Watu wanaofanya mazoezi ya kukimbia na kutembea wana mambo mengi yanayofanana. Wote wanatumia njia mbalimbali kufikia malengo ya kuimarisha afya ya mwili.
Changamoto inajitokeza ni kwenye faida na hasara za mazoezi ya kukimbia au kutembea ambapo kila kundi lina hoja zake ambazo zinatofautiana na kundi lingine. Wakimbiaji wanafikiri kukimbia kunachoma mafuta haraka, kuongeza mzunguko wa damu na kumaliza haraka mazoezi. Watembeaji wanasema athari za viungo vya mwili ni ndogo, mapigo ya moyo huenda vizuri.
Njia ya kuondoa utata kwa makundi yote mawili ni kuwaruhusu wataalamu wa mazoezi kushauri faida na watu gani ambao wanastahili kukimbia au kutembea kulingana na afya ya mtu.
Mazoezi ya Kutembea
Kutembea kunaepusha madhara mbalimbali ikiwemo majeraha ya magoti, kiuno na nyonga. Kukimbia kunatumia nguvu nyingi za kukanyaga ardhi na kusababisha msuguano kwenye mifupa na muunganiko wa mifupa kuliko mazoezi ya kutembea.
Pia kuna muunganiko thabiti wa akili na mwili wakati wa kukimbia. Hata hivyo, kukimbia na kutembea kunaimarisha afya ya akili lakini kutembea kuna faida kubwa zaidi. Stephanie Powers, Mkufunzi wa Afya ya akili na mwandishi ya kitabu cha Thyroid First Aid Kit, anashauri watu watembee haraka na kurusha mikono ili kufaidika zaidi.
Mazoezi ya kutembea
Mazoezi ya Kukimbia
Haina mjadala kuwa kukimbia kunachoma zaidi mafuta ya mwili kuliko kutembea. Daktari Patrick Suarez, Mtaalamu wa afya ya Mifupa ameliambia Jalida la POPSUGAR kuwa mafuta ya mwili yanachomwa mara mbili zaidi kwa wakimbiaji kuliko watembeaji kwasababu kiwango cha mapigo ya moyo huongezeka maradufu.
Ikiwa lengo lako ni kupunguza uzito wa mwili basi kukimbia ni njia rahisi kuliko kutembea ambayo hutumia muda mrefu kuchoma mafuta.
Sio tu wakimbiaji wanachoma mafuta mengi, lakini kukimbia kunatengeneza homoni ya peptide YY, ambayo inawasaidia kutumia mafuta kidogo baada ya mazoezi. Kulingana na utafiti uliofanywa na Chama cha Fiziolojia cha Marekani (2008) unaeleza kuwa kukimbia kunazuia mafuta kutumika kwa wingi mwilini.
Mazoezi ya kukimbia
UAMUZI
Ikiwa unafanya mazoezi ya kutembea au kukimbia unaweza kuendelea nayo ili kupata faida zilizoainishwa hapo juu. Kulingana na Jo-Ann Houston, Mkuu wa Mafunzo wa kampuni ya GYMGUYZ anasema jambo la muhimu ni kutambua na kufurahia faida za muda mfupi na muda mrefu za kila zoezi unalofanya.
Ikiwa ndio unaanza kukimbia au kutembea, chagua zoezi ambalo litakufanya ujisikie vizuri kulingana na mwili wako na malengo unayotaka kuyapata. Jaribu kukimbia na kutembea ili kufanya uchaguzi sahihi wa aina ya mazoezi yanayokufaa. Muhimu chagua zoezi ambalo utadumu nalo muda mrefu.