Licha ya juhudi mbalimbali za serikali na wadau wa uhifadhi wa mazingira kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki, imeibuka aina nyingine ya plastiki ambayo isipodhibitiwa itahatarisha zaidi uhai wa vyanzo vya maji na afya za binadamu.
Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba imepiga marufuku moja kwa moja, utengenezaji, usambazaji, uingizaji nchini na matumizi ya mifuko ya plastiki nchini kuanzia mwaka 2017 hii pia inahusu matumizi ya mifuko ya plastiki inayofungia pombe maarufu kwa jina la viroba.
Matumizi ya mirija ya plastiki ambayo watu hutumia kunywea vimiminika kama juisi, soda, maji, vileo katika maeneo mbalimbali imeleta changamoto nyingine kwa watetezi wa mazingira ikizingatiwa kuwa matumizi yake ni makubwa na hatua za kudhibiti bidhaa hiyo hazionekani.
Kulingana na Umoja wa Mataifa (UN) mirija ya plastiki bilioni 1 hutumiwa kila siku na watu duniani kote na kuchangia tani milioni 12 za takataka za plastiki zinazoelekezwa kwenye bahari na mito.
Akiongea na kituo cha runinga cha Al Jazeera, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Lonely Whale amesema, “Hapa Umoja wa Mataifa pekee tunatumia mirija ya plastiki milioni 500 kwa siku”.
Kutokana na asili yake, mirija hiyo hutumiwa mara moja kisha kutupwa na hairudishwi tena kwenye matumizi mengine ili kulinda afya za watu ambao wanatumia. Lakini matumizi hayo ni tishio kwa uhai wa vyanzo vya maji na binadamu.
Utafiti wa Jukwaa la Uchumi wa Dunia (2016) unaeleza ikiwa matumizi ya mirija ya plastiki yakiendelea kwa kasi iliyotajwa hapo juu, wanatabiri kuwa hadi kufikia 2050 kutakuwa plastiki nyingi baharini kuliko samaki.
Mirija ya plastiki ikiwa kando kando ya ufukwe wa. Picha na Santa Barbara County Board of Supervisors
Madhara kwa viumbe wa majini
Mirija ya plastiki ni tofauti na aina zingine za plastiki. Mirija hiyo ni rahisi kuvunjika katika vipande vidogo vidogo na huchukua muda kuoza. Samaki huviokota vipande hivyo na kuvitumia kama chakula. Plastiki hizo huchangia asilimia 50 ya vifo vyote samaki.
Plastiki hizo huingia baharini au mtoni kwa njia ya mawimbi ya bahari au mabaki ya vyakula vinavyotumiwa kwenye meli. Katika nchi za Afrika ikiwemo Tanzania iko katika hatari ya kupata madhara makubwa kwasababu ya usimamizi usioridhisha wa rasilimali za maji ambapo taka za viwandani na nyumbani huelekezwa kwenye mito, maziwa na bahari ambavyo ni vyanzo muhimu vya maji nchini.
Kemikali zilizopo kwenye mirija ya plastiki huingia kwenye maji; samaki hutumia kemikali hizo ambazo zimechanganyika na maji ya bahari na mito ambapo mzunguko huo humfikia binadamu baada ya kula samaki walioathiriwa na kemikali hizo..
Mwandishi wa makala haya alitembelea duka moja la kuuza juisi ya matunda lilipo Mwenge, Dar es Salaam ambapo alikuta mirija hiyo imesambaa pembeni mwa duka hilo na hakuna juhudi za kuikusanya na kuiweka mahala salama. Baada ya matumizi wateja hutupa chini na hata wasimamizi wa duka hilo hawafaji juhudi kudhibiti hali hiyo.
Muhudumu mmoja wa duka hilo anasema mirija hiyo ni midogo sana kwahiyo sio rahisi kuikusanya pamoja kama zilivyo chupa za maji: “Unajua mirija hii ya plastiki ni midogo halafu kila mteja anatumia mara moja tu kisha hutupwa”.
Hata alipoulizwa kama anafahamu mirija hiyo ni chanzo kikubwa ca uchafuzi wa mazingira, mhudumu huyo alibainisha wazi kuwa hafahamu na kazi yake ni kuwahudumia wateja wake katika mazingira ya usafi.
Mirija ya plastiki tayari kwa matumizi
Wadau wa mazingira
Kutokana na aina hiyo mpya ya plastiki ambayo matumizi yake yameshika kasi huku mamlaka mbalimbali hazijagundua hatari yake, mji wa Seattle uliopo Marekani chini ya taasisi ya Lonely Whale wameanza kampeini ya kuhamasisha na kubadili tabia za watu juu ya matumizi ya mirija ya plastiki na kutafuta njia sahihi ya kuhifadhi rasilimali ya bahari.
Kampeini hiyo imejikita zaidi kuwashauri watu kubadili mirija ya plastiki na kutumia mirija inayotengenezwa kwa miti, chuma na vioo au kuachana kabisa na matumizi ya mirija hiyo.
Akizungumza na vyombo vya habari, Kiongozi wa mji wa Seattle, Becca Fong amesema: “Jambo la muhimu ni kuwaelekeza watu waache na kufikiri kama kweli wanahitaji mirija hiyo? Unaenda kutumia dakika 5 mpaka 10 halafu unatupa na inakwenda kwenye ardhi”.
Kuanzia Julai 2018, Seattle watazuia matumizi ya mirija ya plastiki kwenye migahawa ikiwa ni hatua ya kupunguza matumizi ya bidhaa hiyo. Mpaka kufikia septemba mwaka huu wamefanikiwa kuondoa mirija ya plastiki milioni 2.3 kwenye vyanzo vya maji.
Mamla za uhifadhi wa mazingira Tanzania na wananchi wanashauriwa kuanza kuchukua hatua mapema dhidi ya matumizi ya mirija ya plastiki kabla hayajaleta madhara makubwa kwenye mfumo wa maisha.