Neema ya maji yashuka kijiji cha Amani wilayani Tunduru lakini ina maumivu yake

Jamii Africa

Hatimaye wakazi wa vijiji vinne vya kata ya Namasakata wilayani Tunduru wameondokana na tatizo la ukosefu wa maji ya uhakika baada ya Benki ya Dunia (WB) kukamilisha mradi mkubwa wa maji ya bomba kijijini hapo wenye thamani ya milioni 978.4.

Mradi huo utahudumia vijiji 4 vya kata hiyo ambavyo ni Chiungo, Amani, Mchengamoto na Meamtwaro ambavyo vimeungwanishwa kwa mtandao wa mabomba na vituo vya maji ambavyo vimejengwa katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo.

Licha ya neema hiyo ya maji, wakazi hao watalazimika kuchangia fedha kidogo kwa ajili ya utunzaji na uendelezaji wa mradi huo ambao unaonekana kama mkombozi ikizingatiwa kuwa walikuwa wanatembea umbali mrefu kutafuta maji kwenye vijiji vya jirani.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tunduru, Mbwana Mkwanda Sudi akizungumza na wakazi wa kata ya Namasakata ambako mradi huo umejengwa alisema Serikali imewekeza fedha nyingi na wananchi wanatakiwa kuulinda na kuendeleza ili udumu kwa muda mrefu.

“Hivyo niwatake madiwani wa Kata ya Namasakata na Misechela ambao wanapata huduma ya maji kuhamasisha wananchi juu ya umuhimu wa kutunza, kuchangia na kulinda mradi huu”, alisema Mkwanda.

Aliwataka wananchi wa vijiji hivyo kujiwekea utaratibu mzuri wa kuchangia huduma ya maji na kutunza mazingira ili kuhakikisha kila mwananchi anapata maji safi na salama wakati wote.

“Ni nyema vijiji vikajiwekea utaratibu wa kuchangia huduma ya maji ili mradi uwe endelevu lakini kuna makundi maalumu katika jamii ambayo sio lazima kuchangia mfano wazee na walemavu hawa inabidi kukadiriwa kiwango cha lita za maji wanazotumia kwa siku”, alisema Mkwanda.

Taarifa kutoka katika vikao vya kamati za maji vinavyoendelea kwenye vijiji zinaeleza kuwa makubaliano ni kuchangia fedha kila mwezi ambapo kaya zitatoa kiasi fulani cha fedha ambacho kitakusanywa na kuwasilishwa kwenye mamlaka husika.

Katika baadhi ya vijiji wamekubaliana kuwa kila kaya au familia itoe sh. 1000 (kwa mwaka ni 12,000) ambapo fedha hizo zitagharamia matengenezo ya miundombinu, ulinzi wa vituo vya maji na mtandao wa mabomba yaliyosambazwa katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Tunduru, Eberhard Halla alisema mradi huo ambao uko kwenye kijiji cha Amani umedhaminiwa na Benki ya dunia na mpaka kukamilika kwake umegharimu sh. Milioni 978.4

Alisema mradi huo umeunganishwa na vituo vya kutolea huduma ya maji 48 ambapo katika kijiji  cha Amani kuna vituo 17, Chiungo (10), Meamtwaro (8), Mchengamoto (10) na kitongoji cha Mkarachani (3). Mradi huo unatumia chanzo kimoja cha maji cha mto Nambango kilichopo kijiji cha Amani.

Benki ya Dunia imekuwa mfadhili muhimu wa Tanzania kwenye huduma za kijamii ambapo mradi huo wa maji ni sehemu ya ufadhili wa miradi ya maji kwenye vijiji 10 vya Wilaya ya Tunduru.

 

Tatizo la maji litaisha lini?

Licha ya Tunduru kuwa karibu na Ziwa Nyasa ambalo hutumika kwa matumizi mbalimbali ya kibinadamu, lakini Wilaya hiyo haifaidiki na chanzo hicho ambacho hakijawekewa mikakati endelevu ya kuzalisha maji ya bomba ambayo yangemaliza kabisa tatizo la maji katika Mkoa wa Ruvuma.

Hata hivyo, Wilaya ya Tunduru ina kazi kubwa ya kuinua hali ya upatikanaji wa maji ikizingatiwa kuwa visima ndiyo tegemeo kubwa la wakazi huku maji ya bomba yakipatikana katika maeneo machache.

Wilaya ya Tunduru ina wakazi wapatao 298,279 lakini maji ya bomba yanayozalishwa na Mamlaka ya Maji Mjini Tunduru (TUWASA) yanawafikia wakazi 175,250 tu ambao ni asilimia 58.8. Asilimia iliyobaki hawapati maji ya uhakika kutokana na uwekezaji mdogo usioendana na ongezeko la idadi ya watu.

Mahitaji halisi ya maji kwa mtu mmoja mmoja ni lita 60 kwa siku, ambayo hayapatikani yote na huwalazimu baadhi ya wakazi kutembea umbali mrefu kuyafuata maji katika maeneo yenye vyanzo vya maji.

Hata hivyo Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) yanalenga hadi kufikia 2030 kuongeza matumizi ya maji ya uhakika katika sekta zote na usambazaji wa maji safi ili kupunguza idadi ya watu ambao wanataabika kutokana na uhaba wa maji.

Hata hivyo, kufikia malengo hayo nchi wahisani ikiwemo Tanzania zimetakiwa kuongeza uwekezaji katika miradi ya maji na utunzaji wa vyanzo vya maji ili kuhakikisha watu wanapata maji safi, salama na ya uhakika.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *