Obama na siasa za Mashariki ya Kati: Ataka Israeli irejee mipaka ya 1967

Jamii Africa

Rais wa Marekani Bw. Barack Obama siku ya Alhamisi ametoa hotuba ya kihistoria kuhusiana na mwelekeo wa mchakato wa amani huko Mashariki ya Kati ambapo kikuu alichokianishia ni mwelekeo mpya wa sera za Marekani kuhusiana na mgogoro wa Mashariki ya Kati ya Waisraeli na Wapalestina.

Hata hivyo kabla ya kuainisha maono ya serikali yake kuhusu mgogoro huyo Bw. Obama alitumia muda mrefu kuelezea mtazamo wa taifa lake kufuatia Mwamko wa Waarabu wa mapema mwaka huu ambapo tawala za muda mrefu katika Afrika ya Kaskazini na maeneo mengine ya Mashariki ya Kati zimetikiswa na nyingine kung’oka kufuatia wimbi la maandamano ya raia wakidai haki zao mbalimbali na utu wao.

Mwanzoni kabisa mwa hotuba yake aliyoitoa kwenye Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani chombo ambacho kinahusiana na kusimamia na kutekeleza sera ya Mambo ya Nchi za Nje ya taifa hili lenye nguvu zaidi duniani Bw. Obama alielezea mafanikio ya serikali yake hasa baada ya kuweza kuanza kuwaondoa wapiganaji wapatao 100,000 kutoka Iraq ikiwa ni hatua za mwanzo za kuwarudisha wanajeshi wa Jeshi la Marekani nyumbani pamoja na ahadi ya kuanza kuwaondoa wanajeshi wake huko Afghanistani katikati ya mwaka huu.

Akijivunia mafanikio ya kumuua ghaidi nambari moja duniani Osama bin Laden Rais Obama alisema kuwa “Osama hakuwa shahidi- alikuwa ni muuaji wa halaiki aliyeeneza ujumbe wa chuki – iliyosisitiza kuwa Waislamu wachukue silaha dhidi ya nchi za Magharibi na kuwa matumizi ya nguvu dhidi ya Wanaume, Wanawake na Watoto ndio njia pekee ya kuleta mabadiliko”. Aliendelea kumtaja Osama kuwa mtu “aliyekataa Demokrasia na haki za kila Muislamu mmoja mmoja akichagua msimamo mkali wa matumizi ya nguvu; ajenda yake ikitilia mkazo kile alichoweza kukibomoa – na siyo alichoweza kukijenga”.

Rais Obama alielezea kuwa sera hizo za ghaidi Osama zilishaanza kupoteza mwelekeo na kukataliwa na Waislamu wengi ambao hawakukubaliana nazo. Na ya kuwa Mwamko wa Waarabu wa mapema mwaka huu ulikuwa ni ishara ya wananchi wa mataifa ya Kiislamu kukataa sera za Osama. “Hadi tunampata Bin Laden, ajenda yake ilikuwa imeonekana na watu wengi kuwa haina mpango, na watu wa Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini walikuwa wameamua kuchukua hatima yao mikononi mwao” alisema Bw. Obama akishangiliwa.

Akisimulia mwanzo wa Mwamko huo wa Waarabu ambao ulianzia huko Tunisia Afrika ya Kaskazini Bw. Obama alisema kuwa  tarehe 17 Disemba mwaka jana, mmachinga aitwaye Mohammed Bouazizi alikasirishwa na kuumizwa moyoni baada ya polisi kumnyang’anya mkokoteni wake wa biashara. Kinyume na matarajio ya watu wengi ambao tukio kama hilo lingeweza kuonekana ni kawaida kwani hutokea mara nyingi sehemu zenye zatawala za kibabe duniani. “Safari hii ilikuwa tofauti, kitu tofauti kikatokea. Baada ya kutosikilizwa na watendaji wa eneo lake, huyu kijana ambaye hajawahi kuonekana akijishughulisha na siasa, alifunga safari hadi ofisi ya chama tawala, akajimwagia mafuta na kujitia moto” alielezea Rais Obama.

Matokeo yake kwa mujibu wa Rais Obama akielezea mwamko wa kwanza Waarabu “mamia wakaingia mitaani kuandamana, baadaye maelfu. Pamoja na kupigwa na virungu na risasi hawakutaka kurudi majumbani kwao, siku baada ya siku, wiki baada ya wiki hadi dikteta aliyekaa kwa karibu miaka ishirini madarakani alipoamua kuachia madaraka”.

Kutoka hapo Rais Obama alielezea yale yaliyojiri katika nchi mbalimbali za Kiarabu kuanzia Misri, Yemeni, Libya, Syria na nchi nyingine za Waarabu ambapo maelfu ya raia walianza  kufuata mfano wa Tunisia na kutoa changamoto kwa tawala ambazo zilionekana zimejisimika madarakani bila kutikiswa. Rais Obama alitangaza kuwa taifa lake litaunga mkono juhudi za raia wa nchi mbalimbali ambao wameamua kuchagua demokrasia, uhuru na haki zao.

“Marekani haikuwatuma watu kwenda mitaani kuandamana, ni wao wenyewe walianzisha mwamko huu na ni wao watakaoamua matokeo yake” alisema Rais Obama. Alielezea kuwa serikali yake iko tayari kusaidia nchi zile ambazo zimechagua njia ya demokrasia na mabadiliko ya kisiasa. Alienda kiundani akitaja nchi mbalimbali kwa majina katika mtazamo mpya wa maono yake ya Mashariki ya Kati ambayo ina mabadiliko ya kisiasa. “Hivyo, katika miezi ijayo, Marekani itatumia uwezo wake wote wa ushawishi kuunga mkono mabadiliko katika eneo hilo”aliahidi Rais Obama.

Katika hotuba hiyo Serikali ya Marekani imeamua kuchukua msimamo mkali ambao haikuuchukua moja kwa moja dhidi ya Rais Bashir Assad wa Syria ambaye nchi yake imekuwa katika jaribio la kuzuia mabadiliko ya kisiasa ambayo mamia ya watu tayari wameuawa mikononi mwa vyombo vya dola ambavyo vimekuwa vikijitahidi kuzima maandamano ya kisiasa ya wananchi wanaodai mabadiliko. Rais Obama alisema kuwa “Rais Assad ana uchaguzi; kuongoza kuelekea mpito au kukaa pembeni”. Hii ni kwa mara ya kwanza kwa serikali ya Marekani kuweka wazo kuwa Assad anaweza asiwe sehemu ya mabadiliko yanayokuja nchini Syria.

Hata hivyo, mabadiliko makubwa ya sera za Marekani yalikuja pale alipoanza kuzungumzia mgogoro kati ya Waisraeli na Wapalestina na kuainisha sera mpya ya Taifa hilo kubwa katika kile ambacho wafuatiliaji wa siasa za nje za Marekani wanakitaja kama “mabadiliko makubwa ya sera” kuhusiana na mgogoro huo ambao umedumu katika Mashariki ya kati kwa zaidi ya miaka hamsini sasa.

Rais Obama alikiri kuwa urafiki kati ya Marekani na Israeli ni wa kihistoria na ambao hauwezi kutikisika. Hata hivyo alisema kuwa “ni sababu ya urafiki huu ni lazima tuseme ukweli; hali iliyopo haiwezi kuendelea”. Obama alisema kuwa wakati umefika kwa Waisraeli na wenyewe kuchukua hatua za kuthubutu ili kufikia amani ya kudumu.

Akionesha kuinyoshea kidole Israeli Obama alisema kuwa “jumuiya ya Kimataifa imechoshwa na mchakato usiofikia kikomo  na usiozaa matunda. Njozi ya taifa la Kiyahudi na la Kidemokrasi haiwezi kutimilika wakati kukalia kimabavu kunaendelea” alisema Bw. Obama.

Akiendelea kuonesha nia yake ya kuziambia pande hizo mbili ukweli unaouma Rais Obama alisema kwa Wapalestina kuwa bila kutambua haki ya Israeli kuwepo njozi yao na wao kuwa na taifa lao wenyewe katika amani haitoweza kutimilika. “Viongozi wa Palestina hawatoweza kufikia amani kama Hamas inaendelea na njia ya ughaidi na kuikataa Israeli”.

Akielezea mwelekeo mpya wa sera ya Marekani kuhusu mgogoro huo Rais Obama alisema “Ingawa mambo muhimu ya mgogoro lazima yazungumwe kwa makubaliano, msingi wa makubaliano hayo uko wazi; taifa linalojitegemea la Palestina na taifa lililosalama la Waisraeli. Marekani  inaamini kwamba mazungumzo ya makubaliano yalete mataifa mawili, ambapo Palestina itakuwa na mipaka yake ya kudumu na Israeli, Misri na Jordani na mipaka ya kudumu kati ya Israeli na Palestina.”

Rais Obama alitoa msimamo ambao umewashtua wachunguzi wa siasa za nje na ambao tayari umekataliwa na Waziri Mkuu wa Israeli Bw. Benjamin Netanyahu kuwa “mipaka kati ya Israeli na Palestina iwe ile iliyokuwepo mwaka 1967 na kubadilishana mambo watakayokubaliana ili mipaka salama na ya kudumu iwepo kati ya mataifa hayo mawili”

Kauli hiyo ya Obama imepokewa na wapinzani wake wa kisiasa na watetezi wa Israeli kama ubadilishaji mkubwa wa sera ya Marekani huku baadhi ya wachunguzi wa kisiasa wakidai kuwa kutaka Israeli irudie mipaka ya 1967 ni kutaka Israeli ijiangamize. Netanyahu akitoa kauli yake mara baada ya hotuba ya Obama amesema kuwa kuelekea amani ya kweli haiwezekani kuundwa kwa taifa la Palestina kuwe sababu ya kuangamizwa kwa taifa la Israeli hivyo alikuwa anatarajia Rais Obama atasimamia makubaliano ya Marekani na Israeli ya mwaka 2004 ambayo hayakutaka Israeli irejee mipaka ya 1967. Hofu ya Netanyahu na serikali ni kuwa mipaka ya 1967 “hailindiki” akimaanisha kwamba ni rahisi kushambuliwa.

Mwitikio wa Wapalestina hadi hivi sasa unaonekana wa matumaini kwani habari zilizopatikana jana jioni zionaesha kuwa Rais wa Palestina Abu Mazin ameitisha kikao cha dharura cha Baraza lake la Mawaziri na vile vile ameitisha mazungumzo na baadhi ya viongozi wa nchi za Kiarabu kujadili hutuba hiyo. Hamas kwa upande wake wameibeza hotuba hiyo wakidai kuwa Obama anawalaghai kwani sera za Marekani bado zinaipendelea Israeli.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *