Njia 4 ambazo waliofanikiwa huzitumia kutojali kile wanachofikiria watu wengine

Jamii Africa

Kwa namna moja au nyingine, wote kwa namna fulani tumewahi kujutia kujali sana kile ambacho watu wengine wanakifikiria au watakifikiria. Tunasita kuwa wabunifu, wavumbuzi au kusema kwa uwazi kile tunachokiwaza kwa kuogopa kuonekana kwamba tuna mawazo mabaya au mipango yetu ni mibovu.

Piia tunaweza kujifanyia hivi sisi wenyewe, kwa kukataa changamoto fulani au kuuza mawazo yetu kwa kuhofia kwamba hayatafanikiwa. Mwandishi maarufu Seth Godin anasema siyo “hofu ya kushindwa” inayoturudisha nyuma na kufanya tusiendelee bali “hofu ya kukosolewa”.

 

Je, unawezaje kupuuzia wanachofikiria watu wengine?
Jambo la kwanza unalotakiwa kufahamu ni kwamba, kama watu wengi wamewahi kukumbwa na hali hii na wakafanikiwa kufanya mambo makubwa, waliikabili hofu yao ya kushindwa na kukosolewa na wakafanikiwa. Watu wanaothubutu kwenye mafanikio hufanikiwa kuzuia hali ya kukosolewa kuwakwamisha.

Kama unataka kubadilika kutoka kuwa mtu ambaye ni muoga kuongea mbele za watu na kuwa mzungumzaji mwenye ujasiri, basi jifunze kupitia mbinu hizi zilizotumiwa na watu 4 waliofanikiwa.

 

1. Jiulize wewe mwenyewe: “Nini kitatokea nisipofanya chochote?”
Marie Forleo, mtangazaji wa kituo cha runinga cha Marie anasema, inapotokea nafasi ya kufanya kitu kipya au nje ya uzoefu wako, kitu kinachoweza kukusaidia ni kufikiria hali mbaya kabisa.

Kwa maneno mengine ni kwamba, kabla hujajizuia kufanya jambo kwasababu tu kuna uwezekano wa kushindwa, jiulize kwanza “ Ni jambo gani baya linaloweza kutokea ukifanya…” Je, kuna uwezekano wa wewe kuanguka na kuumia usoni kwa kufanya kitu fulani kipya na chenye changamoto? Na je, ni vipi kama utakaa kimya?

Orodhesha vitu vyote vibaya ambavyo unadhani vitatokea endapo utaikubali fursa hiyo. Andika makosoleo yote unayoweza kuyapata kutokana na uamuzi huo. Na kwa kuongezea hapo orodhesha pia mambo yote ambayo yatatokea kama utaamua kukaa kimya na kuficha mawazo yako na mipango yako kwa ulimwengu. Oanisha orodha yako na fanya maamuzi ya kipi ukifuate baada ya hapo.

 

2. Kumbuka kwamba kazi yako haikuelezei wewe ni nani
Rohan Gunatillake anasema watu wengi tuna desturi mbaya ya kuruhusu kazi zetu zituelezee, hivyo kushindwa kwenye kazi fulani hutufanya tujisikie vibaya kwenye nafsi zetu.

Katika mazungumzo yake Rohan anaelezea tiba ya “kutenganisha nafsi na kazi” ambapo anatumia kauli fulani fupi ambazo mtu huzichagua na kuzitamka kwa sauti, kujihusisha nazo na baadaye utaona jinsi zinavyokufanya ujisikie kuhusu hili.

Kauli hizo ni kama vile: “ Mimi sio utambulisho wa kwenye ukurasa wangu wa mtandaoni”, “Mimi sio kampuni yangu”, “Mimi sio wasifu wangu” na “Mimi sio kazi yangu”. Husisha kauli hizi na nafsi yako na uone zitakupa hisia gani.

Anasema kwa kufanya hivi itakusaidia kutenganisha nafsi yako na kazi yako, na hatimaye hukuondolea maumivu unayoyapata pale unaposhindwa kazini. Kama “wewe sio kazi yako” basi hata pale unapokosea ukiwa kazini (kitu ambacho wengi wetu hututokea) hutabeba maumivu hayo ndani yako na kujisikia vibaya wakati wote.

Hivyo ni sawa kabisa kuikubali fursa hiyo mpya na ngumu kwasababu hata isipofanikiwa haimaanishi kwamba wewe binafsi umeshindwa. Ukikumbuka kwamba wewe ni zaidi ya kazi yako itakusaidia kuwa mbunifu.

 

3. Usiruhusu watu wakushushe au kukukwamisha
Kuzuia hali ya kujikosoa mwenyewe ni hatua ya kwanza kwasababu unatakiwa kujiandaa kwa kuwa watu wengine watakukosoa pia.

Mwandishi maarufu Brene Brown anasema, “Kutojali kile watu wanafikiria ni namna ya kipekee katika kupambana”. Katika mazungumzo yake ya 99U, aliwashirikisha watu msemo kutoka kwa aliyewahi kuwa rais wa Marekani, Theodore Roosevelt ambao ulibadilisha mtazamo wake kuhusu kukosolewa.

Haijalishi anayekosoa ni nani; siyo yule anayeelezea jinsi mtu jasiri anavyopambana au pale mtenda mema angefanya vizuri zaidi. Sifa zinatakiwa ziende kwa mtu ambaye yuko uringoni, ambaye uso wake hufunikwa kwa vumbi, jasho na damu… yule ambaye katika wakati mzuri anajua mwishoni ni furaha ya mafanikio makubwa, na katika magumu hata akishindwa, anashindwa akiwa amejaribu kwa kiwango kikubwa.

Msemo huu ulibadilisha kabisa mtazamo wake wa zamani. Brown aliamua kujali kukosolewa kulikotoka kwa mtu ambaye naye alikuwa kwenye uringo kama wa kwake, lakini mtu aliyemkosoa kwa kuamua tu kukosoa huyo hakujali alichokisema. Hafanyi hivi ili kumpuuza mtu huyo kabisa bali hujibu kwa kusema, “Nimekuona, nimekusikia, lakini bado nitafanya jambo hili.

Hutakiwi kuwapuuza watu wasiokubaliana nawe kama vile hawapo; unachotakiwa kufanya ni kuamua kwamba utaendelea kufanya kile ulichokipanga, kwa kuwa umeona kwamba kufanya kuna manufaa zaidi kuliko kutofanya, na hata kama hutafanikiwa haitamaanisha kwamba wewe ni wa kushindwa.

 

4. Kubali kukosolewa
Seth Godin, ambaye ameelezwa hapo mwanzo, ni mjasiriamali na mwandishi mashuhuri ambaye ameshauza vitabu 18 ambavyo vimetafririwa kwa lugha 35. Anasema kwamba binadamu ana “machaguo mawili tu” kwenye maisha: Kukosolewa au “kupuuzwa”.

Wewe ndiye unayechagua. Ila kama unajizuia kufanya kitu fulani kwa kuogopa kukosolewa basi jiulize maswali haya:
Je, nikikosolewa kwa hiki ninachotaka kufanya, nitapata matatizo yoyote makubwa? Je, nitapoteza kazi yangu au nitapoteza marafiki wa muhimu? Kama madhara pekee unayoweza kuyapata kwenye kukosolewa ni kujisikia vibaya kuhusu kukosolewa, basi oanisha hisia hiyo mbaya na faida unakayoipata kwa kufanya kitu chenye thamani.

Kuwa tofauti ni jambo zuri na lenye faida kubwa sana kwa taaluma yako. Kujisikia vibaya hupotea baada ya muda. Baada ya kuoanisha pande hizo mbili na umeshachagua njia ipi ya kuifuata, jibu swali hili.

Nawezaje kutengeneza kitu ambacho wakosoaji watakikosoa?
Utakapoacha kuwachukulia wanaokukosoa kama ishara ya kwamba umefanya kitu kibaya, na kuwaona kama ishara ya kwamba umefanya kitu kinachoonekana kwenye jamii, hofu hiyo hupotea ghafla. Wakati mwingine hii huwa kama alama ya heshima kwamba ulifanya kitu muhimu sana ambacho watu wengine waliona kuna haja ya wao kutoa maoni yao.

Ni jambo la kawaida kutojiamini au kuruhusu maneno ya watu yaongoze ufahamu wako. Lakini ukizitumia mbinu hizi kubadilisha ufahamu wako, utaweza kuikabili hofu ya kushindwa na kufanikiwa katika kile ulichokusudiwa ukifanye.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *