Imeelezwa kuwa muingiliano wa kisiasa katika kazi za kitaaluma kwenye ofisi za umma kunazuia wataalamu kufanya kazi kwa huru na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (2017), wataalamu katika sekta ya umma kwa sehemu kubwa wanafanya kazi kwa maelekezo ya wanasiasa kinyume na matakwa ya sheria za kazi.
“LHRC pia imeona kwamba muingiliano wa kisiasa katika kazi za kitaalamu unazuia wataalamu kufanya kazi kwa uhuru,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Wanasiasa ambao wana ushawishi serikalini hutumia fursa hiyo kupindisha au kulazimisha baadhi ya maamuzi ili waungwe mkono wakati wa uchaguzi. Hali hiyo imetajwa kuwakosesha huduma wananchi kutokana na rasilimali kuelekezwa kwenye matumizi mengine ambayo hayako kwenye mipango ya taasisi husika.
LHRC imebaini kuwa bado wafanya kazi wengi wana uelewa mdogo kuhusu haki wanapokuwepo mahali pa kazi na kuwarahisishia wanasiasa kuingilia taaluma zao.
“Kupitia msaada wa kisheria ambao LHRC hutoa, imebainika pia kwamba malalamiko/kesi za wafanyakazi wa kada mbalimbali kurubiniwa na kudhulumiwa sababu ya uelewa wao mdogo wa haki za mfanyakazi ni nyingi,” imefafanua ripoti hiyo.
Hata hivyo, hali hiyo inaweza kuwa imesababishwa na waajiriwa wengi wengi hasa kutoka elimu ya juu kukosa stadi muhimu kumudu majukumu muhimu wanayokabidhiwa kazini. Kutokana na changamoto za mfumo wa elimu nchini, wanasiasa wameendelea kutumia ujinga ili kujinufaisha kwa maslahi binafsi.
Kwa mujibu wa tatifi iliyofanywa na Baraza la Vyuo Vikuu la Afrika Mashariki (IUCEA) mwaka 2014, asilimia 61 ya vijana wanaomaliza elimu ya juu hawana stadi au sifa hizo, hivyo kuchangia pia ugumu wao katika kuajiriwa.
Mathalani, maslahi ya kisiasa yaliathiri zoezi la kuwaondoa wafanyakazi wenye vyeti feki lililofanyika mwaka 2017 ambapo baadhi ya wafanyakazi waliondolewa kazini kimakosa bila kufuata sheria za kazi.
“Haki ya kupata kipato kwa kufanya kazi pia iliminywa wakati wa zoezi la kuondoa wafanyakazi wenye vyeti feki/vya kughushi lililofanyika mwaka 2017. Katika zoezi hilo wafanyakazi takribani 9000 walifukuzwa kazi,
Hata hivyo, kati yao 1500 walikata rufaa dhidi ya kuondolewa kwao kazini, ambapo 450 waliripotiwa kurudishwa kazini baada ya kuonekana walifukuzwa au kuachishwa kazi kimakosa. LHRC inatoa wito kwa Serikali kufanya mazoezi kama haya kwa umakini zaidi ili kutoathiri haki za watu wambao hawana makosa,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Licha ya ongezeko la ajira katika sekta binafsi na umma, bado wafanyakazi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji utatuzi ili waweze kufaidika na Haki ya mazingira mazuri ya kufanyia kazi. Upungufu wa rasimali watu kwenye sekta muhimu kama afya na elimu hivyo kupelekea wafanyakazi waliopo kufanya kazi kupita kiasi na kupunguza ufanisi, na muda mwingi kutolipwa kwa kufanya kazi zaidi ya muda wa kazi; na utekelezaji na usimamizi usioridhisha wa sheria za kazi, hasa katika sekta isiyo rasmi.
Kwa upande mwingine LHRC imesema haki ya kupata kipato kwa kufanya kazi iliendelea kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana wengi waliomaliza elimu ya juu, licha ya kutolewa kwa ahadi mbalimbali za kisiasa kupunguza tatizo hilo nchini.
Serikali imeshauriwa kuzingatia na kulinda Haki ya kufanya kazi ambayo inajumuisha haki ya kupata kipato kwa kufanya kazi na haki ya mazingira mazuri ya kufanyia kazi kwa watumishi wote bila kujali hali zao na tofauati zao za kisiasa au kidini ili kuongeza uzalishaji katika sekta zote.