Padri Raymond Mayanga:  Tuidhihirishie dunia kama kweli tumekomaa na tujione kama watoto wa Mungu, taifa moja

Jamii Africa

Kufuatia msiba wa mwanafunzi wa Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) aliyeuawa kwa kupigwa risasi akiwa kwenye daladala wakati wa maandamano ya wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) siku ya ijumaa ya Februari 15 mwaka huu, maoni mbalimbali yametolewa kwa taifa kuimarisha mshikamano na raia kuhakikishiwa usalama wao.

FikraPevu imeipata hotuba ya Padri Raymond Mayanga wa kanisa Katoliki Parokia ya Yohane Mbatizaji Luhanga aliyoitoa siku ya jana wakati wa kuaga mwili wa marehemu katika viwanja vya chuo cha NIT mabibo jijini Dar es Salaam. Sehemu ya hotuba hiyo inasomeka kama ifuatavyo:

“Katika hili kama nilivyosema  limetokea kwa namna hiyo ambavyo limetokea. Tumekusanyika kwa wingi huu kwasababu imetokea kwa namna isiyo ya kawaida. Huu umekuwa msiba tofauti kidogo. Tunaona kabisa kwamba ni msiba kwa namna moja au nyingine ni msiba wa kitaifa”

Kwahiyo natumai ndugu zangu hatujali rangi, hatujali jinsia, hatujali urefu au ufupi , hatujali umri. Tumekusanyika hapa kama taifa kupeana pole. Tumuombe Mungu basi kwasababu tumekusanyika kwa wingi huu na kwa namna hii, Mungu ana ujumbe kwa taifa lake

Ni upendo wa Mungu kila wakati kututakia mema. Mungu hata wakati mmoja hawezi akawatakia watoto wake katika namna yoyote ile Mungu hawezi akatutakia mabaya. Mungu ametupenda tukutane mchana huu tukimwomba atuonyeshe njia kwasababu yeye ndiye kweli na uzima.

Atuonyeshe njia ya jinsi ya kuwa taifa, ya jinsi ya kuwa watoto wake, kuishi maisha yetu tumehesabiwa kuwa hapa duniani na mwisho tuweze kuyafurahia huko mbinguni. Mimi nizungumzie katika imani kwamba Mungu ana ujumbe kwetu sisi na vilevile watoto wake bila kujali tofauti tusikilize ujumbe wa Mungu, tusikilize kitu cha namna hii kisitupite

Kama tulivyosikia basi hili tukio hatujui hawa watu wa habari wanatuambia kwamba amepigwa risasi (Marehemu Akwilina) akafa. Basi mimi siwezi nikazungumzia ni vipi na ndio maana kila mmoja anataka kusikia sasa imekuaje. Ni kweli kama ndio hivyo tumuombe Mungu tufanyeje ili tusianguke tena kwenye hili kwa namna hiyo siku nyingine.

Hilo ni la msingi kwasababu limeishatokea. Leo ni Akwilina tumuombe Mungu lisitokee kwa mwingine, liweze kweli kufanyiwa kazi ili lisitokee tena.

Kwa utaratibu wetu wa kawaida hatutegemei mjadala huu kufa, tunategemea kuwafariji ndugu na jamaa pamoja kwamba tunasikitika sana kwa changamoto tunazokumbana nazo, kwa Mungu kuna uzima, kweli, kwa Mungu kuna upendo, kwa Mungu kuna uvumilivu. Tumuombe Mungu atusaidie tupendane.

Huyu aliyekufa amenyakuliwa kutoka kwa watu, tujifunze basi kama sisi tumekuwa waovu tubadilike! Tubadilike.

Tukiendelea kutafakari hili jambo limetokea kwasababu sio bahati mbaya lakini risasi haiwezi kwenda yenyewe yule ana akili timamu haiwezi ikapigwa na ambaye hana akili timamu. Sasa nini kimetokea huyu mtu emepigwa risasi tuwe na hekima, tujenge amani, tujenge utulivu, tujenge usikivu, kusikilizana bila ya kuwa na matatizo.

Tumesheherekea miaka yetu 50 ya uhuru sitegemei matukio ya namna hii, hivi matukio haya ni ya mtu aliyefikisha miaka 50?. Tusheherekee au tuidhihirishie dunia kama kweli tumekomaa na tujione kama watoto wa Mungu, taifa moja.

Kila mtu kwa imani yake amwombe Mungu kutujalia kuwatumikia watu. Mtu mwenye kumuogopa Mungu, mtu anayejua maisha ni zawadi kutoka kwa Mungu, hakuna anayepaswa kumuua mtu, tumwogope Mungu .

Tumuombe Mungu atujalie kuwa wapole, tupunguze kiburi, tuwe wapole. Basi nisiendelee sana la mwisho ambalo napenda kuligusia ambalo ni la maana kabisa kwa taifa na watoto wa Mungu wote na sisi tuliopo hapa kwa imani zetu tofauti, kwa itikadi zetu tofauti, kwa jinsi na umri wetu tofauti, kwa mazingira tufauti tuwe wapatanishi.

Naomba tusikilize kwa makini heri wapatinishi, tukubali kama nilivyosema tumefika miaka hamsini ya uhuru tumekuwa watu wazima, je tunajikubali kama wana wa Mungu? Hii haina shortcut (mkato) sisi wote ni wana Mungu. Uhai wa mwanadamu unatuonyesha miaka hamsini ya ukomavu wa uhuru wetu?

Tumuombe sana Mwenyezi Mungu atusaidie kuwa wapatanishi, hii ni hekima yetu wote. Na kwa namna hiyo basi nimalizie kwa kusema mimi sio hakimu ila nazungumza hayo kama watoto wengine wa Mungu niwaombe wote tufanye kazi ya upatanishi.

Kwa wale wenye hiyo nafasi kwa hili lililotokea kwa mwenetu Akwilina tunaomba wale wahusika wenye madaraka ya kuweza kusaidia huyu aliyefanya kitendo hiki baada ya kujulikana aliombe taifa msamaha. Akwilina hatarudi amekwenda lakini aliyefanya hivi iwe ni kwa nia njema, kwa nia mbaya  lakini tunaomba basi atajulikana huyo mtu hata kwa kutumia TV  ama kwa kupitia namna inayowezekana haijarishi kama sivyo kila mmoja kwa imani yake awe mnyenyekevu.

Na serikali tuko hapa ni ndugu mmoja tuna imani kwamba itatupatanisha pamoja”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *