Imeelezwa kuwa kukosekana kwa usawa wa utolewaji wa huduma za kijamii kwenye mfumo wa elimu kumeathiri matokeo ya ujifunzaji kwa wanafunzi wa shule za msingi nchini.
Kulingana na ripoti ya utafiti wa Uwezo Tanzania (2017) inayoendeshwa na taasisi ya Twaweza iitwayo : Je, Watoto wetu wanajifunza? Imebainisha wazi kuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja juu ya upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile maji na umeme, chakula na vyoo katika mazingira ya shule na ufaulu wa wanafunzi.
Utafiti huo ambao unatokana na takwimu zilizokusanywa mwaka 2015 ulihusisha wanafunzi 197,451 kutoka shule za msingi 4,750 nchini ambapo umebaini kuwa wanafunzi wanaosoma katika shule zenye huduma muhimu za kijamii walifanya vizuri katika majaribio ya darasani na mitihani ukilinganisha na wanafunzi ambao katika shule zao hakuna umeme wala maji.
Asilimia 64 ya watoto mkoani Dar es Salaam wenye miaka 9 hadi 13 wana uwezo wa kufaulu majaribio yote matatu yaani Hesabu, Kiswahili na Kiingereza, lakini Katavi ni asilimia 23 tu ya watoto wanaoweza kufaulu majaribio hayo.
UFAULU WA MAJARIBIO YA WANAFUNZI KATIKA MIKOA YA TANZANIA
Chanzo: Uwezo Tanzania
Ukitazama kwa makini utagundua wazi kuwa shule nyingi za mkoa wa Dar es Salaam zina huduma za maji na umeme ukilinganisha na maeneo ya pembezoni mwa nchi ikiwemo mkoa wa Katavi.
Ripoti hiyo inaeleza, “Mkoani Dar es Salaam, nusu ya shule (51%) zina huduma ya umeme, lakini Geita ni shule 2 tu (4%) kati ya 50 zinazopata huduma hiyo. Mkoani Geita, shule moja kati kumi (12%) ina huduma ya maji safi na salama lakini mkoa wa Kilimanjaro karibu shule 8 kati ya 10 (78%) zina huduma hiyo”.
Mgawanyo huo usio sawa wa huduma za kijamii unawaathiri zaidi watoto wanaosoma katika shule zilizopo pembezoni mwa nchi hasa maeneo ya vijijini ambako wazazi wengi hawajaelimika na wanakabiliwa na umasikini wa kipato.
ASILIMIA YA SHULE ZA MSINGI ZA SERIKALI ZENYE HUDUMA YA MAJI KIMKOA (2015)
Chanzo: Uwezo Tanzania
Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo jijini Dar es Salaam, Meneja wa Uwezo Tanzania, Zaida Mgalla amesema kukosekana kwa usawa katika sekta ya elimu kunaathiri ujifunzaji wa wanafunzi darasani na hata maendeleo ya eneo husika.
“Takwimu za Uwezo zinaonesha wazi kuwa kukosekana kwa usawa kwenye mfumo wa elimu kunajidhihirisha katika matokeo ya kujifunza, rasilimali na huduma zinazopatikana shuleni”.
Athari za mfumo huo usiozingatia usawa zinadhihirisha dhahiri kwamba maeneo ambayo yana huduma nzuri yamepiga hatua katika maendeleo ambapo kiwango cha umasikini kiko chini ukilinganisha na maeneo ambayo huduma hazipatikani; jamii zake bado ziko kwenye lindi la umasikini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze ameiambia FikraPevu kuwa, “Takwimu za Uwezo zinaonesha kuwa maeneo wanapoishi watoto yana mchango mkubwa katika kujifunza kwa watoto kuliko umasikini, kiwango cha elimu ya mama, iwapo mtoto amesoma shule ya awali au hata watoto wenye udumavu”.
ASILIMIA YA WANAFUNZI WANAOPATA CHAKULA CHA MCHANA KIMKOA (2015)
Chanzo: Uwezo Tanzania
Mitazamo ya Wadau mbalimbali
Prof. Mwesiga Baregu ambaye ni mjumbe wa Kamati kuu ya CHADEMA amesema kinachojitokeza katika elimu ya Tanzania ni mgongano wa maslahi ambayo yanachagizwa na wanasiasa kutumia ujinga na umasikini wa wananchi kama mtaji wa kujipatia nafasi za kisiasa na uongozi wa ngazi mbalimbali katika jami.
“Kilichobadilika katika nchi hii na kuturudisha nyuma kielimu ni kuwa Ujinga na Umasikini vilikuwa maadui lakini sasa Ujinga na Umasikini ni Mitaji ya Kisiasa”, amesema Prof. Baregu.
Kwa upande wake, Mmiliki wa shule moja hapa nchini, Joseph Mmbando amesema kinachochangia kufeli kwa wanafunzi wa shule za serikali hasa za pembezoni mwa nchi ni usimamizi mbovu wa shule na waalimu kutopewa heshima na stahili zao kwa wakati.
“Shule binafsi (private) zinafanya vizuri kwasababu ya uangalizi wa karibu wa wamiliki. Shule za Serikali nyingi uangalizi hauko vema hivyo si rahisi kufanya vizuri kitaaluma”, amefafanua Mwalimu Mmbando.
Naye Mhadhiri wa Shule ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Lulu Mahai amesema wazazi wanapaswa kushirikishwa kwenye masuala yote ya elimu ikiwemo kufahamu maendeleo ya watoto wao wawapo shuleni, “Uelewa, Elimu na ‘Exposure’ ya mzazi vina mchango mkubwa sana katika maendeleo ya mwanafunzi kielimu”
Kichocheo kingine cha kukosekana kwa usawa ni ufinyu wa bajeti na ruzuku inayoelekezwa kwenye shule kwaajili ya uboreshaji wa miundombinu.
“Bajeti zinazopelekwa kwenye shule nadhani zinatolewa bila kuangalia aina ya shule na uhalisia wake. Shule zina hali tofauti na idadi tofauti ya wanafunzi lakini zinapewa kiasi sawa. Kwa hili hatujajipanga vizuri”, amebainisha Dkt. Luka Mkonongwa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Suluhisho
Akitoa suluhu ya kukosekana kwa usawa, Zaida Mgalla amesema, “Habari njema ni kwamba sasa tuna mifano hai ya nini kinachopaswa kufanyika ili kurekebisha hali hii. Serikali inapaswa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa watoto na wilaya za mwisho haziachwi nyuma”.