MUASISI na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alitangaza maadui wakubwa wa Tanganyika (baadaye Tanzania) kuwa ni ujinga, maradhi na umasikini.
Tangu uhuru wa Tanganyika, serikali na wananchi wamekuwa bega kwa bega, kuhakikisha maadui hao wanaondoka.
Hata hivyo, hadi leo, Tanzania ikiwa na zaidi ya miaka 50 ya uhuru, mapambano bado yanaendelea kuwaondoa maadui hao wakubwa wa maendeleo na ustawi wa jamii.
Kati ya maadui hao, mkubwa kabisa anaelezwa kuwa ni maradhi; kwamba ikiwa nchi itakuwa na wananchi wagonjwa, hakuna kinachoweza kufanyika, hivyo sharti, adui huyu apigwe kwa kila namna atoweke.
Hii ndiyo Zahanati ya Dakawa ambayo imefungwa kwa miaka mitatu sasa.
FikraPevu inatambua kuwa katika vita hivyo, wapo wanaozembea na kukwamisha jitihada za kutokomeza maradhi.
Mfano mzuri ni huu, kwamba fedha zinakusanywa, zahanati inajengwa, lakini baada ya kukamilika, inatelekezwa. Inaachwa kuwa nyumba ya wanyama na wadudu.
Hii ni zahanati ya Kijiji cha Dakawa, Kata ya Bwakila Chini, Wilaya ya Morogoro, ambayo kama ingekuwa inafanya kazi ingekuwa ikihudumia wakazi 3,892.
Pia huenda ingekuwa ikitoa huduma kwa wananchi wenye makazi jirani na kijiji hicho, hasa kutoka kata nzima ya Bwakila, yenye wakazi wanaotajwa na sensa ya mwaka 2012 kuwa ni 13,718.
Kukosekana kwa huduma hiyo muhimu, kunawalazimi wakazi wa vijiji vya jirani kupata huduma za afya katika Kituo cha Afya cha Duthumi.
Kilio cha wananchi
Hussein Selegewi anasema kuwa anashangaa kuona viongozi wa wilaya kushindwa kufungua zahanati ya kijiji cha Dakawa wakati jengo la zahanati limekamilika.
Anaiambia FikraPevu kuwa jengo la zahanati hiyo lilikamilika tangu mwaka 2014, lakini halifanyi kazi na kwamba hakuna taarifa rasmi zilizotolewa na serikali ya wilaya kuhusu kutokufunguliwa kwa jengo hilo.
Kutokana na kushindwa kuanza kufanya kazi kwa zahanati hiyo, Selegewi anasema wanalazimika kutembea umbali wa kilomita 5 kutafuta huduma za afya katika kituo cha afya cha Duthumi au zahanati ya Bwakila.
Kwa upande wake, Shija Mwanza anasema kuwa jengo la zahanati hiyo lilijengwa kwa nguvu za wananchi, lakini serikali ina kigugumizi katika kufungua zahanati hiyo.
“Tunaiomba serikali kupitia wizara ya afya kuingilia kati sakata hili ili kuona ni jinsi gani ya kutusaidia tupate huduma ya afya karibu,” Sija anaiambia FikraPevu akiamini kuwa ujumbe wake utafika kunakohusika.
Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu.
Nasra Shabani anasema ukosefu wa huduma za afya unawaathiri wanawake, ambao hutumia takribani saa 3 kusaka huduma za afya nje ya kijiji wakati jengo lipo, ila huduma hakuna.
Kutokana anaiambia FikraPevu kuwa kukosa huduma katika jengo hilo la zahanati, anaiomba serikali ya mkoa kuliangalia suala hilo na kulipatia ufumbuzi.
“Wakinamama tumeteseka kubeba mawe, kuchota maji katika ujenzi wa zahanati yetu,miaka 3 imepita jengo limekamilika lakini halifanyi kazi,”anasema.
Rehema Jackson anasema kuwa waathirika wakubwa katika huduma ya afya ni wanawake, wakati mwingine wanapata ujauzito na kushindwa kuhudhuria kliniki kutokana na ukosefu wa huduma karibu.
Anasema kuwa wanashindwa kufanya shughuli za uzalishaji ndani ya familia kwani hulazimika kutumia muda wa saa sita kutafuta huduma ya afya.
Anaongeza kuwa miradi ya afya inayoibuliwa na wananchi wa vijijini inatakiwa kupewa nguvu na serikali kupitia wizara ya afya ,hii itasaidia kwa kiwango kikubwa kutatua kero za afya zilizopo.
Kauli za serikali
Mwenyekiti wa Kijiji cha Dakawa, Hassan Mwanga anakiri jengo hilo kushindwa kutumika licha ya kukamilika kwa ujenzi wake toka mwaka 2014.
Anasema kuwa ameshatuma maombi kufunguliwa jengo hilo katika ofisi ya mkurugenzi wa wilaya na kuahidi kufunguliwa, ingawa hadi sasa hajaelezwa ni lini litafunguliwa ili kuanza kazi ya kuhudumia wananchi.
Mwanga anasema kuwa ujenzi wa zahanati umegharimu zaidi ya sh. milioni 32, halmashauri ikichangia kiasi cha sh. milioni 24 na wananchi wakichangia kiasi cha sh. milioni 8, pamoja na nguvukazi.
Anasema kutokana na ukosefu wa zahanati katika kipindi cha mwaka mmoja, wajawazito wawili walijifungulia njiani, jambo ambalo ni hatari kiafya.
Mtendaji wa Kijiji cha Dakawa, Hassan Kunambi anasema zahanati yake inashindwa kufunguliwa kutokana na ukosefu wa samani.
Anataja sababu nyingine kuwa ni kukosekana kwa nyumba ya mganga na wahudumu wa afya, licha ya mganga mkuu wa wilaya kuwaahidi kuwa atawapelekea wahudumu wa afya bila mafanikio.
Kunambi anaoimba serikali ya wilaya na mkoa kusadia wakazi hao wa Dakawa ili kuweza kupata huduma ya afya ndani ya kijiji chao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Sudi Mpili anasema wako mbioni kufungua zahanati hiyo mapema iwezekanavyo ili kuondoa kero hiyo.
Anasema kuwa halmashauri iko kwenye mpango wa kuazima waganga wasaidizi na manesi katika zahanati jirani ili waweze kufungua na kuanza rasmi kutoa huduma ya afya kwa wakazi wa kijiji hicho.