Edward Mdaki — Migomo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini vilivyolazimishwa kufunguliwa baada ya uchaguzi wa oktoba 2010, imefikia kilele . Ni kilele kwa sababu ilianzia kwingineko na kwa madai yanayofanana. Kote walikogoma awali walikuwa wakilalamikia ucheleweshwaji wa fedha za kujikimu kutoka bodi ya mikopo (HESLB).
Wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar-es-salaam sehemu ya mlimani ambao walianza kuhamasishana kugoma siku ya alhamisi na siku iliyofuata kuanza maandamano kuelekea ikulu, wana madai tofauti. Hawa wanalo tatizo tofauti.Ingawa ni tatizo tofauti kimsingi limewagusa wanafunzi wote wa elimu ya juu nchini.Wanaitaka serikali iongeze fedha ya kujikimu wanayokopeshwa na serikali kwa siku kutoka 5,000 ya sasa hadi 10,000.
Wanafunzi wa UDSM wamepaza sauti. Serikali kama kawaida yake imeagiza wapigwe mabomu. Mabomu ndiyo msemaji wa serikali kwa kila tatizo inalopelekewa. Wakati wa uchaguzi watu walipochoka kusubiri utangazwaji wa matokeo waliandamana , polisi wakapiga mabomu. Hayo yalitokea Mbeya mjini, Mbozi, Arusha mjini, shinyanga mjini, Mwanza na kwingineko.
Mapema mwaka huu polisi walitumia ubabe wa aina ileile hadi kuua baadhi ya waandamanaji waliokuwa wakielekea kwenye uwanja wa mkutano wakiongozwa na viongozi wa CHADEMA. Hii ni huko Arusha.
Chuo kikuu cha Dodoma- UDOM walipogoma kushinikiza hoja zilizo wazi kabisa za kuwepo kwa mafunzo kwa vitendo walipigwa mabomu. Baada ya kupigwa mabomu mtoto wa mkulima ,Waziri mkuu Mizengo Pinda alikwenda huko na kukiri kuwa wanafunzi walikuwa na hoja ya msingi. Akaagiza ishughulikiwe.
Wanafunzi wa UDSM wameandamana kudai nyongeza ya fedha za kujikimu kwa siku,wamepigwa mabomu.Mawaziri Mh.Shukuru Kawambwa wa elimu na Mh.Shamsi Vuai Nahodha jumamosi wamekutana na menejimenti ya chuo na wawakilishi wa wanafunzi na kukiri kuwa madai ya wanafunzi ni ya msingi.Hapa tunajiuliza,je Serikali ni lazima ipige watu wake mabomu ndipo itambue uzito wa madai yao ya msingi?
Hili la upigaji mabomu tuliache kwanza maana linahitaji makala nzima kulijadili. Yafaa pia kuwapongeza polisi na wanajeshi wa Tunisia na Misri walioapa kutokutumia nguvu dhidi ya waandamanaji waliomng’oa madarakani Ben Ali wa Tunisia na wanaomtaka Rais Hosni Mubaraka wa Misri aondoke pia.
Akitoa taarifa inayoonekana kuchelewa mno,mshauri wa wanafunzi wa UDSM, Dr. Martha Qorro amewataka wanafunzi kuacha mgomo na maandamano kwa kuwa wizara inayohusika na mikopo katika serikali ya wanafunzi-DARUSO tayari iko katika majadiliano na Serikali ili kuweza kutambua gharama halisi ya maisha kwa siku sasa ili mabadiliko yaingizwe katika mchakato wa bajeti ya 2011/2012.
Katika taarifa yake hiyo kwa wanafunzi aliyoitoa siku ya ijumaa wakati maandamano yakiendelea, Dr. Quorro anasema viwango vya fedha za kujikimu kwa siku vimekuwa vikibadilishwa kama ifuatavyo;
Ø Hadi kufikia mwaka 2005/2006 wanafunzi walikuwa wakikopeshwa sh. 2500/= kwa siku.
Ø Mwaka 2006/2007 kiwango hichio kilipandishwa hadi sh. 3500/= kwa siku na
Ø Mwaka 2007/2008, kiwango hicho kilipandishwa hadi sh. 5000/= wanayoendelea kukopeshwa hadi sasa.Hii inamaana kuwa fedha wanayopewa kwa siku imebaki sh. 5000/= kwa miaka mine iliyopita.
Ni aibu kubwa kwa taifa linalotaka kujenga jamii yenye amani,haki na usawa kusubiri maandamano ndipo serikali ielewe kuwa sh.5000/= zilizomuwezesha mwanafunzi kujikimu kwa siku miaka mine iliyopita leo hazitoshi.Ipo aibu nyingine, ikiwa Dr. Qorro ambaye ni mshauri wa wanafunzi UDSM alijua kuwepo kwa mchakato wa kubadili kiwango hiki,kwa nini hakuwapa taarifa wanafunzi? Au thamani ya taarifa hizi ilikuwa sawa na matokeo ya ubunge huko Mbulu,Rombo,Shinyanga mjini,Ilemela,Nyamagana na kwingineko?
Tujiulize swali jingine .Ni mara ngapi serikali imeboresha mishaara ya wafanyakazi wake kuanzia mwaka 2007/2008 hadi leo kwa madai ya kupanda kwa gharama za maisha ? Hawa wanafunzi kulikoni? Ni vigezo gani vinavyohitajika kubainishwa ili kuwezesha fedha yao ya kujikimu kuongezwa? Je wanayo maduka yao yenye bei tofauti? Hoteli,mabasi yao je? Yaani je wapo kweye Tanzania nyingine tofauti yenye kuhitaji utafiti tofauti na ule unaowahusu watanzania wasiokuwa wanafunzi?
Kuna hoja nyingine. Mwaka 2007/2008 wakati kiwango cha sh. 5000/= kikiidhinishwa kwa siku kila mwanafunzi alikuwa na hakika ya malazi katika hostel za vyuo.Serikali imeongeza idadi ya wanafunzi chuoni hapo kwa kasi ya ajabu bila kuongeza hosteli za kuwawezesha wanafunzi hao kupata malazi kwa gharama nafuu. Hili limefanyika hivyo katika vyuo vyote nchini vya umma na visivyokuwa vya umma. Fedha ya malazi kwa kila mwanafunzi hujilipia kutoka katika kiwango hicho hicho cha sh.5000/= anazopewa kwa siku sambamba na nauli yake,chakula,maji sabuni na mahitaji mengine yote. Kwa sasa mwenye uhakika wa malazi katika hosteli za chuo UDSM ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza.Wengine wote hupaswa kupanga vyumba mtaani ambako bei ya chumba kwa mwezi inafika Tsh.50,000/=
Kuna hoja nyingine ndani ya maandamano haya:
Wanafunzi wa elimu ya juu wanafikiri,wanatafiti na kufanya uchambuzi wa mambo mengi ya kijamii, kisiasa,kiuchumi na kiutamaduni. Wanaangalia namna serikali inavyowatendea wao na kuwapendelea wengine. Wanashangaa serikali inayowafanya waishi kwa shida huku ikijiandaa kulipa Dowans sh.94 bilioni. Wanaona usimamizi wa rasilimali za taifa haufanywi kwa usahihi.
Wakati wao wakiishi kwa shida UDSM wameshuhudia rais kikwete akiongoza kikao cha kamati kuu mchana na kuidhinisha malipo ya billion 94 Dowans na usiku akiendesha harambee ya kukusanya sh. 1 bilioni ya kujenga hostel ya chuo hicho.Hapa wanaona serikali inakosa umakini.
Ni bahati mbaya kuwa jeshi letu la polisi lilifundishwa intelijensia ya unabii na utabiri wa kutokea vurugu katika maandamano pekee. Ikiwa lingejifunza intelijensia ya kubaini hoja za wanaotaka kuandamana lingeitaka serikali kutoa majibu kabla ya kuwepo kusudio la maandamano. Ni kwa ajili ya udhaifu wa intelijensia ya polisi na serikali kwa ujumla hoja hizo na nyingine zifuatazo hazina majibu ila waandamanaji watapigwa mabomu.
Ukosefu wa ajira: serikali imeasisi mpango wa shule ya sekondari kwa kila kata. Ikahimiza wanafunzi wasome ualimu.Watu wakaitikia wito. Katika hali ya ajabu imeajiri baadhi tu ya walimu hawa huku shule zikikosa walimu. Waliokosa ajira sasa hivi wataungana na wanaomaliza vyuo mwaka huu. Wote wataandamana baadaye mwaka huu kudai ajira serikalini. Natarajia watapigwa mabomu. Miaka inakwenda haraka, 2012 itafika,wengine watahitimu tena, Serikali itasema uchumi haujakuwa kwa kasi iliyotarajiwa huku ikiingia mikataba feki na hivyo itashindwa kuajiri. Wataandamana kudai ajira nao watapigwa mabomu. Wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka 2010 katika shule ya Benjamini Mkapa katikati ya jiji kati yao 282 wamepata sifuri. Hawa watawakusanya wenzao waliofeli hapa DSM, wataungana na wahitimu wa vyuo walionyimwa ajira ili wawafundishe kuwaponya wasifeli; wataungana na machinga waliozuiwa kuuza bidhaa wanapopataka ili mradi hawavunji sheria; wataungana na wafanyakazi wasiopandishwa madaraja kazini; wataungana na waliochagua Kimau akashinda lakini mshindi akatangazwa kuwa ni Njuguna, wote hawa kwa pamoja wataunda jeshi la waandamanaji wasiokuwa na silaha.
Wote wataunganishwa na wimbo unaowakilisha mahitaji yao. Kwamba wamechoka kuongozwa na viongozi wasiojali maslahi ya wanyonge. Intelijensia ya jeshi na serikali yake haizioni hoja hizi ila wakati wa maandamano watatabiri vurugu. Na hivyo watawapiga mabomu waandamanaji.
Serikali makini haisubiri maandamano ya jinsi hii yatokee. Hujitahidi kutenda vitendo visivyozalisha majeruhi wa tabaka tawala kwenye tabaka tawaliwa.
Waandamanaji wa UDSM walisikika wakisema nguvu ya umma haijawahi kushindwa na jeshi lolote duniani. Tuangalie mifano ya Afrika kusini na India enzi za Mahatma Ghandhi, Tunisia, Ufaransa, Urusi, China, Irani ya Ayatolla Khomenei na Kwingineko.
Watu wenye njaa hujua kuwa wanakaribiwa na kifo.Huona heri kuwaambia watawala tuna njaa wakawaua kama hawataki kuwasikiliza kuliko kukaa kimya na kufa kwa njaa. UDSM wanasema wanakufa njaa kwa sababu sh. 5000/= ya mwaka 2007 leo mwaka 2011 haitoshi. Je mabomu ndilo jawabu lao?