Baada ya Tanzania na Kenya kufanya mabadiliko ya kisheria katika sekta ya madini, ripoti mpya ya utafiti imeeleza kuwa hatua hiyo ni kikwazo katika kuvutia uwekezaji katika nchi hizo za Afrika Mashariki.
Taasisi ya Fraser ya Canada katika utafiti wake wa Makampuni ya Madini 2017, imetaja sheria hizo kama wingu zito kwa kampuni za kigeni kutokana na nchi hizo mbili kushika nafasi ya mwisho katika uvutiaji wa wawekezaji.
Katika taarifa yake ya mwaka, Fraser imeiweka Kenya katika nafasi ya pili kutoka mwisho duniani baada ya Guetemala na ya mwisho katika nchi za Afrika.
Kwa mujibu wa Fraser, taasisi inayoongoza kwa utafiti wa sera na mipango katika sekta binafsi, Tanzania iko miongoni mwa nchi za mwisho kwa kuvutia wawekezaji barani Afrika, na nafasi ya 78 katika ya nchi 91 zilizoshiriki utafiti huo duniani.
Tanzania imeshuka kutoka nafasi ya 59 kati ya nchi 104 mwaka 2016, kutokana na sheria mpya kuweka vikwazo kwa wawekezaji wa kigeni hasa katika utawala, kodi, usuluhishi na usalama.
“Mabadiliko ya kibunge nchini Tanzania, ambayo tayari yameanza kutendewa kazi yanapunguza nguvu ya mikataba na kuondoa nafasi ya usuluhishi wa kimataifa katika kutatua migogoro na serikali. Hili linaondoa uthabiti na kutengeneza mazingira magumu ya uwekezaji,” imeeleza ripoti hiyo.
Mwanahabari, Njiraini Muchira ambaye anafanya kazi na Jalida moja nchini Kenya alimuhoji, Mtendaji Mkuu wa Shirika la Madini la Kenya ambapo alikaririwa akisema, “Utafiti huo unawaambia watunga sera kwamba wawekezaji hawaichukulii Afrika Mashariki kama sehemeu nzuri ya uwekezaji, kwasababu kanuni siyo rafiki.”
Sheria za nchi hizo mbili zinataka mapato ya madini yachangie kiasi kisichopungua asilimia 10 kwenye pato la taifa (GDP) kutoka kiwango cha awali cha chini ya asilimia 1 kwa Kenya na 3.5% kwa Tanzania.
Taarifa kutoka Kenya zinaeleza kuwa, serikali imechapisha kanuni ambazo zinayataka makampuni ya kigeni kugawana hisa na serikali na kushiriki kwenye soko la hisa ili kukidhi matakwa ya sheria ya Madini ya mwaka 2016.
Kanuni hizo zinayataka makampuni ya kigeni kuorodhesha kiasi kisichopungua Dola za Marekani 100 milioni katika soko la hisa ili kuwawezesha wananchi wa Kenya kufaidika na sekta ya madini.
Sheria za nchi hizo mbili zinataka mapato ya madini yachangie kiasi kisichopungua asilimia 10 kwenye pato la taifa
Hata hivyo, wawekezaji wamesema tayari wamelemewa na gharama kubwa za shughuli za utafiti, kutokuwepo kwa takwimu sahihi za madini, jambo linalowalazimisha kufanya utafiti wao binafsi. Pia ulipaji wa fidia kwa wamiliki wa ardhi na asilimia 1 ya faida yao ambayo wanatakiwa kuielekeza kwenye maendeleo ya jamii.
Tanzania ilifanya mabadiliko makubwa kwenye sheria za madini ambapo zinaiwezesha kujadili mikataba ya madini na makampuni ya wawekezaji juu ya kodi, kiasi na aina ya madini yanayosafirishwa nje ya nchi.
Sheria hiyo ya Rasilimali Asilia ya mwaka 2017 inakusudia kuongeza kodi za madini, kuzilazimisha kampuni kujadili mikataba kabla haijaanza kutumika, inaruhusu serikali kumiliki asilimia 50 ya hisa za makampuni ya madini, kuhakikisha kampuni hizo zinawekeza katika mshine za kuchakata mchanga wa madini nchini na kutengeneza ajira kwa wazawa.
Kutokana na mabadiliko hayo, baadhi ya kampuni zimesitisha mipango yake ya kuwekeza Tanzania.
Kampuni ya Uwekezaji ya Tremont ya Uingereza imesitisha tenda na kampuni ya Cradle Resources ya Australia huku Shanta Gold ikisitisha kuchukua tenda na kampuni ya Helio Resource Corp.
Mabadiliko hayo ya sheria, yameshuhudia baadhi ya kampuni ikiwemo ya Acacia kupunguza utendaji na inatathmini mikakati yake ya kuendelea na shughuli zake nchini.
“Mazingira mazuri ni yale yanashabihana na viwango vya dunia vya usimamizi wa mazingira, ushindani wa kodi, kutokuwepo kwa matishio ya kisiasa na utawala mzuri wa sekta ya madini,” imeeleza ripoti hiyo.
Fraser imeitaja Finland kama nchi inayoongoza kuvutia uwekezaji wa madini ambapo kwa Afrika, Ghana inashika nafasi ya kwanza na 22 duniani. Guetemala ni nchi ya mwisho kabisa kwa sera mbovu za kuvutia wawekezaji. Nchi zingine ni Kenya, Argentina, Msumbiji, Bolivia, Venezuela, Romania, China na Nicaragua.