Magonjwa yanayosababisha kutoa usaha, kuumwa na kuwashwa sehemu za siri!

Jamii Africa

KUNA magonjwa mengi yanayosababisha mtu kukojoa udenda (usaha), uume kuuma au kuwasha wakati wa kukojoa.

Magonjwa yanayosababisha hali hiyo kwa sana ni pamoja na klamidia (chlamydia), kisonono (gonorrhea), trichomoniasis na magonjwa mengine yanayoathiri njia ya mkojo (nongonococcal urethritis) ambayo FikraPevu inayachambua.

Klamidia (Chlamydia)

Klamidia (Chlamydia) ni moja ya magonjwa ya zinaa. Ugonjwa huu unasababishwa na viini vya bakteria vwanaojulikana kitalaamu kama Chlamydia trachomatis na waweza kuathiri uke, mrija wa kupitisha mkojo, uume au sehemu ya kupitishia haja kubwa.

Klamidia (Chlamydia) ndio ugonjwa wa zinaa unaotokana na bakteria unaoongoza kwa maambukizi mengi zaidi duniani ukifuatiwa na ugonjwa wa kisonono (gonorrhea).

Ugonjwa wa klamidia (chlamydia) huweza kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya kujamiana. Ugonjwa huu ni wa hatari kwa sababu mama mjamzito anaweza kumuambukiza mtoto wake wakati wa ujauzito.

Pia, kuchangia vifaa vya kuogea kama taulo vya mtu mwenye maambukizi, kuchangia vyoo vya kukaa na mtu mwenye maambukizi na kukumbatiana na mtu mwenye maaambukizi.

Vile vile ugonjwa huu unaweza kuambukizwa kupitia mbawa, kupitia vinyesi vya ndege kama kuku, bata na kasuku walioambukizwa klamidia (chlamydia) inayopatikana kwa wanyama ijulikanayo kitaalamu kama Chlamydophila psittaci na kusababisha aina ya homa ya mapafu au homa ya kasuku (psittacosis).

Klamidia huathiri sehemu tofauti za mwili wa binadamu kama macho, mfumo wa upumuaji, sehemu za siri kama makalio, viungo vya uzazi na tezi (lymph nodes).

Huchukua siku 1-14 tangu maambukizi hadi kuonekana kwa dalili. Asilimia 75 ya wanawake na asilimia 50 ya wanaume wanaopata maambukizi ya ugonjwa huu huwa hawaonyeshi dalili za moja kwa moja.

Kwa wanaume, ugonjwa huu huathiri mrija wa kupitishia mkojo, dalili kama vile uume kuwasha, kutokwa na ute na kusikia maumivu wakati wa kukojoa, sehemu ya tundu kwenye uume kuwa nyekundu, kuvimba na kuwasha pia kuhisi maumivu kwenye korodani na tezi zilizopo sehemu za siri ambazo huvimba na kuambatana na maumivu.

Dalili za ugonjwa huu kama umeathiri makalio (puru) kwa wanawake na wanaume ni kama kuwashwa na kutokwa na damu kwenye puru, maumivu wakati wa kujisaidia haja kubwa na kutokwa na uchafu kama kamasi kutoka kwenye puru.

Iwapo vimelea vya klamidia vitaathiri macho, wanawake na wanaume huwa na dalili kama kuvimba macho, macho kuwa mekundu, kuwasha na hata kutokwa na majimaji machoni.

Klamidia inayoambukiza kwenye macho hujulikana kitaalamu kama Chlamydia conjunctivitis au Trakoma (trachoma) na ndiyo inayoongoza kwa kusababisha upofu duniani.

Dalili za klamidia kwa watoto wachanga hutokea katika kipindi cha wiki mbili kwenye macho, na iwapo ni homa ya mapafu dalili zake hujitokeza katika kipindi cha wiki mbili hadi miezi 3 baada ya kuzaliwa.

Madhara ya ugonjwa huu kwa wanaume ni kuathiri korodani na kusababisha mwanamume kukosa uwezo wa kutengeneza mbegu za uzazi (manii/shahawa) au kuwa tasa na pia husababisha maambukizi kwenye tezi dume (prostatitis).

Kwa wanawake, husababisha maambukizi kwenye mirija ya uzazi, mfuko wa uzazi, na mayai ya uzazi, kwa hivyo kusababisha ugonjwa wa uvimbe katika fupanyonga (PID).

Pia huongeza uwezekano wa wanawake kupata mimba zinazotunga nje ya mfuko wa uzazi (ectopic pregnancies).

Mwanamke hupata maumivu sugu kwenye nyonga na ugonjwa wa mifupa (arthritis) aina ya Reiters syndrome. Vilevile, klamidia huweza kusababisha ugumba kwa mwanamke kama hatapata tiba na kwa wanawake wajawazito, klamidia husababisha wajifungue kabla ya wakati wao.

Aidha, mtoto anaweza kuzaliwa na maambukizi kwenye masikio, sehemu za siri, macho na kwenye mapafu, yaani homa ya mapafu, na kama mtoto hatapatiwa tiba ya haraka ya macho baada ya kuzaliwa basi anaweza kuwa kipofu.

Kisonono (Gonorrhea)

Ugonjwa wa Kisonono (gonorrhea) husababishwa pia na bakteria waitwao kitalaamu Neisseria gonorrhoeae unapofanya mapenzi na mtu mwenye kisonono.

Ugonjwa huu unaweza kuaathiri viungo kama vile uke, uume, sehemu ya haja kubwa na ya haja ndogo, na hata koo au mdomo kama ukifanya mapenzi ya kunyonyana.

Wanaume huwa na dalili kama uume kutoa ute wa njano au kijani, na kupata maumivu wakati wa kukojoa (mkojo kuchoma).

Pia kuna uwezekano wa kuwashwa ama kutokwa na maji maji katika sehemu ya kupitishia haja kubwa. Ingawa hivyo baadhi ya watu hawaoni dalili zozote kabisa lakini bado wanaweza kuwaambukiza wanaofanya mapenzi nao.

Trichomoniasis

Ugonjwa wa Trichomoniasis unasababishwa na vimelea vya jamii ya protozoa vinavyojulikana kitalaamu kama Trichomonas vaginalis.

Ugonjwa huu huathiri mrija wa kupitisha mkojo (urethra) na tupu ya mwanamke (vagina). Huathiri sana wanawake kuliko wanaume na wanawake wenye umri mkubwa wako katika hatari zaidi kuliko mabinti wadogo.

Ugonjwa huu hupatikana kwa njia ya kujamiana bila kutumia kinga na mtu aliyeathirika na Trichomoniasis.

Dalili za Trichomoniasis huanza kuonekana kuanzia siku ya 4 mpaka ya 28 baada ya mtu kupata maambukizi. Wanaume huwa hawaonyeshi dalili zozote lakini baadhi wanaonyesha dalili kama kuwasha ndani ya uume, kutokwa na uchafu au majimaji kutoka kwenye uume, kuwasha au mkojo kuchoma wakati wa kukojoa au baada ya kutoa shahawa.

Mwanaume asipopata matibabu mapema huongeza hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI na huongeza hatari ya kupata saratani ya tezi dume.

Magonjwa mengine ya njia ya mkojo

Magonjwa mengine yanayoathiri njia ya mkojo husababishwa na bakteria na huathiri mfereji wa kupitisha mkojo (urethra). Magonjwa hayo husambazwa kwa kujamiiana. Dalili kwa wanaume ni kutokwa na ute kwenye tundu la uume na huenda akahisi maumivu wakati wa kukojoa au akahisi maumivu na kuwashwa-washwa kwa pamoja.

Ikiwa unapata dalili isiyo ya kawaida ni busara kutafuta msaada wa kitabibu na siyo kusubiri mpaka hali inakuwa mbaya au kujinywea tu dawa bila ushauri wa daktari.

Njia sahihi ya kujikinga na magonjwa ya zinaa ni kuacha, kuepuka kujamiiana au kufanya ngono zembe na sizizo salama.

Kwa wanawake wajawazito, ni vizuri kuhudhuria kliniki mapema wakati wa ujauzito na kupimwa vipimo mbalimbali ili kubaini ikiwa mama mjamzito ameambukizwa na ugonjwa wowote wa zinaa na kupatiwa matibabu mapema.

Kwa wale wenye maambukizi wanashauriwa kuchukua tahadhari ya kutowaambukiza wapenzi wao kwa kufanya ngono salama.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *