Mbunge Leticia Nyerere aangua kilio hadharani

Sitta Tumma

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Mageni Nyerere (CHADEMA), amejikuta akimwaga machozi hadharani, baada ya kutembelea na kujionea mrundikano mkubwa wa wanafunzi katika Shule ya Msingi, Hungumalwa iliyopo Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

Mbali na wanafunzi hao kurundikana darasani, pia mbunge huyo machachari alijionea wanafunzi hao wakiwa wameketi chini kwenye vumbi katika shule hiyo, jambo lililoonekana kumkera, hivyo kujikuta akidondosha machozi mbele ya kadamnasi.


Hali hiyo ilitokea wakati mbunge huyo Nyerere (pichani), alipofanya ziara ya kutembelea miradi mbali mbali ya maendeleo, pamoja na kusikiliza kero za wananchi wa jimbo hilo la Kwimba, ikiwa ni maandalizi ya kukusanya kero na hoja mbali mbali atakazokwenda kuziwasilisha katika vikao vya Bunge linalotarajiwa kuanza hivi karibuni mjini Dodoma.

Kufuatia hali hiyo mbaya, ambapo zaidi ya wanafunzi 45 wanasoma darasa moja, mbunge huyo wa viti maalumu, aliahidi papo hapo kutoa mabati 200 na mbao 85 ndani ya muda mfupi kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule mbili za Mwajikuga na Ibaya, zitakazosaidia kupunguza mrundikano wa wanafunzi hao shuleni.

"Hii hali siyo nzuri kabisa kwa maendeleo ya watoto wetu kielimu. Mrundikano huu siyo wa kawaida….inaniuma sana kuona watoto hawa wanakaa chini wakati Serikali ipo.

Katika hatua nyingine iliyoonekana kumkera pia mbunge huyo, ni adha kubwa ya maji safi na salama inayowakabili wananchi wa Ngudu wilayani humo, kwani wananchi wa mji huo walimueleza Leticia Nyerere kwamba, hivi sasa wanalazimika kunywa maji machafu kwa kuchangia na mifugo kutoka kwenye bwawa la Mwamasururu wilayani Kwimba.

Habari hii imeandaliwa na Sitta Tumma – FikraPevu, Kwimba

5 Comments
  • hapaswi kulia achukue hatua kama mbunge hii ndo tz imekuwa ni wachache mno alafu ajiulize kuna watoto wangapi wa vigogo hapo kama jibu sio hakuna

  • kwani kulia ni kutatua matatizo? hapaswi kulia cha msingi atafute njia mbadala ya kutatua changamoto zinazoikabili shule hiyo ili kufikia hali bora , lakini yoote hayo ni matokeo ya viongozi wabovu wa watokanao na chama tawala, ni ajabu kuwa na nchi masikini ndani ya nchi yenye utajiri wa kutosha kutatua kero kama hizo.

  • kwani ndio unaliona hilo sasa!! hata hapa dsm, kuna shule ya msing ipo mbagala (jina kapuni) its worse. for those who remember, some deligation went to visit with a Vx worth 250million and student crushed it with stones before one of our kigogo ran in the forest to save his life. If Iwas there I could be one of those students. one dest worth abou15000. one landcruser could make 16million desks. it could save more than 100000 schools run short of desks. hata wewe mama, ungelitembelea suzuk escudo ungesaidia shule zaidi ya 20 kupata madawati 50 kila darasa na ujenzi wa zaidi ya madarasa 70. brainstorm!!

  • kwaujumla hata mimi nashangaa kuona kwamba bado kuna wananchi wana pata kero ya maji na serikali ina jua alafu ina fumbia macho, niaibu;ukiaangalia kwa undani niwalipa kodi hawa wanao teseka.

  • Jamani mbona nimekuwa nikimsikia huyu mbunge wa viti maalum akiwahangaikia wakazi wa Kwimba kwani Kwimba hawana mbunge? Maana hata mwezi uliopita nilisoma akiwa gereza la Ngudu akiongea na wafungwa.Baada ya wiki mbili niliona akitoa misaada ya vyerehani kwenye kata zote za Kwimba. Jamani huyu mama ana mapenzi ya dhati na wana Kwimba. Leo tena nimemsikia bungeni akizungumzia swala la maji Kwimba. Jamani huyo mbunge wa jimbo yuko wapi?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *