Connect with us

Afya

Mambo 5 ambayo mtu hawezi kukwepa muda mfupi kabla ya kufa

Published

on

Una majuto yoyote? Naamini watu wengi wana majuto (regrets) kwasababu wamefanya baadhi ya maamuzi yenye matokeo hasi au hawakufanikiwa kupata yale waliyoyatarajia yangetokea katika maisha yao.

 Lakini majuto yetu yanapata nguvu wakati tunakaribia mwisho wa maisha yetu hasa siku chache kabla ya kifo.

Kwa miaka mingi, Bronnie Ware,  Muuguzi na Mshauri wa masuala ya afya katika nchi ya Australia, amekuwa akifanya kazi katika kitengo cha Kuwapunguzia wagonjwa maumivu huku akijikita kuwasaidia wale ambao wana hali mbaya na wanakaribia kufa. 

Wagonjwa wake walikuwa wazee wenye matatizo makubwa ya kiafya wakisubiri kufa. Alitumia muda mwingi kuwapa ushauri, faraja na kuwapunguzia maumivu ya akili na mwili ambayo yanakuja mtu anapokikabili kifo.

 Kifo sio jambo la kufurahisha na kukubalika kwa watu wengi; tunapendelea kutofikiri au kuzungumzia. Habari ya kusikitisha ni kwamba kila mtu atakufa kwa wakati wake.

 Kujua unaenda kufa wiki chache zijazo ni jambo linaloumiza sana. Bronnie amekuwa akishuhudia hali wanayoipata wagonjwa wake muda mfupi kabla ya kufa ambapo wengi wao wanajikana, halafu wanapata hofu, hasira, majuto, kujikana zaidi na mwisho kukubali hali halisi ya kinachoenda kutokea.

Kama sehemu ya kazi, Bronie amekuwa akiwauliza wagonjwa wake kuhusu majuto waliyonayo katika maisha na kama kuna jambo ambalo wangelifanya kama wangepewa nafasi ya pili ya kuishi.

Katika majibu yote aliyoyapata kutoka kwa wagonjwa wake, aligundua majuto 5 ambayo yamekuwa yakijurudia sana. Yafuatayo ni majuto ambayo wagonjwa wanajutia sana muda mfupi kabla ya kufa:

 

1) Natamani  ningetimiza ndoto na malengo yangu na sio maisha ambayo watu wengine wangetarajia kutoka kwangu

Kwa mujibu wa Bronnie, anasema hili ndio juto la kawaida kwa watu wengi. Watu wakifahamu kuwa maisha yao yanafika mwisho, ni rahisi kuangalia nyuma na kukumbuka ndoto na malengo yote ambayo hawakutimiza lakini hawana ujasiri tena wa kutekeleza.

 Anaeleza kuwa kushindwa kutimiza malengo kwa watu hao ni kwasababu waliwekeza nguvu zao kutekeleza matakwa ya watu wengine- kawaida ni familia, marafiki na jamii.

 Mmoja wa wagonjwa wake aitwaye Grace alimwambia Bronnie anaahidi kutekeleza ndoto zake zote na kuishi maisha yake kwa utoshelevu bila kujali watu wanasema nini.

 Bronnie anasema kwa muda mrefu ndoa ya Grace haikuwa na furaha, na mume wake alikuwa akitibiwa nyumbani. Majuto makubwa ya Grace ni kuwa hakuwa na uwezo wa kuzifikia ndoto zake kwasababu ya kumuuguza mume wake kwa muda mrefu.

 

 2) Natamani ningeimarisha mahusiano ya familia

 Kwa mujibu wa Bronnie anasema majuto ya aina hii yamemkuta kila mwanaume mgonjwa aliyemuuguza huku wanawake wakiwa wachache. Wengi wao walikuwa wakifanya kazi kwa saa nyingi na kuzisahau familia zao.

 Majuto yao yalikuwa ni kukosa ukaribu kwa watoto na wake zao. Walipouliza nani atafanya tofauti ikiwa atapata nafasi ya pili, majibu yalishangaza sana. Wengi wao waliamini kuwa wangerahisisha maisha na kufanya maamuzi sahihi ya kutumia muda mwingi na familia.

Kwa jinsi hiyo tunaweza kuyapa maisha nafasi ya kupata furaha na kuimarisha upendo na amani kwa watu walio karibu yetu.

 

 3) Ningekuwa na ujasiri wa kuelezea hisia zangu na kuongea kile ninachokiamini

 Bronnie anaendelea kusema kuwa wagonjwa wake wengi waliamini kuwa hawaheshimu hisia zao na hawakuongea yale waliyoyaamini kwasababu walitaka kudumisha amani na watu.

 Wengi wao walichagua kutokabiliana na hali ngumu, watu hata kama walidharirishwa. Ili kutuliza hasira, walijijengea maumivu na uchungu kati mioyo yao na mwisho yakaathiri afya zao. Jambo baya zaidi ni kukumbatia vinyongo na uchungu ambapo huathiri hisia na kuzuia mafanikio yetu.

Kuzuia aina hii ya majuto katika maisha ya baadaye ni muhimu kuelewa kuwa busara na kukabiliana na matatizo ni sehemu ya kuimarisha mahusiano na kutengeneza furaha.

 Kwa kuongea yale yaliyopo moyoni tunatoa hisia za kweli na kupunguza hatari ya kujenga machungu na majuto ambayo yanaweza kutuumiza.

 

4) Natamani ningekaa karibu na marafiki zangu

Bronnie amegundua kuwa wagonjwa wake wanakosa ukaribu na rafiki zao na wanajuta kwanini hawakutumia muda mwingi na marafiki hao kama ilivyowapasa.

 “Kila mmoja anawakumbuka rafiki zake wakati wa kufa”, anasema John-Paul Iwuoh, Mtaalamu na Mshauri wa biashara na ujasiriamali.

 Wakati afya na ujana ukiteteleka na kifo kinakaribia, watu wanatambua kuwa urafiki na baadhi ya watu ulikuwa na thamani kuliko utajiri na mafanikio. Bronnie anaongeza kuwa yote hayo yanatokea wakati wa mwisho wa safari ambapo mtu hukumbuka upendo na mahusiano mazuri.

 Tunaishi katika dunia yenye shughuli nyingi na kutusahaulisha kuwa tuna marafiki ambao wanaweza kutupatia furaha na thamani katika maisha.

 

5)Natamani ningeishi kwa furaha

Wagonjwa wa Bronnie hawakutambua hadi walipofika mwisho wa maisha yao kuwa furaha ni uchaguzi. Wanatamani wangefahamu kuwa furaha sio jambo la kukimbilia na kujipatia utajiri, kukubalika katika jamii na masumbufu ya maisha.

Wakiwa kwenye vitanda vya mauti, wagonjwa hao wanatambua kuwa wangechagua furaha bila kujali hali za maisha- utajiri au umaskini.

John-Paul Iwuoh anasema wakati mwanadamu akiwa mzima na mwenye afya anawekeza nguvu zake kujipatia vitu, utajiri, hadhi, madaraka na mafanikio. Na tumekuwa tukiamini kuwa hivi vitu vitatuletea furaha.

 Walipoulizwa wanaweza kufanya tofauti, hili ndilo jibu walilolitoa: Jifunze kuridhika na kukubali vitu vizuri katika maisha yako. Na hii ndio njia ya kweli ya kupata furaha.

  

Inawezekana kuishi bila kuwa na majuto?

John-Paul Iwuoh anasema hakuna mwanadamu aliyekamilika, na anapata mashaka juu ya ‘maisha ya ukamilifu’. “Natumaini kila mmoja awe na majuto katika siku yake ya kufa. Lakini nafikiri jambo la muhimu ni kuwa na majuto machache kadiri tuwezavyo”.

Hata hivyo, Iuoh anasema kufa ukiwa na majuto machache ni kuishi maisha kwa kiwango kinachostahili na kutambua kuwa unaweza ukafa wakati wowote. Katika yote hakuna anayefahamu siku ya kufa kwake.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Afya

Watumishi wa afya 200 kupatiwa mafunzo ya utoaji dawa ya usingizi kuokoa maisha wajawazito

Published

on

Kufuatia upungufu wa wataalamu wa dawa za usingizi (anaesthesia), serikali itatoa mafunzo ya dawa za usingizi kwa watumishi wa afya 200 katika vituo vya afya vya upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito.

Hatua hiyo inakuja ikiwa imepita miezi 6 baada ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kutangaza kuanza kutoa shahada ya dawa ya usingizi (Bsc. Anaesthesia Nursing).

Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano serikalini cha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaeleza kuwa mafunzo hayo yatatolewa sambamba na uboreshaji wa huduma ya upasuaji wa dharura kwa wajawazito ili kuokoa maisha ya wanawake na watoto ambao hufariki kwa kosa huduma muhimu za uzazi kwenye vituo vya afya.

“Mkakati wa kuhakikisha huduma za afya kwa akina mama wajawazito zinakuwa salama na uhakika kwa kuandaa rasilimali watu, miundombinu ya majengo na vifaa vitakavyowezesha huduma hizi ikiwemo upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito wakati wa kujifungua,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, vifo 556 vitokanavyo na uzazi kwa kila viumbe hai 100,000 huripotiwa kila mwaka katika maeneo mbalimbali nchini. Maana yake ni kwamba watoto na wajawazito hufariki hasa wakati wa mama akijifungua.

Aidha, serikali itaboresha vituo vya afya 288 vya serikali vilivyopo nchini ili kuviwezesha kutoa huduma ya dharura ya upasuaji kwa wajawazito ambapo waaguzi katika vituo hivyo watapatiwa mafunzo ya dawa za usingizi ili kuokoa maisha ya akina mama na watoto wachanga.

Utekelezaji wa mafunzo hayo ni matokeo ya ushirikiano wa Wizara ya Afya na Mfuko wa Pamoja wa Afya ambapo zaidi ya sh1,079 bilioni zimepatikana kufakisha mafunzo hayo ya dawa ya usingizi kwa wauguzi na matabibu waliopo kwenye vtuo vya afya nchini.

“Fedha hizo zitasomesha watumishi wapatao 200, kati ya watumishi hao 100 watapata mafunzo yao katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na MOI, watumishi 50 watafanya mafunzo katika hospitali ya KCMC, na 50 watafanya mafunzo hayo kwenye hospitali ya Bugando,” imefafanua taarifa ya wizara.

Lengo la serikali ni kuhakikisha ifikapo 2019 na kabla ya 2020 vituo vyote vya afya vinavyomilikiwa na serikali vinakuwa na watumishi maalum wa kutoa huduma ya dawa ya usingizi kwaajili ya wapasuaji wasiopungua wawili kwa kila kituo.

Mafunzo hayo ya mwaka mmoja ni mpito wakati serikali ikiendelea kukamilisha taratibu za kurasimisha utoaji wa shahada ya kwanza ya kutoa dawa ya usingizi katika Chuo cha MUHAS katka mwaka huu wa 2018/2019.

Hali halisi ya huduma ya dawa za usingizi nchini
Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa kuna upungufu mkubwa wa madaktari wenye utaalamu wa kutoa dawa ya usingizi hasa wakati wa huduma ya upasuaji ambapo kwa sasa waliopo ni asilimia 1.2 tu ya mahitaji yote.

Ili kuweza kukidhi mahitaji yote ya huduma hiyo wanahitajika madaktari 2000, lakini waliopo sasa ni madaktari 30 pekee.

Kufuatia changamoto hiyo Januari 31, mwaka huu wadau mbalimbali wa afya na elimu walikutana na kujadili namna ya kuondoa changamoto hiyo na kupendekeza mtaala utakaotumika kufundishia kozi ya Aesthesia kabla ya kuupeleka kwa Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU).

” Ni kweli kumekuwepo kwa changamoto hiyo ya watalaamu wa dawa hizo lakini sasa mpango huu ukikamilika maana yake tutaongeza idadi ya madaktari kamili maana hawa waliopo wengi ni wale ambao wamesoma kozi kwa mwaka mmoja au miwili.

” Mafunzo yakianza kutolewa hapa chuoni Muhimbili wataweza kuchukua wanafunzi 200, Bugando 50 na KCMC 50 jambo ambalo litaongeza idadi kubwa ya watalaamu ili kuweza kufikia lengo letu la kuwa na wataalamu 2000 nchi nzima,” alinukuliwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya.

Continue Reading

Afya

Vyakula hivi vitakulinda dhidi ya athari za kiafya za uchafuzi wa hewa

Published

on

Tunaishi katika ulimwengu unaokabiliwa na athari kubwa za mabadiliko ya hali ya hewa. Moja ya athari hizo ni kuongezeka kwa joto na kupungua kwa mvua katika maeneo mbalimbali. Athari hizi zinagusa moja kwa moja afya ya binadamu.

Ripoti ya mabadiliko ya hali ya hewa ya mwaka 2017 imeonesha kuwa kuongezeka kwa joto kunaathiri afya ya binadamu kwa kiasi kikubwa. Ripoti hiyo inatoka kundi la vyuo mbalimbali na mashirika tofauti ya Umoja wa Mataifa inasema watu wengi wanaathirika na joto pamoja na mlo hafifu sambamba na kusambaa kwa magonjwa.

Moja ya kisababishi cha mabadiliko ya hali ya hewa ni uchafuzi wa anga. Uchafuzi wa anga ni kuchanganyika kwa hewa asili katika anga na vitu kama vile moshi, majivu, gesi za kemikali katika hali na kiwango ambacho huathiri sifa ya hewa na kusababisha madhara kwa binadamu na viumbe vingine.

Baadhi ya vitu na vitendo huathiri vibaya anga letu. Baadhi ya vitu hivyo ni kama gesi na moshi unaotoka kwenye viwanda, moshi kutoka kwenye magari, marashi, dawa ya kuuwa wadudu shambani na kadhalika.

Lakini umewahi kujiuliza kuwa aina ya chakula unachokula kinaweza kukusaidia kukabiliana na athari za kiafya zinazotokana na uchafuzi wa hewa?

Wanasayansi katika utafiti wao uliotolewa hivi karibuni, wanaeleza ulaji wa chakula cha Mediterania ( Mediterranean diet) chenye matunda mengi, mbogamboga, nafaka isiyokobolewa, samaki, maharage jamii ya soya, mafuta ya mizeituni na mayai yanaweza kuwalinda watu dhidi ya athari za afya zinazotokana na uchafuzi wa hewa.

Wanasayansi hao kutoka Shule kuu ya Udaktari ya NYU ya Marekani, walichambua data za watu takribani 550,000 wenye wastani wa umri wa miaka 62 kwa miaka zaidi ya 17 ambapo waliwapanga watu hao kwenye makundi kulingana na ulaji wao unaoendana na chakula cha Mediterania na kulinganisha na muda waliokaa kwenye hewa iliyochafuliwa.

Walibaini kuwa watu ambao walizingatia kula vyakula vilivyotajwa hapo juu walikuwa na uwezekano mkubwa wa kuepuka magonjwa na vifo vinavyotokana na uchafuzi wa hali ya hewa. Magonjwa hayo ni yale ya mfumo wa upumuaji, moyo na kansa.

                                   Vyakula  jamii ya Mediterania

Vyakula hivyo jamii ya Mediterania vina uwezo mkubwa wa kukabiliana na vimelea vya maambukizi ya magonjwa kwa mtu ambaye atazingatia kwa usahihi kutumia katika maisha yake.

Uchafuzi wa hewa unasababisha athari mbaya za kiafya kupitia hewa ukaa na mlo wa Mediterania una virutubisho muhimu kupambana na vimelea vya magonjwa,” anasema Mwandishi Mtafiti wa utafiti huo, Chris Lim wa Chuo cha NYU.

Lim anasema vyakula vya aina nyingine vinaweza kusaidia kukabiliana na athari hiyo. “Nilipoangalia kila mchanganyiko wa chakula cha Mediterania, kina matunda, mbogamboga na mafuta yanayoweza kupambana na athari za hewa chafu,” anasema.

Utafiti kuhusu ulaji kama unaweza kuzuia athari za kiafya za uchafuzi wa hewa bado haujahakikiwa na kukubalika kisayansi. Lakini utafiti huo sio wa kwanza kutafuta uhusiano wa mlo na athari za kiafya za uchafuzi wa hali ya hewa.

Wakala wa Uhifadhi wa Mazingira wa Marekani (U.S. Environmental Protection Agency (EPA)) unatafiti kama mlo unaweza kumlinda mtu dhidi ya athari za uchafuzi wa mazingira. Pia wanatafiti ili kujiridhisha kama virutubisho hivyo vinaweza kutumika badala ya dawa za kitabibu na kwa kiasi gani mtu anatakiwa apate virutubisho hivyo kumhakikishia usalama dhidi ya uchafuzi huo.

Hata hivyo, bado watu wanashauriwa kutumia zaidi matunda na mbogamboga kwenye milo yao ya kila siku ili kupata faida mbalimbali za kiafya.

Continue Reading

Afya

Ulaji mbaya wa chakula watajwa kusababisha kansa ya matiti kwa wanawake

Published

on

Thamani ya maisha haiko kwenye muonekano wa mtu na vitu vinavyomzunguka bali kwenye chakula anachokula kila siku ili kuwa na afya njema. Lakini umewahi kujiuliza, chakula kinawezaje kupunguza uwezekano wa kufa kutokana na magonjwa ikiwemo kansa?

Utafiti mpya uliofanyika huko Marekani umebaini kuwa kwa sehemu mlo kamili unaweza kupunguza hatari ya kufa kwa kansa.

Mtafiti Dk. Rowan Chlebowski wa Kituo cha Taifa cha Uuguzi cha City of Hope na wenzake walichambua takwimu za wanawake 48,000 waliosajiliwa katika mpango wa Afya ya Mwanamke unaoratibiwa katika vituo 40 nchini Marekani.

Awali wanawake wote walipata vipimo na hakuna aliyegundulika kuwa na kansa ya matiti lakini 20,000 kati yao walishauriwa kubadilisha mlo na kupunguza ulaji wa mafuta kwa asilimia 20 katika milo yao ya kila siku.

Pia waliambiwa wale zaidi matunda, mbogamboga na nafaka zisizokobolewa. Wanawake wengine hawakupewa maelekezo yoyote ya kuzingatia mlo kamili lakini walifundishwa kuhusu lishe nzuri na mlo wenye afya.

Baada ya miaka nane ya kuwafuatilia wanawake hao, watafiti hao waliangalia idadi ya kansa ambazo wanawake hao walitibiwa na zile ambazo zilisababisha vifo. Walibaini kuwa wanawake ambao walitumia kiasi kidogo cha mafuta walikuwa na hatari ndogo ya kufa kwa kansa ya matiti kwa asilimia 22, ukilinganisha na wanawake wengine.

Pia wanawake hao walipunguza kwa asilimia 24 hatari ya kufa kwa kansa zingine ikiwemo kwa 38%  magonjwa ya moyo ikilinganishwa na wanawake wa kundi ambalo walipata elimu ya mlo.

“Tunachokiona ni matokeo halisi,” anasema Dk. Chlebowski. Tafiti za awali ziliangalia madhara kabla ya uchunguzi wa kansa, lakini utafiti huu ulichambua kwa kiasi gani mlo unaweza kumuathiri mtu baada ya uchunguzi.

“Tulichobaini ni kuwa ushauri wa mlo baada ya uchunguzi wa kansa ya matiti ulikuwa muhimu kuliko kabla ya uchunguzi.”

                        Ulaji wa matunda na mboga unasaidia kupunguza hatari ya kupata kansa

Hata hivyo, utafiti huo ulibaini kuwa wanawake ambao wanazingatia kutumia kiasi kidogo cha mafuta katika maisha yao wana nafasi kubwa ya kuepuka kansa ya matiti.

Kutokana na idadi ya watu walioshirikishwa kwenye utafiti huo, Dkt. Chlebowski anasema wazo la kuhusisha mlo katika programu ya matibabu lilikuwa ni muhimu ili kupata matokeo chanya katika kukabiliana na kansa ya matiti kwa wanawake.

Watafiti hao wanaendelea na uchunguzi ili kufahamu kama ulaji wa chakula unaweza kuwa sehemu ya matibabu ya kansa ya matiti. “Inahamasisha kwasababu tunajaribu kuziba pengo kati ya mtindo wa maisha na mchakato wa kibaiolojia uliopo nyuma ya ugonjwa huo.”

 

Kansa ya matiti

Saratani ya matiti ni ugonjwa ambao huwapata wanawake na unatokana na athari za chembe ndogo ama seli kwenye matiti na matokeo yake ni kwamba hubadili mfumo wa kawaida wa kukua na kuongezeka.

Mabadiliko haya huanza polepole na yanaweza yakachukua muda mrefu hadi mtu kuweza kujua kama ana matatizo hayo. Ikiwa katika hatua hizo za mwanzo kwa kawaida huwa hakuna maumivu jambo hilo ni moja ya mambo ambayo huchangia baadhi ya wagonjwa kubaini tatizo hilo wakati tayari limekomaa.

Ni kutokana na sababu hizo, wanawake hutakiwa kuchunguza afya zao mara kwa mara kwasababu ugonjwa huweza kutibiwa kirahisi iwapo utabainika mapema.

Miongoni mwa dalili za saratani ya matiti ni uvimbe kwenye matiti ama makwapani. Titi kubadilika kiumbo, titi kutoa majimaji yaliyochanganyika na damu ama chuchu kuingia ndani.

Zipo aina mbalimbali za tiba na mojawapo ni upasuaji. Upasuaji huu kwa kawaida hufanywa katika hatua za mwanzo. Njia nyingine ni tiba ya mionzi au kupewa dawa. Jambo la kukumbukwa ni kwamba ugonjwa huu unaweza kusababisha kifo iwapo hautabainika mapema na kupatiwa tiba mwafaka.

Njia ambayo mtu aweza kujilinda asiathirike na saratani hii ya matiti ni kujichunguza mara kwa mara ili kubaini mapema na kupatiwa dawa.

Mwanamke anapaswa kuchunguzwa mara moja kwa mwaka ili kuona kama ameathirika na ugonjwa huo au la.

Continue Reading

Muhimu Kusoma