Rais John Magufuli amevitaka vyombo vya dola kuwafikisha mahakamani watu wanaobadilisha takwimu zinazotolewa na serikali na kuwapotosha watanzania.
Akitoa maagizo hayo Ikulu leo wakati wa kuwatunuku vyeti wajumbe wa Kamati iliyokuwa inafanya mazungumzo na kampuni ya dhahabu ya Barrick ili kuongeza mapato ya madini, Rais Magufuli amesema watu wanaopingana na takwimu za hali ya uchumi na mapato wana lengo la kuichonganisha serikali na wananchi.
“Niwaombe watanzania tofauti na watu wengine wachache ambao kwao kubadilisha takwimu ni kitu cha kawaida muwapuuze, watu wa namna hiyo wapo tu kwasababu wanatutoa katika dira ya uchumi na lengo lao ni kuichonganisha serikali na wananchi”, amesema Rais Magufuli
Kauli ya Rais imekuja siku chache baada ya baadhi ya wanasiasa kusikika wakitofautiana na takwimu za serikali za hali ya uchumi na zile zinazoonyesha kuwa mapato yatokanayo na kodi yameongezeka na kudai kuwa takwimu hizo sio sahihi na haziendani na hali halisi ya uchumi wa wananchi wa kawaida.
Hivi karibuni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitangaza kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2017/2018 (Julai, Agosti na Septemba) imekusanya jumla ya trilioni 3.65 ambayo ni ongezeko la asilimia 1.2 ikilinganishwa na makusanyo ya kipindi hicho kwa mwaka uliopita. Na inatarajia kufikia lengo lake la kukusanya trilioni 17 kwa mwaka.
Kutokana na maoni hayo ya wananchi, Rais amemtaka Waziri wa Sheria na Katiba Prof. Palamagamba Kabudi na vyombo vya dola kuwafuatilia watu hao ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakibadilisha takwimu za serikali na kuwapotisha wananchi ili wafikishwe mahakamani kuthibitisha tuhuma zao.
“Lakini nafikiri vyombo vya dola na Prof. Kabudi wewe ndio Waziri wa Sheria muanze kuangalia watu wa namna hiyo ambao kwao ni kubadilisha takwimu. Unakuta mtu anazungumza makusanyo yameshuka wakati anajua kabisa si kweli. Watu wa namna hii wangekuwa wanapelekwa mahakamani wakathibitishe” amesema Rais na kuongeza kuwa,
“Katika hesabu za kawaida tu kama mapato yanashuka utaweza kusaini mkataba wa kujenga reli ya standard gauge yenye thamani ya zaidi ya trilioni 7 kutoka Dar es salaam hadi Morogoro kilometa 300 na kutoka Morogoro hadi Dodoma kilomita 426 na ni reli ya aina yake, utazipata wapi fedha kama makusanyo yameshuka”.
Kulingana na Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 ambayo imefanyiwa maboresho katika kifungu cha 5 kinaeleza kuwa mtu yeyote ambaye atatoa au kuchapisha takwimu ambazo zinapingana na Sheria atakabiliana na adhabu ya kulipa faini isiyopungua milioni 5 au kufungwa jela kwa muda usiopungua mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.
Kwa upande wake, Waziri wa Sheria na Katiba Prof. Palamagamba Kabudi amemshukuru Rais kwa kuiamini kamati hiyo aliyoiteua kufanya kazi ya kutetea maslahi ya taifa na kuhakikisha wananchi hawaibiwi tena katika sekta ya madini.
Amesema wataendelea kutoa ushirikiano na kwamba watachunguza maeneo mengine ya madini ya Almasi na Tanzanite ili kuihakikishia serikali mapato. Na amewataka watanzania kuendelea kuiamini serikali yao katika kuwaletea maendeleo wanayoyataka.
“Ukitaka kupima mafanikio aliyofikia mtu usiangalie kimo alichofika, bali uwezo wa shimo aliofikia”
Akizungumzia suala la kutoa vyeti kwa wajumbe walioshirika mazungumza na kampuni ya Barrick, Rais amesema watanzania hao wamefanya kazi nzuri ya kupigania maslahi ya taifa katika sekta ya madini. Mazungumzo hayo yaliwezesha kampuni ya Barrick kukubali kulipa fidia ya bilioni 700 kama hatua ya kuendelea na mazungumzo.
Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli
Awamu nyingine itahusisha kamati ndogo ambayo itaendelea na mazungumzo na wawakilishi wa kampuni hiyo ili kufikia muafaka wa kugawana faida ya 50/50 baada ya kodi zote kulipwa na kuiwezesha serikali kumiliki hisa za 16% na kupata kodi ya 70%.
Makubaliano hayo yamezua mijadala miongoni mwa wananchi huku wengine wakisema haiwezekani serikali yenye hisa 16% kupata faida ya 50/50. Wananchi wengine wanaona serikali imepiga hatua nzuri kwa kuongea na wawekezaji hao ili kuongeza mapato yatakayosaidia kuboresha huduma za kijamii.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe hivi karibuni alikaririwa na vyombo vya habari juu ya makubaliano ya serikali na Kampuni ya Barrick kuipa Tanzania fidia ya bilioni 700 na kugawana faida 50 kwa 50 licha ya serikali kumiliki hisa za asilimia 16, alisema suala hilo haliwezekani na serikali inapaswa kuwaambia ukweli wananchi juu ya mchakato mzima wa upatikanaji wa mapato katika sekta ya madini.
“Tanzania changamoto zake ni mbili tu kwenye sekta ya madini, umiliki na mfumo wa kodi ya kimataifa. Mfumo wa kodi ya kimataifa unayaruhusu makampuni kufungua makampuni dada kwenye nchi zenye kodi ndogo (tax haven)” amesema Zitto na kuongeza kuwa,
“Hapana sivyo, huwezi kuwa na hisa ya 16% ukapata faida ya 50% haiwezekani, haipo kokote duniani lakini unaweza kama ukimfanya muwekezaji kuwa mkandarasi sababu utamlipa fee yake na wala sio jambo la ajabu tunafanya hivyo kwenye sekta ya mafuta. Tuna mfumo maalumu wa kugawana faida”
Katika hatua nyingine, Prof. Florens Luoga ambaye alikuwa miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo, ameteuliwa na Rais kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) akichukua nafasi ya Prof. Benno Ndulu ambaye anamaliza muda wake wa utumishi.
Hafla hiyo ya kuwatunuku vyeti wajumbe wa kamati walioshiriki mazungumzo na Barrick imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, vyama vya siasa na watendaji wa serikali wakiwemo mawaziri.