Haki za binadamu zinapokanyagwa, nchi haitakuwa salama

Jamii Africa
SAMSUNG

Ifikapo Desemba 10 kila mwaka, dunia huadhimisha siku ya Azimio la Haki za Binadamu lililoasisiwa mwaka 1948 na kuwa tamko rasmi linaloainisha haki za msingi ambazo kila binadamu anatakiwa azipate.

Dhima ya kuazimisha siku hiyo ni kutathmini kwa kina hatua zilizopigwa na nchi wahisani katika kutetea na kulinda haki za binadamu. Pia kuangalia mapungufu na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa mkataba huo wa kimataifa.

 Kifungu cha 18 hadi 21 cha Azimio hilo kinaelezea haki za msingi ambazo jamii ikizipindisha, mweleko wa jamii hiyo hauatakuwa na mwisho mzuri kwa watawala na wataliwa. Haki hizo ni pamoja na Uhuru wa Vyombo vya Habari, uhuru wa kutoa maoni/kujieleza, kukusanyika, kupata taarifa na kuishi.

Ikiwa zimebaki siku chache kuifikia siku hiyo muhimu duniani, Tanzania inashuhudia baadhi ya matukio yanayoashiria ukiukwaji wa haki za msingi za raia wake huku wale waliopewa jukumu la kuzilinda hawawajibiki ipasavyo kuhakikisha ustawi wa raia unazingatiwa.

Huu ni wakati wa nchi kujithmini kama tuko katika njia sahihi kuimarisha kwa sababu tuliridhia Mkataba wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa na ule wa Afrika kuwa tutalinda haki za binadamu.

Haki ya kukusanyika

Kifungu cha 21 cha Mkataba huo kinaeleza kuwa kila mtu anayo haki ya kushiriki katika mkutano na chama kwa hali ya amani. Mtu ye yote asilazimishwe kuwa manachama wa chama fulani.

Tumeshuhudia kuzuiliwa kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ambayo ilikuwa inawapa fursa wananchi kuwasiliana na viongozi wa kisiasa. 

Baadhi ya wanasiasa hawako huru kufanya shughuli zao, wengine wanatishwa, kushambuliwa na hata kuwekwa kifungoni kwasababu wanatoa maoni ambayo yanaathiri maslahi ya viongozi katika jamii.

Hali hiyo ikiendelea inaweza kusababisha ukatili wa kisiasa na kuitumbukiza nchi katika machafuko  na wananchi kuchukua maamuzi magumu ya kubadili uongozi wa kidemokrasia.

“Sisi watanzania tuna unafiki wa ndani kwa hata viongozi tunaowapata wanawasilisha tabia zetu za ndani za kunyimana uhuru wa kujieleza. Mfumo wetu wa vyama unaundwa na tabia za ndani na zina akisi aina ya viongozi tunaowapata.  Hili taifa litaenda kwenye ukatili wa ajabu wa kisiasa”, amesema Dkt.  Vicensia Shule kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Madhara mengine  ni kudhoofisha mfumo wa kisiasa ambapo watu wachache kuwa na maamuzi na sauti juu ya rasilimali za nchi na kuharibu mfumo wa ushindani baina ya vyama vya siasa.

 

Uhuru wa Maoni na kujieleza

Kumekuwa na jitihada mbalimbali za kuzuia watu kutoa maoni yao na kueleza yale wanayoamini kuwa yanaakisi mstakabali wa maisha yao.

 Baadhi ya watu wameendelea kupaza sauti licha ya vitisho vya kisheria wanavyopewa. Mfano ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kumbusho Dawson kupitia ukurasa wake Facebook alionyesha kasoro za ujenzi zilizopo kwenye hosteli za Magufuli zilizopo katika chuo hicho lakini alikamatwa na polisi ili ajieleze kuhusu nia yake ya kuandika mambo kama hayo kwenye mtandao.

Takwimu za Twaweza zimebainisha kuwa mwaka 2015 pekee watu 358 walikamatwa kwa kutoa lugha mbaya na mwaka uliofuatia, 2016 watu 911 walikamatwa kwa kosa hilohilo. Na hawa walionekana ni wachochezi kwa sababu waliongea mambo ambayo serikali haikutaka kuyasikia.

 

Uhuru wa Vyombo vya Habari na Kupata taarifa

Kifungu cha 19 cha Azimio la Haki za Binadamu kinaeleza kuwa, Kila mmoja ana haki ya uhuru wa kutoa na kueleza maoni yake; haki hii inahusu pia uhuru wa kushikilia maoni yake bila kuingiliwa kati, na uhuru wa kutafuta na kutoa habari na maoni kwa njia yo yote bila kujali mipaka

Kutungwa kwa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Huduma za Habari (2016) na Sheria ya Takwimu (2015) kumetajwa kuwa ni jitihada za kisheria za kubana uhuru wa vyombo vya habari na watu kupata taarifa ikizingatiwa utekelezaji wake unaleta changamoto katika baadhi ya maeneo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media, Maxence Melo akizungumzia  kuhusu Uhuru wa Vyombo vya Habari na Uhuru wa Maoni, amesema Serikali haifanyi vema na jitihada za wazi zinahitajika kuboresha upande huu. Pia ameonesha kutoridhishwa na kufungiwa kwa magazeti kadhaa kwa kauli ya Waziri tu na uvamizi uliofanywa kwenye kituo cha runinga cha Clouds Media.

Hata hivyo, Maxence amesema serikali inavihitaji Vyombo vya Habari na Asasi za Kiraia katika kuwezesha mapambano dhidi ya Ufisadi hivyo ni vyema kutoa nafasi kwa wadau kushiriki kikamilifu  maendeleo ya Taifa.

“Uhuru wa kuongea na Bunge huru vimesaidia haya kuibuliwa awamu zilizopita, awamu hii ikitoa uhuru wa kutosha basi  vyombo vya habari vitakuwa vimeshaibua mengine makubwa ambayo yatachangia juhudi za kupambana na ufisadi.” amesema Maxence.

 Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Tanzania Media Foundation (TMF), Ernest Sungura amesema ili jitihada za kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari zifanikiwe nchini, wamiliki wa vyombo vya habari wanapaswa kuboresha utendaji wa vyombo vyao kwa kubuni vyanzo vingine vya mapato na kuongeza weledi kwa waandishi na wahariri.

“Muundo wa uendeshaji wa vyombo vya habari lazima ubadilike ili kuwepo na uhuru wa uhariri. Lazima vyanzo vya mapato na teknolojia zibadilike ili kuendana na wakati”, amesema Sungura.

 

Kushambuliwa na Kupotea kwa watu

Uhuru wa kwenda popote bado unatatizwa na matukio ya kutekwa na kushambuliwa kwa baadhi ya watu ambao wanadhaniwa kuwa na maoni tofauti na watawala. Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alishambuliwa na watu wasiojulikana kwa risasi na mpaka leo walitekeleza uharifu huo hawajakamatwa.

Pia baadhi ya watu akiwemo Msaanii Roma Mkatoliki, mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda na mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wametekwa na watu wasiojulikana aliyefanikiwa kuachiwa ni Roma pekee lakini wengine haifahamiki wako wapi.

Matukio kama hayo yanaleta hofu kwa wananchi na kutengeneza hisia hasi dhidi ya wanaowajibika kuwalinda wananchi na mali zao.

 

Suluhisho

Kulingana na mazingira yaliyopo ya kuminywa kwa misingi ya  demokrasia inayohimiza uwazi na uwajibikaji, wananchi bado wana nafasi kubwa ya kusimama na kudai mambo ya msingi yanayohusu maendeleo yao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *