Magugu maji tishio kwa uhai Ziwa Victoria, nchi zinazotumia mto Nile hatarini kukosa maji

Jamii Africa

Ziwa Victoria ni miongoni mwa rasilimali muhimu zilizopo Tanzania, lina sifa moja ya pekee ambayo ni kina kirefu  cha maji kuliko maziwa yote Afrika. Upekee wake umelifanya ziwa hilo kuwa chanzo kikubwa cha maji yanayotumika katika shughuli mbalimbali za binadamu.

Ziwa hilo limezungukwa na nchi za; Kenya, Uganda na Tanzania ambapo sehemu kubwa ya ziwa hilo iko Tanzania likiwa linazungungwa na mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera na Geita. Ziwa hili limekuwa chanzo kikuu cha maji ya mto Nile ambao unapita katika nchi kumi ambazo huutumia kwa shughuli mbalimbali za kilimo, mifugo, uvuvi na usafiri.

Licha ya umuhimu wake kwa maendeleo ya nchi husika, uhai wa Ziwa Victoria unatishiwa na ongezeko la magugu maji (hyacinth) ambayo yanaathiri upatikanaji wa maji katika nchi zinazozunguka ziwa hilo na kutishia uhai wa viumbe.

Athari kubwa inayojitokeza ni kupungua kwa eneo la maji na kuchukuliwa na magugu maji ambayo huzaliana kwa kasi na kusambaa katika eneo kubwa. Kutokana asili ya magugu hayo kutumia maji mengi  na huzuia maji yanayokwenda katika mto Nile ambao hutumiwa na nchi 10 ambazo zinaunda umoja wa nchi za bonde la mto Nile.

Magugu maji juu ya ziwa

Nchi wanachama wa Bonde la Mto Nile ni Uganda, Kenya, Tanzania, Burundi, Rwanda, Sudan, Sudan Kusini, Ethiopia, Congo DRC na Misri.  Zilianzisha umoja wao mwaka 1999 ili kuwa na matumizi sahihi ya maji lakini harakati hizo zinakwamishwa na magugu maji katika Ziwa Victoria.

Ili kukabiliana na magugu maji nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekuwa wakitekeleza miradi mbalimbali ya utunzaji wa mazingira katika ziwa hilo ili kuhakikisha uwepo wa ziwa hilo unaendelea kuwa wenye manufaa katika vizazi vingi vijavyo.

Wanatekeleza Mradi wa Utunzaji wa Mazingira katika Ziwa Victoria Awamu ya II (LVEMP-II) ambao majukumu yake ni kupambana na kutokomeza mazalia ya  magugu maji katika eneo la Ziwa Victoria.

Katika ripoti ya LVEMP-II iliyotolewa hivi karibuni inaeleza kuwa wamefanikiwa kupunguza eneo lenye magugu maji katika ziwa hilo kutoka hekta 520 mwaka 2010 hadi kufikia hekta 106 mwezi Mei mwaka huu. Kiwango hicho ni sawa na asilimia 80 ya magugu yote yaling’olewa katika ziwa hilo.

Mratibu wa mradi wa LVEMP-II, Omary Muyanza akiongea na vyombo vya habari mkoani Mwanza amesema  mradi huo uko chini ya nchi 5 za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo zinatumia ukanda wa Ziwa Victoria – Burundi, Rwanda, Tanzania, Uganda na Kenya.

 Mradi wa LVEMP – II ni matokeo mazuri ya utekelezaji wa mradi wa LVEMP-I ambao shughuli zake ziliisha Desemba 2005 ambapo uliingia katika hatua ya pili ili kuhakikisha rasilimali maji katika nchi wanachama inapatikana kwa uhakika. Utekelezaji wa mradi huo unafanywa kwa ushirikiano wa vikundi 42 vya kijamii kupitia Wilaya ambazo mradi huo unatekelezwa.

Muyanza amesema njia inayotumika sasa kudhibiti magugu maji ni kumtumia mdudu ajulikanye kama ‘Weevil’ ambaye hupendelea kutafuna majani ya magugu maji. Njia hiyo ambayo ni salama imekuwa ikitumika kwa muda mrefu na ni endelevu. Pia njia ya kuong’oa magugu kwa kutumia mashine maalum ambazo zimekuwa zikitumiwa na vikundi vya kijamii nayo ni muhimu katika kupambana na uoto huo wa Ziwa Victoria.

Inaelezwa kuwa wadudu hao waliingizwa kwa mara ya kwanza kwenye magugu maji ya Ziwa Victoria mwaka 1997, ambapo wamekuwa wakitumika katika mto Sepik nchini Papua New Guinea ambao nao unakabiliwa na tatizo hilo. 

Picha iliyopigwa kutoka angani kuonyesha aneo la Magugu maji

Madhara ya Magugu Maji

Ziwa Victoria ambalo ndio chanzo kikuu cha mto Nile kila mwaka limekuwa likipunguza uwezo wake wa kuhudumia shughuli mbalimbali zinazoratibiwa na binadamu. Inaelezwa kuwa athari za magugu maji zilijitokeza zaidi mwaka 1998 ambapo magugu hayo yalisambaa katika eneo kubwa na kuzuia meli kutia nanga, vijiji vingi vya uvuvi kupotea na kutishia baa la njaa katika maeneo yanayozunguka eneo hilo.

Mipango ya kutokomeza Magugu Maji

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan mwanzoni mwa mwaka huu aliwataka wanachama wa  nchi zinazounda Umoja wa Bonde la mto Nile kufanya utafiti kubaini sababu za kuwapo magugu maji katika Ziwa Victoria ambayo yamekuwa yakisababisha upungufu wa maji katika Mto Nile na kutafuta njia za kudumu kuhifadhi rasilimali hiyo.

Wanachama wa bonde hilo wana jukumu la kushirikiana katika kufikia malengo ya Sita ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ili kuwezesha upatikanaji wa maji safi na salama sambamba na kuondoa tofauti zinazoweza kutokea za kimaslahi katika rasilimali maji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *