Mimba za Utotoni, tatizo ni mtoto wa kike?

Jacob Mulikuza

JUMA lililopita, Rais John Pombe Magufuli alitoa agizo ya kuwa hakuna mwanafunzi aliyepata ujauzito atarudi shule kuendelea kwa masomo kwa kuwa serikali haiwezi kusomesha wazazi.

Wito huu wa Rais unaweza kuwa sehemu ya suluhisho la mimba kwa wanafunzi wa kike ila sio suluhisho bora kwa ustawi wa mtoto wa kike katika nyanja ya elimu.

Kwa maoni yangu, ni vyema tukajikita katika kutizama mzizi wa tatizo na kuweza kuondoa tatizo katika mzizi ili lisiendelee kujirudia badala ya kuishia kuangalia matokeo ambayo ni mimba yenyewe na kuishia kumhukumu mwanafunzi huyu kwa kumnyima elimu.

Natambua ya kuwa watu wengi wanadhani mwanafunzi kupata mimba ni swala la mwanafunzi husika kuwa muhuni tu ama tabia ya wanafunzi wa kike kupenda ngono.

Aina ya mawazo haya yanatokana na dhana za kibepari ambazo huaminisha watu ya kuwa tatizo la mtu husika ni tatizo lake mwenyewe na sio tatizo la mfumo husika. Hapa ndipo utasikia unaambiwa ya kuwa mtu yuu masikini kwa kuwa hajasoma, hajajiajiri, amelogwa, sio mchapa kazi na mengine mengi.

Aina hii ya mawazo tunayasikia kila siku kwa kuwa ubepari unaamini katika dhana ya ubinafsi na sio dhana nzima ya jamii. Hali hii ndio inayotukumba katika swala hili la mimba za wanafunzi tunafikiri ya kuwa hili ni tatizo la watoto wa kike kwa kuwa hawajieshimu, hawapendi masomo, wanatamaa ya ngono, pesa, wakaidi, hawana maadili na mengine mengi.

Kama ingalikuwa tatizo la mimba za wanafunzi ni lao moja kwa moja ama sababu kama hizo nilizotaja hapo juu zenye mrengo wa kibepari basi kuwafukuza shule ingekuwa suluhisho.

Kwa mtizamo wangu mimba kwa wanafunzi wa shule sio tatizo binafsi tu bali ni tatizo la kimfumo linalochangiwa kwa asilimia kubwa sana na mazingira.

Natambua dhana ya mazingira ni pana hivyo ntatumia nadharia ya Human Ecology kueleza maana ya mazingira katika muktadha huu.

Nadharia ya Human Ecology inasisitiza ya kuwa mazingira ya asili ama yale ya kutengenezwa na binadamu huchangia mabadiliko ya tabia ya mtu husika. Kwa mantiki hii, mazingira yanaweza kuwa yale yaliyotengenezwa na binadamu, mazingira ya asili na mazingira ya kijamii tamaduni ambayo mtu husika hupatikana.

Nadharia hii inatuonyesha wazi ya kuwa tabia ya mtu yeyete huchangiwa na mwingiliano alionao na mazingira yake. Kwa kusisitiza zaidi vile tunavyoona tabia za watu leo hii ndio mwingiliano alionao na mazingira yake ya asili ama yale ya kutengenezwa na mwanadamu mwenyewe.

Labda nitoe mfano kidogo, leo hii urembo na utanashati unatafsiri tofauti kutokana na mazingira ya sasa. Kwa wanawake ili waonekane warembo lazima watinde nyusi, wapake vipodozi, waweke nywele bandia na kuvaa mavazi tunayodhani ndo yakisasa.

Kwa wanaume, lazima uvae suruali za kubana mithili ya zile za kike, ushushe suruali nusu makalio, unyoe kiduku, kujichubua kidogo, kuvaa viatu bila soksi na kadhila.

Hiyo mifano hapo juu inatoa taswira ya namna mazingira yetu yanaweza kuwa na nguvu kubwa ya ushawishi kiasi cha kukufanya utende bila kutumia utashi kwani usipofanya utaonekana wa kale hivyo ili kuendana na mazingira binadamu aliyoyatengeneza lazima ufanye kawa wao ili ufanane nao.

Tukirudi katika swala la mimba za wanafunzi ambalo mimi naamini ya kuwa ni tunda la mazingira ambayo inawakumba wanafunzi wetu hawa. Na kama tunataka kutatua tatizo hili ni vyema tuanze na kurekebisha mazingira yale ambayo sio rafiki kwa wanafunzi wa kike ili kuondoa ama kupunguza kabisa tatizo la mimba za wanafunzi angali wako shuleni.

Hebu tutafakari kidogo, je, watoto wa kike kwanini hupata mimba nini hasa huwa kichocheo?

Kama nilivyosema hapo awali, wanafunzi hawa wakike huishi katika mazingira aidha yaliyo rafiki ama sio rafiki kwao. Hapa nitapenda kuangalia mambo kama umbali kufika shuleni, aina ya elimu inayotolewa shuleni, adhabu zitolewazo shuleni, mahitaji muhimu ya wanafunzi shuleni, umasikini, kukosa mlo wawapo shuleni, ukosefu wa vyumba vya kulala kwa wanafunzi watokao mbali, malezi hafifu, talaka, malezi kutokuwa ya jamii nzima, ombwe la maadili, elimu kutokuwa na mvuto, elimu isiyoleta matumaini ya ajira, tamaduni, siasa, ufisadi na mengine mengi.

Haya yote ni mazingira ama ya asili ama yale yakutengenezwa na mwanadamu yanaweza kuchangia yote kwa pamoja, ama kwa moja moja kwa asilimia nyingi sana mwanafunzi kupata mimba.

Tunapoamua kuwahukumu wanafunzi kwa kuwanyima fursa ya kusoma ni kanakwamba tunasema wanafunzi hawa wanaishi katika ulimwengu wao peke yao na hili ni kosa lao binafsi na sio kosa la mfumo wala mazingira.

Suluhisho la kweli katika vita dhidi ya mimba za wanafunzi ni kupambana na mazingira yanayowakumba wanafunzi wa kike badala ya kuendelea kuwakandamiza kwa kuwanyima haki ya kukosa elimu.

Endapo wanafunzi wa kike waliojifungua watakosa elimu ni dhahiri ya kuwa mzunguko wa umasikini utaendelea na kuongeza idadi kuwa ya watoto wa kike kutopata elimu na kuruhusu mgawanyiko baina ya wanawake na wanaume kuwa kubwa.

Nihitimishe kwa kusema, makatazo pekee sio suluhisho muhimu katika vita hii dhidi ya mimba za wanafunzi, bila kuyarekebisha mazingira yote yanayopelekea kuwepo kwa mimba za wanafunzi. Ni vyema sasa wizara ya elimu na idara zake husika itakafanya utafiti wa kina kugundua changamoto za kimazingira, binafsi na za kisaikolojia ili kuweza kuja na mbinu mbadala itakayokuwa na tija zaidi kwa watoto wa kike ili mapambano yawe ya kisayansi zaidi.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *