Tunaishi katika dunia ambayo watu wengi wanapenda kujipiga picha ‘selfie’na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii. Tabia hiyo ya kujipiga selfie inatajwa kuwa ni mapinduzi makubwa ya tasnia ya upigaji picha duniani. Pamoja na uzuri wake kuna matokeo hasi ambayo yanaweza kujitokeza kwa mtu pale anapotumia vibaya teknolojia hiyo.
Moja ya madhara hayo ni vifo vya mshtuko wa moyo ambavyo hutokana na watu hao kujipiga picha kwenye maeneo hatarishi na muda usiofaa. Hapa chini ni orodha ya watu waliofariki kwa mshtuko wa moyo wakati wakijipiga picha katika maeneo mbalimbali duniani.
Tunaanzia huko Urusi ambako msichana mdogo aitwae Xenia Ignatyeya alifariki wakati akiwa juu ya jengo refu nchini humo. Taarifa zinaeleza kuwa hakushika vizuri fimbo aliyokuwa imeshikilia simu ambayo alikuwa anatumia kujipiga picha, alikosa mwelekeo na akaanguka chini kutoka kwenye jengo hilo ambalo lina urefu wa futi 820.
Chakushangaza ni kwamba alifariki kabla hajafika chini kwasababu aligusa nyaya za umeme wakati akishuka chini.
Xenia Ignatyeya akiwa juu ya jengo kabla ya mauti kumkuta
Mwingine ni David Gonzalez Lopez (23) kutoka nchini Uispania. Kilichomkuta kijana huyu ni kusimama mbele ya kile kinachotajwa kuwa ni ng’ombe mkubwa wa mashindano, wakati akishiriki sherehe katika mji wa Villaseca de la Sagra nchini humo. Lopez alijaribu kujipiga selfie na ng’ombe huyo na hakuna mtu yeyote alishangaa lakini ghafla alirushwa na alipoanguka chini alifariki dunia. Na hapo huwezi kumlaumu ng’ombe.
David Gonzalez Lopez wakati wa uhai wake
Wanaofuata ni wanandoa kutoka Poland ambao walikutana na mauti bila kutarajia mwaka 2014 kwasababu tu ya kujipiga selfie. Wakati wakijipiga selfie kwenye ncha ya mwamba uitwao Cabo da Roca uliopo Magharibi ya Ugiriki, wanandoa hao walivuka kizuizi cha usalama ili wafike kwenye kilele cha mwamba huo ambao uko karibu na bahari.
Walikosa mwelekeo kwenye eneo ambalo hawaruhusiwi kufika na kuanguka chini na baadaye kufa. Jambo la kusikitisha ni kuwa walikufa wakati watoto wao wawili, miaka 5 na 6 wakishuhudia tukio hilo la wazazi wao kupanda kwenye kilele cha mwamba huo.
Orodha ni ndefu, kifo kingine kilikuwa cha mtalii kutoka Japan mwaka 2015 ambacho kilitokea kwenye moja ya maajabu saba ya dunia- Taja Mahal katika mji wa Agra, India. Ripoti zinaeleza kuwa mwanaume huyo alisimama kwenye ngazi za jengo kubwa la kihistoria huku akijipiga selfie ghafla dhoruba ikatokea. Mtalii huyo alikosa uthabiti na kuanguka chini na baadaye alikufa kutokana na majeraha aliyoyapata kichwani.
Tunaamini wasomaji mnajifunza kitu kwa mfano huu na kuna haja ya kutanguliza usalama kwa kila kitu tunachofanya.
Nyumba la Taja Mahal katika mji wa Agra, India
Raia wa China aliyetambulika kwa jina la Chen alikutwa amekufa kwenye bonde karibu na maporomoko ya maji ya Zhejiang Kaskazini mwa China mwaka 2015. Mwili wake ulikutwa ukiwa na simu ya mkononi na fimbo ya kujipigia selfie. Iligundulika kwenye picha zilizokutwa kwenye simu yake ambapo alikosa mwelekeo wakati akipiga selfie na baadaye kuanguka chini ya bonde hilo na kupoteza maisha.
Anayefuata katika orodha ya vifo vya mshtuko wa moyo wakati wa kujipiga selfie ni mwanafunzi wa miaka 14, Marie Rocello kutoka Ufilipino. Alikutana na mauti wakati wakati akijipiga picha kwenye ncha ya ngazi zilizopo katikati ya ghorofa namba 1 na 2 za shule yake ya Rizal iliyopo jiji la Pasig. Rocelo alianguka chini na moja ya mbavu zake ilijeruhi figo na baadaye alikufa.
Jarida la Time limeitaja Ufilipino kama ‘Jiji la Selfie Duniani’ na hasara yake ni kukutwa kwa watu wengi wakiwa wamekufa kwasababu ya kujipiga picha.
Kifo kingine kilitokea kwenye Chuo Kikuu cha Taifa cha Urusi ambapo mwanamke (21) alikufa wakati akienda kujipiga picha kwenye daraja ambalo lina muonekano mzuri. Lakini, bahati mbaya aliteleza na kuanguka kwenye maji na matokeo yake alikufa. Tukio hilo lilitokea mwaka 2015 mbele ya Kituo cha Kimataifa cha Biashara cha Moscow.
Anayefuata kwenye orodha hii ni mwanamke aliyetambulika kwa jina la Courtney Sandord. Siku ya Aprili 26, 2014, muda wa saa 2 asubuhi aliweka picha yake ya selfie kwenye mtandao wa Facebook na kuandika “Wimbo wa furaha unanifanya niwe na furaha zaidi”.
Dakika chache baadaye gari lake liligongana na roli na kufariki papo hapo na gari lake lilishika moto. Hili pia linathibitisha kuwa tunatakiwa kuwa makini tunapokuwa barabarani na hatupaswi kutumia simu, kutuma ujumbe au kupiga simu.
Mwanamuziki Ramon Gonzalez (a.ka Jadiel El Tsunami) kutoka Puerto Rico, alikuwa akiendesha baiskeli wakati akijipiga picha ambapo alikutana na mauti ikawa mwisho wa maisha yake. Gonzalez alipoteza mweleko na kugongana na gari lililokuwa linakuja mbele yake. Japokuwa alikimbizwa hospitalini lakini hawakufanikiwa kuokoa uhai wake. Mashabiki wengi waliomboleza kifo chake lakini hawakuweza kurejesha uhai wake.
Mwanamuziki Ramon Gonzalez kabla ya kufariki
Kifo kingine ni cha mtembeaji wa milima ambaye alifariki wakati akifanya matembezi hayo huku akijipiga selfie kwenye mteremko wa mlima Lion Rock katika jiji la Hong Kong. Taarifa zinaeleza kuwa kijana mwenye umri wa miaka 30 alikuwa akitembea mwenyewe na kujaribu kujipiga selfie kuifikia sanamu ya kichwa cha samba kilichopo kwenye milima hiyo.
Alipoendelea juu zaidi bila kutumia fimbo, ghafla alipotea na mtu aliyekuwa anamshuhudia alisikia akipiga kelele. Mshuhudiaji huyo alipoenda kumtafuta alimuona akiwa amening’inia kwenye kichaka cha majani kabla ya kuanguka chini. Ilithibitishwa kuwa amefariki na madaktari kutoka kitengo cha Serikali kinachotoa huduma ya watu wanaotembelea safu za milima hiyo.
Kifo kingine ambacho kilileta simanzi ni cha binti aliyetambulika kwa jina la Anna Ursu (18) kutoka Romania. Mei, 2015 alienda kwenye Stesheni ya Treni ya Lasi kwa nia ya kujipiga picha na kuiweke Facebook. Alipoisogelea karibu Treni iliyokuwa na watu wengi ili apate picha nzuri, alinyanyua mguu wake ambapo kwa bahati mbaya uligusa waya wa umeme.
Ghafla, Ursu alirushwa na kupashuka, japokuwa alikimbizwa hospitalini lakini alifariki kwa asilimia 50 ya mwili wake kuungua.
Anna Ursu kabla ya kufariki
Kujipiga selfie ni ugonjwa?
Imeelezwa kuwa tabia ya kujipiga picha mwenyewe (selfie) na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii kunahusishwa na ugonjwa wa akili ujulikanao kitaalamu ‘Selfitis’ ambapo mgonjwa wa tatizo hili hugunduliwa kwa idadi ya picha alizopiga na kuziweka kwenye mitandao ya kijamii.
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Nottingham Trent na Shule Kuu ya Utawala iliyopo nchini India ndio waliogundua ugonjwa huo wa ‘Selfitis’ baada ya taarifa kuripotiwa na vyombo vya habari mwaka 2014 ambazo zilitolewa na Chama Cha Marekani cha Tiba ya Akili kuwa kujipiga picha mara kwa mara ni moja ya dalili za kupata ugonjwa wa akili.
Sababu za Kujipiga selfie
Ziko sababu sita zinazowashawishi watu ambao wameathirika na ugonjwa wa akili wa selfitis ambapo hutafuta; Kuongeza kujiamini, kukubalika na kusikilizwa, kuboresha msawazo wa mawazo, kutengeneza kumbukumbu ya eneo alilotembelea, kuongeza ukaribu na ushindani kwa watu wanaowafuatilia kwenye mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, tunatakiwa kuchukua tahadhari wakati wa kujipiga picha hasa kwenye maeneo hatarishi ambayo yanaweza kugharimu uhai wa maisha yetu kwa tabia ambazo tunaweza kuziepuka.