SERIKALI imewaonya viongozi wa vyama vya siasa kuacha mara moja kuwapotosha Watanzania kuhusu suala zima la Katiba mpya, na kusema wanaozunguka nchi nzima na kupotosha Umma juu ya Katiba huenda akili zao hazipo sawasawa.
Imeelezwa kwamba, upotoshwaji unaofanywa na baadhi ya wanasiasa na viongizi wengine juu ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba mpya 2011, umelenga kuwavuruga wananchi, na kwamba Rais Jakaya Kikwete alichosaini si Katiba, bali ni Sheria ya kuweka utaratibu wa uundwaji wa Katiba mpya.
Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja wakati alipokuwa akihutubia maelfu ya watu kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika stendi ya Mabasi mjini Sengerema mkoani Mwanza.
Alisema, wapo baadhi ya wanasiasa na viongozi wengine wenye heshima wamekuwa wakipotosha ukweli kuhusu suala zima la Katiba mpya, na kwamba, kilichopitishwa na Wabunge Bungeni si muundo wa Katiba bali ni sheria itakayosimamia uundwaji wa Katiba hiyo mpya.
“Naomba leo niwaambie ukweli katika hili la Katiba mpya. Katiba mpya bado haijatungwa, wala maoni ya namna ya Watanzania jinsi wanavyotaka Katiba iwe hayajakusanywa.
“Nawashangaa wale wote wanaosema eti Katiba mpya ni mbovu. Itakuwaje mbovu wakati haijatungwa wala kupitishwa?. Tunataka waache kuwapotosha wananchi, maana Rais Kikwete amesaini sheria tu na si katiba mpya!”, alisema Waziri huyo wa Nishati na madini ambaye alihutubia mkutano wake kuanzia saa 10 jioni hadi saa 2:00 usiku.
Akikazia zaidi katika hilo, Waziri Ngeleja alisema, baada ya Bunge kupitisha sheria hiyo ya kuweka utaratibu wa muundo wa Katiba mpya, Rais anatakiwa kuunda Tume ya kukusanya maoni ya wananchi sambamba na Bunge la Katiba.
Kwa mujibu wa Waziri Ngeleja, Rais anatarajiwa kuunda Bunge la Katiba kwa kuwashirikisha Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wawakilishi wa Baraza la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na wajumbe wengine 166 kutoka asasi za kiraia, dini, vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu.
Taasisi za elimu ya juu, makundi maalumu ya kijamii, vyama vya wafanyakazi, jumuiya ya wakulima, wafugaji, vikundi vingine vya watu vyenye malengo yanayofanana, na alisema wanaozunguka nchi nzima kuwahadaa wananchi hao huenda wana tatizo la akili au hawaujui kabisa mchakato huo.
Aidha alisema, katika sheria hiyo mpya ya Katiba inawapa fursa Watanzania kupiga kura za maoni kukubali kama wanataka katiba ampya ama lah, na watakaokuwa na sifa za kupiga kura hizo za maoni ni wale wenye shahada za kupigia kura na waliopo kwenye daftari la wapiga kura Tanzania Bara na Visiwani.
Akihitimisha hotuba yake hiyo, Waziri Ngeleja alisema: “Wapo baadhi ya wananchi wanadanganywa eti kuna sheria ya kuwakamata na kuwafunga watakapohoji mchakato mzima wa Katiba mpya, hilo halina ukweli na hakuna sheria ya namna hiyo, ila pale mtu atakayeizuia Tume kufanyakazi yake huyo ndiye atachukuliwa hatua za kisheria”.
Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Sengerema