Mwanza: MV Victoria yanusurika kuteketea kwa Moto!

Sitta Tumma

KWA mara nyingine tena, Serikali imeingia hasara baada ya Meli yake ya Mv. Victoria inayofanya safari zake kutoka Jijini Mwanza kwenda Bukoba mkoani Kagera, kuwaka moto muda mfupi baada ya kuanza safari yake ya kwenda Bukoba.

Tukio la meli hiyo kubwa kuliko zote hapa nchini, limetokea leo majira ya saa 9:15 alasili, baada ya chombo hicho kulipuka moto kutoka ndani ya vyumba vya kuhifadhia mizigo, na watu kadhaa wamenusurika kufa kutokana na ajali hiyo mbaya.

Chanzo cha moto huo kimeelezwa kuwa, kimetokana na fundi mmoja wa meli hiyo (jina lake hajatajafahamika), alipokuwa akichomelea vyuma katika eneo la Gamla kwenye vyumba vya mizigo. Haijafahamika iwapo fundi huyo aliruhusiwa na uongozi wa meli hiyo kufanyakazi hizo.

Kaimu Mkuu wa Bandari ya Mwanza, ambaye pia ni Mkaguzi Mkuu wa Meli Kanda ya Ziwa, Richard Msechu alipotakiwa na FikraPevu kuzungumzia tukio hilo la Meli kuwaka moto, alisema kwa kifupi: "Mimi suala la meli hiyo kuungua moto  halinihusu kabisaaa, watafute watu wa Maline Service ndiyo wanaoweza kukueleza".

Hata hivyo, FikraPevu ilimtafuta na kumpata Kaimu Meneja wa kampuni ya Huduma za Meli (Maline Service), inayomiliki meli hiyo, Exavier Kapinga naye alikataa katakata kuelezea chanzo cha moto huo wala hasara iliyopatikana, badala yake alisema: "Wapo wakubwa zangu wanaopaswa kuzungumzia suala hilo kabla ya mimi".

Akizungumza na waandishi wa habari eneo la Bandari ya Mwanza, Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Kanda ya Ziwa, Mhandisi Japhet Loisimaye alisema wanafanya uchunguzi kubaini kama shughuli za uchomeleaji vyuma vilivyosababisha meli hiyo kulipuka moto, iwapo zilikuwa na baraka kwa uongozi wa meli hiyo.

Baadhi ya abiria wanaotarajia kusafiri leo usiku kwa kutumia meli hiyo ya Mv. Victoria, walisema kwamba wanahofia usalama wao punde meli itakapokuwa majini kuelekea mjini Bukoba mkoani Kagera, hivyo walishauri meli hiyo kusitisha safari zake hadi hapo uchunguzi wa kina utakapofanyika kisha kubaini tatizo na madhara yake.

Mwaka 1996 Serikali ilipata hasara kubwa baada ya Meli yake ya Mv. Bukoba kuzama maji maili chache wakati ilipokaribia kufika Jijini Mwanza ikitokea Bukoba, ambapo mamia ya Watanzania na raia wa kigeni walifariki dunia kutokana na ajali hiyo mbaya. Hadi sasa Meli hiyo ya Mv. Bukoba haijapatikana ambapo inadaiwa kuzama zaidi ndani ya tope  Ziwa Victoria.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *