WAKAZI wa mji wa Kyaka wilayani Missenyi wamesema hawako tayari kupisha ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya Kyaka – Bugene bila kupewa fidia vinginevyo watalala barabarani kupinga uamuzi huo.
Hivi karibuni Waziri wa Ujenzi John Magufuli alikaririwa akisema kuwa wizara yake iko mbioni kuwatumia askari wa kikosi cha kupambana na ghasia(FFU) kukabiliana na wananchi wataokataa kupisha ujenzi wa barabara.
Wakitoa malalamiko mbele ya Angela Robert ambaye ni ofisa wa Tanroads makao makuu walisema hawakubaliani na uamuzi wa kubomoa nyumba zao bila kupewa fidia kwa madai ya kujenga kwenye hifadhi ya barabara.
Ofisa huyo alidai anazunguka maeneo mbalimbali nchini kuelimisha wananchi umuhimu wa kupisha maeneo ya hifadhi za barabara na kuwa alikuwa akitimiza wajibu wake wa kufikisha agizo la serikali kwa wananchi hao.
Katika mkutano uliofanyika katika viwanja vya ofisi ya Kata ya Kyaka alisema wananchi watakaopewa fidia ni wale waliojenga nje ya mita 22 na nusu kila upande huku ikionekana idadi kubwa ya wananchi hawastahili fidia.
Wananchi walionekana kushangazwa na maelezo ya ofisa huyo aliyerejea sheria ya mwaka 1958 inayobainisha maeneo ya hifadhi ya barabara na kudai kuwa mtaalamu aliyefanya tathimini ya awali aliwadanganya baadhi ya wananchi kuwa watapata fidia.
Baada ya kubanwa na wananchi Anjela Robert alijitetea kuwa hakuwa na muda wa kuzunguka nchi nzima kuwafafanulia wananchi matakwa ya sheria hiyo ikizingatiwa kuwa yeye ni ofisa peke yake mwenye jukumu la kufanya hivyo.
Diwani wa Kata hiyo Projestus Tegamaisho aliungana na kilio cha wananchi wake huku akionya kuwa serikali ijiandae kukabiliana na aibu ya kushindwa kuwahifadhi wananchi watakaokosa makazi huku ikitoa misaada kwa nchi zinazokabiliwa na maafa.
Aidha alisema idadi kubwa ya wananchi watajikuta hawana makazi huku wananchi wakimsimamisha mzee mwenye umri wa zaidi ya miaka tisini aliyetambulika kwa jina la Mwaga ambaye ni miongoni mwa watu watakaoathiriwa na zoezi la ubomoaji bila fidia.
Alisema wiki ijayo wananchi na viongozi wa kata hiyo watafanya kikao cha kupinga uamuzi wa kuwahamisha bila fidia ambapo malalamiko hayo yatawasilishwa serikalini.
Katika kikao hicho Mkuu wa wilaya hiyo Kanali Issa Njiku aliwaomba wananchi hao kuwa na subira na kuwa ofisi yake haikuwa na uwezo wa kubatilisha suala lolote kwani uamuzi huo ulikuwa juu ya uwezo wake.
Habari hii imeandikwa na mwandishi Phinias Bashaya aliyeko mkoani Kagera