Pembe za ndovu za sh. milioni 192 zakamatwa Namtumbo

Albano Midelo

KAMPUNI ya Game Frontiers Tanzania(GFT) inayojishughulisha na uwindaji wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, kwa kushirikiana na kikosi cha askari wanyamapori katika pori la akiba la Selous, wamefanikiwa kukamata pembe za ndovu zenye thamani ya shilingi milioni 192.

Kaimu mkuu wa pori la akiba la Selous kanda ya kusini Magharibi Likuyuseka, Bernald Lijaji alisema pembe hizo zilikamatwa mwezi  Februari 17 mwaka huu majira ya asubuhi, huko katika maeneo ya wazi ya jumuiya ya Mbarang'andu ambayo yamekaribiana na pori la akiba la Selous wilayani humo.

Kulingana na kaimu mkuu huyo wa pori la Selous pembe zilizokamatwa zilikuwa 15 , risasi tisa na bunduki mbili kati ya hizo moja ni aina ya Gobole na nyingine Raifo na kwamba pembe hizo na bunduki zilizokamatwa hivi sasa vinashikiliwa katika ofisi ya pori la akiba la Selous iliyopo wilayani Namtumbo.

“Majangili ambao walikutwa wakiwa na nyara hizo za serikali mara baada ya kukurupushwa na askari wa wanyamapori walitoroka na kutokomea mahali ambako hadi sasa haijafahamika ingawa bado wanaendelea kusakwa ili wakikamatwa waweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria’’,alisisitiza.

Alibainisha zaidi  kuwa pembe hizo 15 zilizokamatwa ni sawa na Tembo wa nane waliouawa, na kwamba vitendo vya ujangili katika pori la akiba la Selous vimekuwa vikiwatesa kutokana na watu wasiokuwa waaminifu kuingia ndani ya pori na kuua wanyama bila kufuata taratibu na sheria za nchi.

Hata hivyo alisema  kuwa jitihada za kukabiliana na  majangili hao zinatokana na ushirikiano uliopo kati ya kampuni ya Game Frontiers(GFT), askari uhifadhi wa vijiji(VGS) na kikosi cha askari wanyama pori (Game reserve) cha pori la akiba la Selous.

Kampuni ya GFT kwa muda mrefu sasa imekuwa inatoa mafuta na gari ya doria, chakula, mawasiliano na kuwalipa posho askari ambao hushughulika katika kazi ya kupambana na ujaingili katika pori la akiba la Selous.

Kampuni ya uwindaji ya (GFT) inayofanya shughuli zake kwenye pori la Selous katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma imetoa misaada mbalimbali yenye thamani ya zaidi shillingi milioni 200 kwa ajili ya kuendeleza shughuli za maendeleo katika vijiji vinavyozunguka pori hilo katika kipindi cha mwaka 2012.

Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Sheni Abdalah amesema kampuni hiyo imetoa vifaa mbalimbali kwa jamii ya vijiji saba vinavyozunguka pori hilo ambavyo amevitaja kuwa ni Likuyu seka,Mandela,Mchomolo,Kilimasera,Mtonya na Songambele ambavyo ni  umoja wa jumuiya ya Mbarang’andu inayojumuisha vijiji hivyo.

Sheni anasema katika kipindi chote cha uwepo wake kwenye uwekezeji katika pori hilo ameweza kutoa misaada mbalimbali ikiwemo trekta moja kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kilimo, gari dogo moja kwa lengo la kuimarisha doria dhidi ya kupambana na ujangili unaofanyika katika pori la akiba la Selous.

Katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali kufuatia kukabiliana na wimbi kubwa la ujangili unaofanywa na baadhi ya watu  kwenye pori la akiba la Selous, kampuni ya uwindaji ya [GFT] imetoa msaada wa gari dogo lenye thamani ya zaidi ya shilingi milion10 kwa uongozi wa jumuiya ya Mbarang'andu inayo jumisha vijiji saba vinavyozunguka eneo hilo .

Pori la akiba la Selous linakabiliwa na ujangili wa nyara mbalimbali za serikali,uwindaji haramu kwa kutumia silaha haramu za aina mbalimbali na za sumu,uvuvi haramu na uvunaji haramu wa miti ya mbao ni baadhi ya matatizo.

Katika hatua nyingine wananchi wa jumuiya ya mbarang'andu walimwomba mwekezaji huyo kuwasaidia silaha za kisasa kwa kwa lengo la  kuwathibiti majangili kirahisi kwa kuwa majangili hao wamebainika  kutumia silaha kali katika vitendo vyao vya ujangili na kusababisha kuuwa wanyama ovyo.

Vitendo vya ujangili kwa wanyamapori vimekithiri sehemu mbalimbali nchini hali ambayo pia ilimlazimu hivi karibuni Naibu waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu,alieleza  Bungeni mjini Dodoma kuwa hali ya ujangili katika hifadhi za wanyama pori hapa nchini imekidhili  jambo ambalo linasababisha kupotea kwa wanyamapori wengi ambao wangeweza kulipatia Taifa fedha za kigeni akaagiza hatua za haraka zichukuliwe ili kukabiliana na hali hiyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *