Biashara ya wanawake wanaouza miili yao inazidi kushika kasi katika mji wa Dodoma, hali ikijitokeza sana hasa wakati wa mikutano mikubwa ya kitaifa, ikiwemo Bunge na mingine ya vyama vya kisiasa.
Hata hivyo utafiti wa mwandishi wa makala hii umebaini kwamba asilimia kubwa ya wanawake wanaofanya biashara hiyo ya ngono wanatoka mikoa mbalimbali ikiwemo Morogoro, Dar es Salaam, Arusha,
Wanawake hawa wanafanyia shughuli zao katika baadhi ya mitaa maarufu kama Dodoma In ambapo husimama kando ya barabara huku wengine hupanga chumba kimoja wakiishi wanawake watano hadi kumi kwaajili ya kufanya shughuli hiyo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma,kamishina msaidizi mwandamizi David Misime amesema kuwa tatizo hilo ni kubwa na linapaswa kufanyiwa kazi ili kunusuru afya za wananchi kutokana na maradhi kama vile ukimwi na mengineyo.
Kamanda Misime anasema kuwa katika kipindi cha mwaka 2013 hadi 2014 jeshi la Polisi lilifanikiwa kuwakamata wanawake na wasichana wanaofanya biashara hiyo 65 katika mitaa mbalimbali ya mji wa Dodoma.
Kamanda Misime anasema kuwa wanawake hao walifikishwa mahakamani ambapo miongoni mwao walihukumiwa vifungo na wengine walitozwa faini.
Kamanda Misime amewatahadharisha wanawake wenye tabia hiyo kuacha mara moja kwani jeshi lake bado linaendelea kuwakamata na kuwafikisha mahakamani.
Msichana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Asha Bakari mkazi wa Dar-es-salaam,akizungumza na mwandishi wa makala hii amesema kuwa huwa anakuja Dodoma kufanya biashara ya kujiuza lengo lake ni kutafuta fedha ili aweze kujikimu,msichana huyo ameeleza kuwa yeye pamoja na wenzake wana utaratibu wa kutumia mipira ya kiume kwa ajili ya kujikinga na ukimwi.
Msichana mwingine Mariam john (25) ,kutoka Morogoro amesema kuwa yeye anafanya biashara hiyo kwa lengo la kupata fedha kwaajili ya familia yake,kwani ana watoto wawili ,na mume wake alifariki dunia hivyo hana msaada kutoka sehemu nyingine zaidi ya kutegemea biashara hiyo.
Amesema yeye hutumia kondomu na akifanya na mwanaume tendo moja humchaji shilingi elfu kumi,lakini bila kutumia kondomu humchaji shilingi elfu kumi na tano.
Mbunge Inocent Karogeles wa Morogoro kusini,amesema yeye huja Dodoma na mke wake,hajui iwapo kuna wabunge wanaohusika na mambo hayo.
Amesema kuwa masuala hayo ni imani ya mtu binafsi,lakini sio jambo zuri kama wapo viongozi wanaojamiiana na wasichana wanaouza miili yao .
Mbunge mwingine Peter Msigwa amesema kuwa yeye hajui lolote kama kuna wasichana wanaokuja Dodoma,wakati wa vikao vya bunge na mikutano mingine mikubwa ya kitaifa kwa ajili ya kufanya biashara ya ngono.
Kwa upande wake Abdsalaam Mohamed mbunge wa Jimbo la Mikumi amesema kuwa ni hali ya kusikitisha ambayo inaweza kusababisha maambukizi ya ukimwi kuendelea kuwa juu.
Amesema ipo haja kwa Serikali na taasisi mbalimbali kuwapitia wasichana hao katika maeneo yao na kuwapatia elimu na vipeperushi ili wabadili tabia.
Nao baadhi ya wakazi wa Dodoma,bwana James Nestory ambaye ni dereva wa teksi eneo la Jamatini amesema ni kweli kuna idadi kubwa ya wanawake katika mtaa wa Uhindini ambao huuza miili yao nyakati za usiku.
Amesema wengi husimama barabarani na kuita wanaume wanaopita kwa magari na hata wanaotembea kwa miguu.
Akizungumzia tatizo hilo mkuu wa mkoa Dodoma Dkt Rehema Nchimbi alielezea kusikitishwa na tabia hiyo,na aliwataka wasichana wenye tabia ya kuja Dodoma kwa lengo la kufanya biashara ya ngono kuacha mara moja na wajikite katika shughuli nyingine za ujasiriamali .
Amefafanua kuwa biashara hiyo sio tu inakwenda kinyume na tamaduni pamoja utu wa binadamu lakini pia ni dhambi na ni machukizo mbele za Mungu,mkuu huyo wa mkoa ameongeza kuwa ipo haja kwa wadau wote ,ikiwemo viongozi wa dini,tasisi zisizo za Kiserikali zikaunganisha nguvu kupiga vita tabia hiyo mbaya.
Kwa upande wake afisa ustawi wa jamii manispaa ya Dodoma bibi Hellen Minja ameeleza kuwa wanaandaa mkakati wa kupita maeneo yote wanaofanyia biashara hiyo haramu wasichana hao ili waweze kukaa nao na kuwapa elimu ya kushawishi waweze kuachana na tabia hiyo.
Baadhi ya wamiliki wa nyumba za kulala wageni mjini Dodoma,wamesema kuwa wateja wanaoingia kwenye nyumba zao hawawezi kujua kama ni wale wanaojiuza au wateja wa kawaida.
Miliki wa nyumba ya kulala wageni ya Kaita lodge anasema ni kweli wakati wa mikutano ya kitaifa wateja wengi huja bwana na bibi, tofauti na siku ambazo hakuna mikutano ya kitaifa.