Mkorogo wizara ya Mwakyembe na Mamlaka ya Bandari

Sitta Tumma

UDHAIFU umejitokeza ndani ya Wizara ya Uchukuzi baada ya Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe kuigeuka Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), kuhusiana na usimamishwaji wa kivuko cha cha Mv. Samar III kinachosafirisha abiria kati ya Jiji la Mwanza na Sengerema mkoani Mwanza.

Hali hiyo imeashiria kuwapo kwa utata katika maamuzi hayo, na sasa Wizara ya Uchukuzi, inaigeuzia kibao TPA ambayo aliiagiza kusitisha huduma za kivuko hicho bila kuwasiliana na uongozi wa serikali mkoani Mwanza.

mv-samar-mwanza

Kivuko cha MV Samar III

Taarifa iliyotolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo, Injinia Evarist Welle Ndikilo, imeeleza kwamba, Waziri Mwakyembe ametengua mara moja maagizo ya kusimamishwa kwa kivuko hicho kinachomilikiwa na Salum Ali, kwa madai kwamba yeye hana taarifa zozote kuhusu agizo hilo.

RC Ndikilo ambaye juzi alipingana na maamuzi ya Wizara ya Uchukuzi kuhusu kusimamishwa kwa kivuko hicho, leo aliiambia FikraPevu kwamba: "Waziri Mwakyembe ameeleza kushitushwa na taarifa ya Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), inayodai kupewa maagizo na wizara hiyo kuhusu kukisimamisha kivuko cha hiki. Na tayari ameanza kuchunguza ili kubaini 'mchawi' wa nani aliyetoa maagizo hayo, yanayoonekana kudharau madaraka ya Serikali ya mkoa wa Mwanza.

Januari 29 mwaka huu, kupitia barua yenye kumbukumbu namba MN/2/3/04 iliyoandikwa na kusainiwa na Kaimu Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Mwanza, Richard Msechu, ilimuagiza Mkurugenzi wa kampuni ya Samar III, Salum Ali kusimamisha mara moja huduma ya kivuko chake katika eneo la karibu na Kamanga, na kwamba barua hiyo ilieleza uamuzi huo umetolewa na Wizara ya Uchukuzi kwa kuiagiza Makao makuu ya TPA kukisimamisha mara moja kivuko hicho.

MV-SAMAR-barua

Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Uchukuzi,  aliagiza kusimamishwa kwa kivuko hicho cha Mv. Samar III, kwa madai kwamba gati lake limejengwa karibu na njia ya Reli ya mizigo, agizo ambalo baadaye lilitenguliwa na kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mwanza, baada ya kamati hiyo kuhofia kutokea maafa makubwa kutokana na kivuko cha Kamanga Ferry kuonekana kuzidiwa abiria na Mwakyembe hajatoa kauli yoyote wakati huo.

Katika kile kilichoonekana kama sinema, leo wananchi wa Kamanga wilayani Sengerema mkoani hapa, waliandamana wakiwa na mabango mbali mbali kumpongeza Waziri Mwakyembe na uongozi wa Mkoa wa Mwanza kwa kurejesha usafiri wa kivuko hicho, ambapo walimtaka Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba apime, atafakari na hatimaye ajiuzulu nafasi yake hiyo, kwa kile walichodai ndiye chanzo cha mgogoro huo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *