa ya kucheza raundi ya pili na mshindi kati ya Uganda na Sudan Kusini.

Kwa takriban siku tano, Stars ilikuwa imepiga kambi jijini Mwanza kujiwinda na mechi hiyo muhimu ambapo ikivuka hatua zote inaweza kushiriki fainali za CHAN ambazo zitafanyika katika nchi jirani ya Kenya Februari  2018.

Hata hivyo, katika mchezo huo wa marudiano, Stars itamkosa mlinzi wa kulia, Shomari Kapombe, ambaye alipata majeraha katika mechi ya kwanza.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga, amehidi kwamba timu hiyo itafanya vizuri baada ya kurekebisha makosa kadhaa yaliyojitokeza katika mechi ya kwanza.

Kwa upande mwingine, Uganda iko katika wakati mgumu wa kusonga mbele na inahitaji ushindi dhidi ya Sudan Kusini katika mechi ya marudiano itakayofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Nakivubo jijini Kampala baada ya timu hizo kutoka suluhu mchezo wa kwanza.

Uganda Cranes ambayo inanolewa na Milutin Sredojevic ‘Micho’, Mserbia ambaye amekuwa ‘Mswahili’ kwa kuzamia kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa miaka mingi, inatakiwa kujipanga vyema ili iweze kusonga mbele.

“Tulicheza mechi nzuri lakini tukashindwa kufunga licha ya kupata nafasi nyingi,” allisema Micho.

Lakini timu ya Sudan Kusini, maarufu kama Bright Stars, inayonolewa na Felix Komoyangi imejipanga vyema licha ya kushindwa kupata ushindi wa nyumbani.

Zambia inapalilia ushindi wake wa mabao 4-0 dhidi ya Swaziland ilioupata ugenini Jumamosi iliyopita, ambapo inahitaji sare tu ili iweze kusonga mbele.

Kocha wa Zambia, Wedson Nyirenda, amesema pamoja na ushindi walioupata, lakini hawatafanya makosa katika mechi ya marudiano kwa kuwa Waswazi hawatabiriki.

Kocha wa Isihlangu Semnikati kama timu ya taifa ya Swaziland inavyoitwa, Pieter De Jongh, ana wakati mgumu wa kuhakikisha vijana wake wanafanya vyema mjini Lusaka.

Mshindi baina yao atakumbana na mshindi kati ya Afrika Kusini na Botswana kwenye raundi ya pili.

Afrika Kusini, ambayo Jumamosi iliyopita ilipata ushindiwa mabao 2-0 ugenini, itaikaribisha Botswana katika Uwanja wa Moruleng Stadium katikaJimbo la Kaskazini Magharibi.

Matokeo ya mechi zilizopita ni kama yafuatayo:

Julai 15,2017: Sierra Leone 1 – 1 Senegal; Gambia 0 – 0 Mali; Guinea-Bissau 1 – 3 Guinea; Botswana 0 – 2 Afrika Kusini; Tanzania 1 – 1 Rwanda; Comoros 2 – 0 Lesotho; na Djibouti 1 – 5 Ethiopia.

Julai 16, 2017: Liberia 0 – 2 Mauritania; Togo 1 – 1 Benin; Namibia 1 – 0 Zimbabwe; Swaziland 0 – 4 Zambia; Madagascar 2 – 2 Msumbiji; Mauritius 0 – 1 Angola.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *