Mgongano wa sheria za kampuni, madini unavyoikosesha serikali mapato

Jamii Africa

Licha ya bunge kupitisha Sheria ya Kuzuia  Utakatishaji Fedha ya mwaka 2006, imeelezwa kuwa serikali ya Tanzania haina mfumo mzuri wa sheria wa kuweka wazi wanufaika wa umiliki wa kampuni za uzalishaji zilizosajiliwa nchini, jambo linalopelekea matumizi mabaya ya rasilimali za nchi.

Udhaifu huo unajitokeza kwasababu Sheria ya Kampuni ya mwaka 2002 inayohusu usajili wa kampuni binafsi, umma na zile za wawekezaji kutoka nje hazitoi haizilazimishi kuweka wazi umiliki wa kampuni husika.

Japokuwa Katiba ya Tanzania inawataka wanasiasa na viongozi wa umma kuweka wazi mali wanazomiliki, lakini utaratibu huo hauwahusu watu wote nchini wakiwemo wawekezaji katika sekta mbalimbali.

Sheria ya Kuzuia Utakatishaji Fedha ilianzisha Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu ambacho kinawajibika kupokea, kuchambua na kusambaza ripoti za miamala na taarifa muhimu za utakatishaji wa fedha na shughuli za ugaidi kutoka kwenye taasisi za fedha kulingana na uhitaji wa sheria hiyo.

Kulingana na utafiti wa shirika la Tax Justice Network (2018) juu ya usiri wa masuala ya fedha  unaeleza kuwa Tanzania inaweza kuwa inaendesha kampeni dhidi ya utakatishaji fedha, lakini bado imeshikilia msimamo wa kutunza usiri wa taarifa za akaunti za benki za watu wanaomiliki kampuni na wale wanaotoka nje ya nchi.

Ripoti ya utafiti huo inaeleza kuwa watu wengi kutoka nchi ya China na India wanaiona Tanzania kama eneo zuri kwa kuhifadhi utajiri wao. Licha ya sheria za kodi kuwapendelea wawekezaji, pia inasifika kwa sheria imara za siri hasa kwenye masula ya fedha.

Kutokana na sifa hiyo imeshika nafasi ya 73 kati ya 112 duniani ambazo zina sera nzuri za usiri kwenye masuala ya fedha lakini ina udhaifu wa utekelezaji wa sheria za kufuatilia taarifa za benki hasa wamiliki wa kampuni kutoka nje ya nchi. Kutokana na udhaifu huo kwenye sheria, imetoa nafasi ya matumizi mabaya rasilimali za nchi.

Suala hilo linajihidhihirisha kwenye Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano (2016/17-2020/21) ambao unakusudia kukuza utawala bora ili kuhakikisha matumizi mazuri ya rasilimali za umma, kudhibiti rushwa, kuboresha huduma za kijamii, ukwepaji kodi na ukiritimba wa taasisi za serikali. Hata hivyo, Tanzania ilijitoa kwenye Mpango wa Uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi (OGP) ambao ulikuwa nguzo muhimu kupambana na rushwa.

Hali hiyo imeathiri sana sekta ya madini ambayo mara nyingi imekuwa ikikumbwa na rushwa na ufisadi. Hivi karibuni kampuni ya madini ya Acacia iligundulika kukwepa kodi; kwa mujibu wa kamati iliyoundwa na Rais John Magufuli mwaka jana ilibaini mapungufu mbalimbali katika mikataba ya madini ambayo imeliingizia taifa hasara kubwa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa kwenye Mkutano wa kupambana na Rushwa jijini London, Uingereza Mei 2016 aliahidi kuweka wazi taarifa za wanufaika wa umiliki wa makampuni katika sekta ya madini kwa umma.

Hata hivyo, Bado mfumo wa sheria za umiliki wa kampuni haujapatikana. Kulingana na Sheria ya Uchimbaji (Madini, mafuta na gesi) ya mwaka 2015 inazitaka kampuni kuchapisha majina ya wamiliki wao, lakini hakuna kanuni zinazoongoza sheria hiyo mpaka leo.

Ripoti iliyotolewa na kampuni ya Mawakili ya MM mwaka 2017 imehitimisha kuwa Tanzania haina mfumo wa sheria uliojitosheleza. Kwasababu hiyo hakuna mahitaji ya kisheria ya kuweka wazi wamiliki wa kampuni. Wakati huo huo Wakala wa Usajili wa Biashara na leseni (BRELA) haihitaji kampuni kuonyesha nani ana miliki kampuni na idadi ya hisa.

Msajili wa kampuni hana taarifa muhimu za wamiliki wa kampuni na kwa muktadha huo ni vigumu kubaini unufaika wa kampuni. Kutokana na juhudi za serikali kupambana na ufisadi hasa kwenye sekta madini lakini sheria bado hazijitoshelezi kufanikisha mapambano hayo.

 

Nini kinafuata?

Wakati huu ambapo nchi inatekeleza sera ya viwanda na Malengo ya Maendeleo ya 2025, ni muhimu mfumo wa sheria ukapitiwa, kufanyiwa marekebisho na kutekelezwa kwa agenda za uwajibikaji hasa kuihusianisha sekta ya madini na fedha kutekeleza majukumu yake kwa uwazi. Kutengeneza orodha ya wazi ya wamiliki wa makampuni iwe ni kipaumbele cha kwanza.?

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *