WATANZANIA wanaendelea kuwa wafupi kwa kukosa lishe bora, kukumbwa na magonjwa ya utotoni na kuishi mazingira ya ovyo.

Imebainika kuwa urefu wa kimo kwa Watanzania umepungua kwa kasi kutoka ongezeko la sentimita 2.9 hadi kufikia 1.2, katika kipindi cha miongo mitano iliyopita. Muongo mmoja ni miaka 10.

Matokeo ya utafiti uliofanywa na timu ya wataalamu wa lishe kwa kushirikiana na wale wa magonjwa yasiyoambukiza kutoka Marekani, wameeleza kuwa Watanzania, huenda wakawa wafupi zaidi miaka 50 ijayo.

“Katika miaka ya 1960, Watanzania wengi walikuwa wakizaliwa na kuendelea kuwa warefu, lakini hali hiyo imebadilika, wanapungua kimo kutokana na magonjwa, lishe duni na kuishi mazingira ya umasikini,” inaeleza taarifa ya matokeo ya utafiti huo.

Wataalamu hao wa afya wanasema kuwa makuzi ya watoto huanza kipindi mama anapobeba mimba na hutegemea zaidi lishe yake; ikiwa bora, mtoto hukua vyema, ikiwa mbaya, basi ukuaji wa mtoto tumboni huathirika.

Matokeo ya utafiti huu yamechapwa katika gazeti la kitabibu la eLife la Julai mwaka huu – la Marekani ambapo yanaonesha kuwa Tanzania ilikuwa inashika nafasi ya 157 duniani kwa kuwa na wastani wa watu wenye urefu wa sentimita 167.7. Nchi 200 zilihusika katika utafiti huo.

Hivi sasa, kwa mujibu wa utafiti huo, Tanzania inashika nafasi ya 179 duniani kwa kuwa na watu wenye urefu wa sentimita 164.48. Urefu huu ni kwa wanaume wenye umri kati ya miaka 25 hadi 50.

Kwa upande wa wanawake wenye umri huo, Tanzania ilikuwa ikishika nafasi ya 152 kwa kuwa na wastani wa urefu wa 157.1 miaka ya 1960, hadi kufikia nafasi ya 160 kwa urefu wa wasitani wa 155.9

“Watoto wanaokula vyema, hukua vizuri na kwa haraka zaidi, wale wanaokula ovyo na bila mpangilio, hudumaa, sasa hali hiyo imeikumba Tanzania pia,” inaonesha sehemu ya matokeo ya utafiti huo.

Unapoanza huduma ya ujauzito/kliniki, moja kati ya mambo unayopaswa kumuuliza kwanza mjamzito ni kama ana dalili zozote zinazoashiria lishe duni au ukosefu wa madini ya iodini kwa mlo wake. Hii ni muhimu sana, kwa sababu lishe duni kwa mama huhusishwa na matokeo duni ya mimba kama vile mtoto mdogo, na anaweza kuwa mfupi.

Aidha, lishe duni inatajwa kuwa moja ya sababu zinazochangia kudumaa kwa watoto na kuzorota kwa kiwango cha elimu nchini.

Pamoja na utafiti huo kuja na wastani wa urefu huo, Mtanzania mmoja, Baraka Tolu, ndiye anatajwa kuwa mrefu zaidi sasa akiwa na sentimita 223.5.

baraka-tolu_fp

Baraka Tolu, mtanzania anayetajwa kuwa mrefu zaidi akiwa na urefu wa sentimita 223.5

Tolu anasema anapenda kuutumia urefu wake kumuingizia kipato kwa kufuata nyayo za Mtanzania mwingine, Hasheem Thabit anyecheza ligi ya mpira wa kikapu Marekani (NBA).

Hasheem ana urefu wa sentimita 221, akiwa anazidiwa na Tolu kwa sentimita 2.5 

Hasheem Thabeet

Kijana wa kitanzania, Hasheem Thabit ambaye amefanikiwa kucheza mpira wa kikapu nchini Marekani

Utafiti wa wataalamu hao pia unazitaja Niger, Rwanda, Sierra Leone na Uganda kukumbwa na ufupi kwa watu wake wengi kwa sababu ileile ya lishe duni na magonjwa.

Madagascar ina wastani wa watu wenye urefu wa sentimita 161.5 na Malawi – sentimita 162.2.

Niger nayo inatajwa kuwa miongoni na watu wafupi miongoni mwa nchi zilizofanyiwa utafiti kwa kuwa na mporomoko wa wastani wa sentimita 3.9 – kwa wanaume na 3.7 kwa wanawake. Watu wake wengi wana urefu wa wastani wa sentimita 160.1.

Katika hatua nyingine, utafiti huo umebaini kuwa watu warefu wako katika hatari zaidi ya kukumbwa na magonjwa ya maungo ya uzazi, ikiwamo saratani.

Dk. Simeon Mesaki wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mtaalamu wa masuala yanayohusu Elimu ya Jamii na Mazingira, ameiambia FikraPevu kwamba utafiti huo unabeba hali halisi ya maisha ya Watanzania walio wengi.

“Kutokana na maisha ya watu kuwa magumu, hawawezi kula vyakula vyenye ubora, bali wanakula ili wasife kwa kujaza matumbo,” anaongeza.

Utafiti huo wa wataalamu unaoana na mtazamo wa Dk. Mesaki juu ya vyakula; kwamba wanaokula vyema, hukua vyema – hujenga mwili, hivyo kuwa na urefu mzuri.

Wataalamu hao wa afya, kwenye utafiti wao wanazitaja Korea Kusini na Irani kuwa miongoni mwa nchi zenye wastani mzuri wa urefu kwa watu wake kutokana na kinachotajwa kuwa “maisha mazuri.”

Watu warefu zaidi wanatajwa kutokea Uholanzi, wakiwa na wastani wa sentimita 182.5 na wafupi zaidi wakitokea Guetemala, wakiwa na wastani wa sentimita 140.3 sentimita.

Hata hivyo, pamoja na utafiti huo, dunia inamtaja Sultan Kosen, raia wa Uturuki kuwa binadamu mrefu zaidi akiwa na urefu wa futi 8 na nchi 3, wakati mfupi zaidi alikuwa marehemu Chadra Dangi raia wa Nepal akiwa na urefu wa futi 1na inchi 7 (sentimeta 54.6).

Watu hawa wawili wanatajwa na vyanzo vingi kuwa na maumbile yasiyokuwa ya kawaida na mara kadhaa wamekuwa wakikutana na kustaajabisha umma. Chandra Dangi alifariki mwaka jana (2015) akiwa na umri wa miaka 75.

Lakini, pamoja na urefu ama ufupi wa watu hao maarufu duniani, taarifa za kitabibu zinaeleza kuwa makuzi yao yanatokana na magonjwa; ulemavu wa maungo yao na hayahusishwi na vyakula.

By Jamii Africa

JamiiForums' Editorial Website | Tanzania's Online News Portal | Dedicated for Public Interest Journalism

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *