Kufanya mazoezi kupita kawaida ni hatari kwa afya yako

Jamii Africa

Kuishi muda mrefu ni matamanio ya kila binadamu, kwa sababu kila aliyezaliwa ana kusudi la kutimiza kabla ya kuondoka duniani.

 Mazoezi ya mwili na ulaji wa chakula bora yanatajwa kuwa sehemu muhimu ya kumfanya mtu kuishi muda mrefu kwa sababu  huufanya mwili kuwa na mzunguko mzuri wa damu, mapigo ya moyo kwenda yanavyotakiwa na kuimarisha misuli ili kuwa na msawazo sawa wa viungo vyote.

Lakini baadhi ya mazoezi yakifanyika isivyotakiwa huweza kupunguza umri wa kuishi wa mtu. Mfano kukimbia kupita kawaida (extreme running) kunaweza kupunguza siku za kuishi pasipo muhusika kujua.

Tafiti mbalimbali zinabainisha kuwa ikiwa mtu atakimbia kwa mpangilio mzuri wa masaa 2 hadi 3 kwa wiki na dakika 15-30 kwa siku anajihakikishia kuishi muda mrefu ikilinganishwa na mtu anayefanya hivyo bila kuwa na mpangilio mzuri wa ukimbiaji wake.

Hata hivyo,  inaelezwa kuwa watu ambao hawafanyi mazoezi ya kukimbia na wanaokimbia kupita kawaida kwa kiasi kikubwa wana maisha mafupi ikilinganishwa na wale wanaokimbia kawaida. Lakini baadhi ya Waatalamu wa mazoezi wanapingana na tafiti hizo kwa kusema kuwa hakuna mahusiano ya moja kwa moja katika ya kukimbia na umri wa kuishi.

Wakimbiaji wa mbio ndefu

Jarida la TIME ambalo ni mahusu kwa masuala ya afya katika makala yake ya hivi karibuni linaeleza kuwa kupata mazoezi ya kawaida inasaidia kuimarisha mwili na kuwa na afya bora. Lakini mazoezi yaliyopitiliza kiwango kinachohitajika ni hatari kwa afya.

Jarida hilo lilimuhoji Mtafiti Dkt. James O’Keefe, Daktari wa Moyo katika hospitali ya Mtakatifu Luka iliyopo jiji la Kansas Marekani ambapo alisema mazoezi kama zilivyo dawa nyingine zikitumiwa zaidi ya inavyopendekezwa na daktari zinaweza kuleta madhara katika mwili.

“ Mazoezi yana faida kama zilivyo dawa” alisema. “ lakini lazima yafanyike kwa kiwango kinachostahili, zaidi ya hapo madhara yanaweza kutokea na kuleta matatizo kwa afya na hata kupunguza umri wa kuishi”.

Dkt. O’Keefe alipitia tafiti za watu ambao walifunzwa na kushiriki katika mbio ndefu na mashindano ya baiskeli kwa kiwango kinachostahili ambapo alibaini kuwa watu walioshiriki mbio hizo walipata faida nyingi za kiafya, na walitarajiwa kuishi miaka saba zaidi kuliko watu ambao hawafanyi mazoezi kabisa.

Anasema wakimbiaji wa mbio ndefu ambao walikimbia kupita kawaida walipata madhara fulani ya kiafya ambayo yalitokana na sumu iliyotengenezwa katika mwili na hivyo kupunguza umri wa kuishi.  

 Tafiti zinaonyesha kuwa wakati mtu anashiriki mbio ndefu mapigo ya moyo huenda kasi na ikiwa atakimbia kwa kasi sana, moyo unaweza kudhurika kwa sababu unafanya kazi kupita kawaida.  

 “Ukiwa umekaa, mapigo ya moyo wako yanasukuma damu mara 5 kwa dakika moja, lakini ukikimbia kwenye ngazi za ghorofa ili kujiweka sawa, moyo utasukuma damu mara 35 au 40 kwa dakika,” anasema Dkt. O’Keefe.

“ikiwa utakimbia maili 26 bila kupumzika unaufanyisha moyo kazi kupita kawaida. Moyo utasukuma damu mara 25 kila dakika na kuifanya misuli kukakamaa na kusababisha baadhi ya seli za misuli ya moyo kufa”

 Hali hiyo huufanya moyo kutanuka ili kuendana na mabadiliko ya mzunguko wa damu na mtu anaweza kupata matatizo ya moyo ikiwemo moyo kushindwa kusukuma damu na hatimaye kifo.

 Mtazamo wa Dkt. Martin Matsumura ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Moyo ya Lehigh Valley Health Network ya Marekani anasema wakati mwingine tafiti zinachanganya watu kwa sababu hazitoi majibu ya moja kwa moja.

Njia sahihi ya kukubaliana na kutokukubaliana na tafiti ambazo zinahusu mazoezi ya kukimbia ni kufanya mazoezi kwa maelekezo ya daktari ili kujiweka katika upande ulio salama. Hata hivyo, tunatakiwa kujifunza kufanya jambo lolote kwa kiasi.

 

 

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *