WAKATI maumivu ya Dar es Salaam kupamba orodha ya shule 10 zilizofanya vibaya matokeo ya mitihani wa Kidato cha Nne 2016 bado hayajapoa, kuna uwezekano wa mkoa huo kuongeza maumivu mengine, kwani ratiba ya mitihani ya Kidato cha Sita imekwishatoka.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), mitihani hiyo inatarajiwa kuanza Jumanne, Mei 2, 2017 na kumalizika Mei 19, 2017.
Mitihani hiyo huenda ikatoa taswira mpya kwa Mkoa wa Dar es Salaam, ambao umeporoka kwa kiasi cha kutisha katika matokeo ya kidato cha nne baada ya shule zake sita za Kitonga, Nyeburu, Mbopo, Mbondole, Somangila Day na Kidete zilikuwemo kwenye orodha ya ‘Shule 10 mbovu’ zikiungana na shule za Masaki ya mkoani Pwani, Dahani ya Kilimanjaro, Ruponda kutoka Lindi na Makiba kutoka Arusha.
Kwa bahati nzuri, matokeo ya Kidato cha Sita mwaka 2016 Dar es Salaam ilifanya vizuri kwa kuingiza shule mbili za Feza Boys na Feza Girls ikiungana na Arusha ambayo nayo iliingiza shule mbili za Kisimiri iliyoongoza na Ilboru.
Orodha ya shule 10 bora katika mitihani ya kidato cha sita ilihusisha shule za Alliance Girls (Mwanza), Marian Boys (Pwani), Tabora Boys (Tabora), Kibaha (Pwani), Mzumbe (Morogoro) na Tanahimba (Mtwara).
Katika ufaulu huo wa asilimia 98.87, ambao ulishuka kwa asilimia 0.93 ikilinganishwa na mwaka 2015, Dar es Salaam pia ilikuwa miongoni mwa mikoa iliyotoa ‘shule zilizofanya vibaya’ ambapo shule kongwe ya Azania ilishika nafasi ya 9
Unguja ndiyo iliyoongoza kwenye orodha hiyo kwa kuwa na shule saba ambazo ni Mpendae, Ben Bella, Tumekuja, Jang’ombe, Kiembe Samaki, Al-Ishan na Lumumba, wakati shule nyingine zilikuwa Green Bird Boys (Kilimanjaro) na Tanzania Adventist (Arusha).