Mila na desturi, kikwazo cha wanaume kushiriki afya ya uzazi Tanzania

Gordon Kalulunga

MILA na desturi ni kikwazo moja wapo kinachokwamisha malengo ya milenia ya kupunguza vifo vya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kufikia asilimia 75 kati ya vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2015.

Kwa mujibu wa utafiti wa masuala ya afya ya uzazi ya Tanzania ya serikali mwaka 2010(TDHS), unaeleza kuwa kila siku wajawazito 23 wanapoteza maisha kwa matatizo mbalimbali ya uzazi wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.

Baadhi ya wanaume wana mawazo ya kimazoea kuwa kuongozena na wake zao Kliniki ni kama wamelishwa dawa za kupumbazwa(Limbwata).

Wanaume wengi wanasema kuwa kuongozana na wake zao kwenda Kiliniki si utamaduni wao.

Katika utafiti niliofanya kwa miezi sita katika mikoa kadhaa hapa nchini chini, imebainika kuwa bado hali hiyo ipo ingawa baadhi ya wanaume wameanza kuelimika na kushiriki pamoja na wenza wao kwenda sehemu za kutolea huduma za afya za kitaalam.

Katika wilaya ya Ileje mkoani Mbeya kijana Henry Kayuni anasema kuwa kutokana na mila za kabila la Wandali wanaume walikuwa hawaendi na wake zao Kliniki lakini kwa sasa akiwemo yeye anaongozana na mkewe ikiwa ni pamoja na kumpeleka mtoto Kliniki.

‘’Nilifanya hivyo tangu wakati wa mimba kwa ajili ya kujua afya zetu kwa pamoja hasa ugonjwa wa Ukimwi.’’ Anasema Kayuni.

Kijana Samson James mkazi wa Kijiji cha Kambubu wilaya ya Bunda mkoani Mara, anasema kuwa yeye ni mmoja kati ya vijana wanaojisikia vizuri kuongozana na mkewe kwenda Kliniki.

Anasema mbali na mwitikio huo, lakini kikwazo ni huduma duni wanazozipata hasa katika kituo cha afya cha Ikizu maarufu kwa jina la Nyamuswa.

‘’Tunaongozana na wenza wetu lakini tatizo ni huduma bora ambapo hata katika magonjwa ya kawaida tunapata vipimo tu, lakini dawa huwa tunanunua maduka ya dawa na endapo katika maduka ya dawa kungekuwa na vipimo tusingethubutu kwenda huko’’ anasema Samsoni.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kambubu Warioba Kiharata anasema kuongozana na mkewe kwenda hospitali siyo shida bali tatizo ni kupata huduma bora za afya hasa kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano ambapo kwa masikini ni tatizo!.

‘’Wananchi wengi hasa vijana wanahamasika kwenda na wake zao Hospitali hasa wakati wa kujifungua na malezi ya watoto, shida ni majibu yasiyoridhisha kutoka kwa wataalam wa afya, ukiwaambia kuwa wakusaidie mkeo anaumwa wanakuuliza kuwa sasa wao wafanyeje!’’ anasema Kiharata.

Anasema kutokana na hali hiyo, wananchi wa kijiji chao wamehamasishana kujenga zahanati ya kijiji na tayari wamekusanya mchanga na mawe.

‘’Kwa sasa katika kijiji chetu tunasubiri kibali cha kujenga zahanati ambapo wanaotukwamisha ni serikali hawataki kutupa ramani’’ anasema Mwenyekiti huyo.

Mjamzito Agnes Baraka anakiri kuwa wanashirikiana na mumewe katika kulea mimba na kushiriki kumpeleka hospitalini lakini anasema kuwa endapo mimba hiyo haitakuwa na matatizo atajifungulia nyumbani au kwa mkunga wa jadi kutokana na hospitali kutokuwa na huduma bora.

Naye Anna Japhet(35) anasema kuwa wakunga wa jadi wanatoa huduma bure na wale wanaotoza fedha ni Sh. 3,000 tofauti na hospitalini ambako mjamzito analazimika kununua karatasi, gharama za kitanda, na mafuta ya taa 1,000 jambo ambalo kutokana na uchumi wake anaona anamtesa mumewe.

Msaidizi wa mganga wa zahanati ya Bunda mkoani humo, Victoria Awino anasema kuwa katika zahanati hiyo ili kuhamasisha wanaume kushiriki katika afya ya uzazi wanawapa kipaumbele zaidi wajawazito wanaoenda na wenza wao.

‘’Mjamzito anayekuja na mumewe ndiye tunaanza kumuhudumia kisha tunaendelea na wengine ambao hawaji na waume zao’’ anasema Victoria.

Anasema kuwa baada ya kufanya hivyo, wanawake wengi wamekuwa wakijitokeza na waume zao kwenda kupata huduma za Kliniki kabla, wakati na baada ya kujifungua.

Anasema kwa sasa zahanati hiyo inahudumia wagonjwa kati ya 30 mpaka 40 kwa siku.

Mjamzito Nyangeta Makori mkazi wa kijiji cha Nyambono wilaya ya Musoma vijijini, kutokana na usafiri unaofaa kwa mjamzito kutokuwepo, alilazimika kukodi pikipiki na mumewe na kupita katika barabara mbovu kwa saa nne, huku akisikilizia uchungu kutoka Msoma vijijini mpaka Kituo cha afya cha Manyamanyama wilaya ya Bunda.

Alitoka saa 8;30 nyumbani kwake na kufika saa 11:30 jioni kisha kupokelewa katika kituo cha afya cha Manyamanyama, baada ya muda wa saa moja alijifungua mapacha, Doto akiwa na kilo 3.1 na Kulwa naye ana kilo 3.5.

Nyangeta anasema huo ni uzao wake wa tano ana watoto sita wote wakiume, watoto wa nne amejifungulia nyumbani akisaidiwa na wifi yake kwa kumshika sehemu ya mgongo wakati wa kujifungua na yeye kusukuma na kujifungua mtoto.

Kitu kinachosababisha Nyangeta kuzalia nyumbani watoto wanne ni kijiji anachokaa hakuna zahanati na hospitali iko mbali.

Wifi yake Nyangeta ambaye tunaweza kumwita shujaa, amemuokoa Nyangeta asipoteze maisha kwa kumshawishi kwenda katika kituo cha afya kujifungua pamoja na kumsindikiza kutoka musoma vijijini mpaka Bunda, lakini pia ndiye mwanamke aliyemsaidia kujifungua nyumbani watoto wanne.

Huyo ni mmoja wa wajawazito Tanzania wanaokumbana na shida wakati wa kutafuta huduma za kujifungua ikiwa pamoja na umbali, usafiri usio wa uhakika, umasikini na barabara mbovu.

Endapo mumewe hasingeweza kumkodia pikipiki hueda angefariki maana awali anasema alipohudhuria Kliniki aliambiwa mimba yake inamatatizo na alikuwa akiugua tofauti na mimba zilizopita.

Katika wilaya za Butiama na Musoma Mjini mkoa wa Mara, wajawazito wanapokwenda kliniki wanachangia huduma za upimaji kama kupima wingi wa damu wanalipia shilingi 1,000, kadi la kliniki wananunua shilingi 1,000.

Tatizo la kuchangia huduma kwa wajawazito kinyume na sera ya afya ya mwaka 2007 inayosema kuwa wajawazito watapata huduma bure, pia lipo katika wilaya ya Nachingwea mkoa wa Lindi, idadi ni kubwa ya wajawazito lakini wanakosa huduma bora ya kujifungua.

Pia katika wilaya ya Songea mkoa wa Ruvuma hali sio nzuri katika upatikanaji wa huduma za kliniki, katika zahanati ya Ifinga kwenye kijiji cha Ifinga wajawazito wanachangia huduma mbalimbali za kliniki, kupima ujauzito wanalipia shilingi 2,000, kupima wingi wa damu wnalipa shilingi 1500.

Kama mjamzito damu yake ni pungufu hupewa dawa za kuongeza damu kwa malipo ya shilingi 1,000.

Kwa upande wake ofisa mradi mwandamizi mawasiliano mradi wa CHAMPION Muganyizi Mutta, alipokuwa akitoa mada kwa baadhi ya waandishi wa habari mkoani Mbeya zinazolenga kushirikisha wanaume katika mapambano dhidi ya maambukizi ya (VVU), anasema kuwa ni vema wanaume wakajua haki za kushiriki Kliniki na wenza wao.

Mutta anasema mradi huo ni mradi wa kwanza Tanzania unaolenga kushirikisha wanaume katika mapambano chanya dhidi ya maambukizi ya VVU.

Anasema kinachokwamisha baadhi ya wanaume kushiriki katika huduma za afya na kwenda hospitalini na wake au wenza wao ni pamoja na mila na desturi zinazoeleza kuwa jukumu la kutunza mimba na kulea mtoto ni la mwanamke.

"Mbali na hilo pia kuna mitazamo ya kimazoea Stereotype ambapo mwanaume kwenda na mkewe kliniki jamii inamshangaa, hivyo umefika wakati jamii ibadilike na kuona suala la mimba kabla na baada ya kujifungua ni jukumu la wote yaani mwanamke na mwanaume'' anasema Mutta.

Mradi huo unasimamiwa na shirika la EngenderHealth na shirika mwenza linalojulikana kwa jina la FHI360 na kufadhiliwa na USAID ambapo wanaifikia jamii hasa wanaume kwa njia mbalibali ikiwemo mwanaume mmojammoja, mikusanyiko (jamii) na maeneo ya kazi.

Kupitia makala hii, ili jamii iweze kuepukana na ongezeko la VVU inapaswa elimu iwafikie kikamilifu wanaume wenye umri wa kuingia kwenye ndoa na walioko kwenye ndoa.

Lengo likiwa ni kujua umhumi wa kabla ya kupanga kuzaa watoto, wanandoa waweze kufika katika vituo vya afya na hospitali kupima afya zao ili hata kama watakuwa wameambukizwa au mmoja wao waweze kupata mbinu ya kutomwambukiza mtoto anayetarajiwa kuzaliwa.

Vipimo vinavyopimwa kwa mjamzito siku za kwanza ni pamoja na VVU, kipimo cha wingi wa damu (HB test), maambukizi ya kaswende na gonorea (VDRL test) na mfumo wa mkojo.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu 0754 440749 na Barua pepe;[email protected]

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *