Rwanda imewaonya raia wake wanaoingia kinyume cha sheria katika Mbuga za Wanyama mkoani Kagera kwa madai kuwa wanahatarisha ujirani mwema baina ya nchi hiyo na Tanzania.
Hatua hiyo imekuja siku chache, baada ya wanaume wanne kuvuka mpaka na kuingia upande wa Tanzania kwa shughuli za kuchanja kuni. Watanzania walimkamata mmoja wao ambaye alitambulika kwa jina la Shumbushu na kumpiga vibaya na kumjeruhi. Wengine walifanikiwa kutoroka na kurudi Rwanda.
Gavana wa jimbo la Mashariki mwa Rwanda, Fredy Mfulunje akizungumza na wananchi wanaoishi mpakani mwa Tanzania amesema vitendo vya kuingia kwenye ardhi ya nchi nyingine bila kufuata taratibu za kisheria hazikubaliki kwasababu vinaweza kuhatarisha amani ya nchi hizo mbili.
“Kuna makosa yanayofanywa na wananchi wetu wanaovuka na kuingia kwenye ardhi ya nchi nyingine kinyume cha sheria, ndiyo maana tumekuja hapa kuwaeleza kuwa vitendo hivi havikubaliki hata kidogo. Sisi tunawaasa wananchi kuachana na vitendo hivi ambavyo havikubaliki kabisa,” amesema Mfulunje.
Raia hao wa Rwanda wamekuwa wakivuka mpaka na kuingia kwenye Hifadhi za Wanyama zilizopo mkoani Kagera kwa ajili ya uwindaji wanyama na kuchanja kuni kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
“Hayo mambo ya kuvuka kinyume cha sheria na kwenda Tanzania ni hatari kwasababu watu wanapata matatizo na kimsingi hakuna vyovyote vya maana wanavyotafuta huko huenda tu ni kuokota kuni, vitu vya kawaida tu,” amenukuliwa raia mmoja wa Rwanda wakati wa ziara hiyo ya Gavana Mfulunje.
Ndege wanaopatikana katika Pori la Akiba Burigi mkoani Kagera.
Taarifa za jimbo la Mashariki mwa Rwanda zinaeleza kuwa mwaka jana Wanyarandwa watano walipoteza maisha na wengine kujeruliwa baada ya kuingia kwenye mbuga ya Kagera kuwinda wanyama.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Jimbo la Mashariki na jiji la Kigali, Meja Jenerali Mbaraka Muganga amesema wataendelea kudumisha ujirani mwema na Tanzania licha ya kuwepo kwa kasoro ndogo za wananchi kukiuka sheria za mipakani.
Mazungumzo hayo ya viongozi wa Rwanda yanatarajiwa kuendelea kwa wananchi wote wanaoishi kwenye wilaya zilizo karibu na mipaka ya Burundi na Uganda.
Ikumbukwe kuwa mapema mwaka huu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangala aliwataka Askari wa Hifadhi ya Wanyamapori kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria raia wa Rwanda wanaovuka mpaka na kuingia kwenye kisiwa cha Izinga kilichopo kwenye pori la akiba la Kimisi mkoani Kagera.
Dk. Kigwangalla alidai kuwa watanzania wakienda upande wa Rwanda kuvua samaki katika Ziwa Ihema wanauawa mara moja bila mjadala, wakati upande wa Tanzania raia wa nchi hiyo wapo wengi na wengine wamepewa uraia wa kuasili na huwa hawafanyiwi vitendo vya unyanyasaji wala mauaji.
Kisiwa cha Izinga ambacho kipo katika wilaya ya Karagwe mkoani Kagera kina ukubwa wa kilomita za mraba 12 na kinapakana na Rwanda. Pori la Akiba la Kimisi lilianzishwa mwaka 2003 kwa Tangazo la Serikali namba 116 na lina ukubwa wa 1,030 km. Pori hilo lina wanyama mbalimbali wakiwemo Tembo, Twiga, Simba na Chui.