Rushwa haijapungua Tanzania, usalama wa wanahabari, AZAKI shakani

Jamii Africa

Licha ya taasisi ya Twaweza kuonyesha rushwa imepungua kwa asilimia 80, taasisi nyingine imejitokeza na kudai kuwa juhudi za kutokomeza rushwa nchini hazionyeshi mweleko mzuri kwasababu ya kupungua kwa uwazi katika taasisi za umma na kukosekana kwa usalama wa vyombo vya habari na asasi za kiraia.

Taasisi ya Kimataifa ya Uwazi (Transparency International- IT) imetoa utafiti wake mpya jana juu ya hali ya rushwa duniani kwa mwaka 2017 ambapo imebaini kuwa nchi nyingi duniani hazijapambana kwa ukamilifu kutokomeza rushwa  katika sekta ya umma.

Taarifa ya utafiti huo inaeleeza sababu kubwa inayokwamisha mapambano hayo ni tabia ya baadhi ya serikali duniani kuwatisha na kuwatesa waandishi wa habari na Asasi za kiraia zinazoibua rushwa inayotokea kwenye sekta ya umma.

Tanzania imeshika nafasi ya 103 kati ya nchi 180 duniani zilizochunguzwa ambapo imepata alama 36 ya kiwango ambacho ni cha chini ukilinganisha na wastani wa dunia uliowekwa wa 43, na kuitaja nchi hiyo kuwa miongoni mwa nchi zenye vitendo vingi vya rushwa.

Katika upangaji wa madaraja, Transparency International  ilihusisha nchi 180 na kutumia kipimo 0 hadi 100, ambapo alama 0 ikiwakilisha nchi zenye kiwango kikubwa cha rushwa huku 100 ni nchi ambazo hazina au zina kiwango kidogo cha rushwa. Mwaka uliopita zaidi ya theluthi mbili ya nchi zilipata alama chini ya 50  kudhihirisha kuwa juhudi za mapambano ya rushwa zimepungua.

Uchambuzi wa matokeo ya utafiti huo unaonyesha kuwa nchi ambazo hazina ulinzi madhubuti kwa vyombo vya habari na Asasi za kiraia zimetajwa kuwa na viwango vikubwa cha rushwa.  Inaelezwa kuwa kila wiki mwandishi  mmoja anauawa katika nchi zinazohusishwa na viwango vikubwa vya rushwa. Uchambuzi huo unadai kuwa kwa miaka sita iliyopita, zaidi ya waandishi 9 kati ya 10 waliuawa kwenye nchi zilizopata alama 45 au chini ya hapo.

Nchi za New Zealand na Denmark zimeshika nafasi ya juu kwa kuwa na viwango vidogo vya rushwa kwa alama 89 na 88. Syria, Sudan Kusin na Somalia zimewekwa nafasi ya mwisho ambapo zimepata alama 14, 12 na 9. Afrika kwa ujumla haijafanya vyema katika kudhibiti rushwa huku nchi nyingi za bara hilo zikipata alama chini ya 32.

 

Tanzania imepona?

Utafiti huo kwa kiasi fulani unaakisi hali halisi iliyopo Tanzania katika nyanja za uwajibikaji na uwazi wa taasisi za umma kutokana na baadhi ya matukio ya hivi karibuni ikiwemo kuonywa, kufungiwa kwa vyombo vya habari na kupotea kwa baadhi ya waandishi katika mazingira yasiyoelezeka.

Matukio ya usiri yalishamiri sana mwaka uliopita ambapo Tanzania ilijitoa kwenya Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi (OGP) ambao ulikuwa unazitaka nchi kuondokana na kasumba  ya kuendesha mambo kwa usiri kati yake na wananchi.

Tanzania ilijiunga na mpango huo mwaka 2011 na hivyo kuwa nchi ya pili barani Afrika ikitanguliwa na Afrika Kusini ambapo ilitekeleza baadhi ya vipengele ikiwemo kutungwa kwa Sheria ya Upatikanaji wa Habari ya mwaka 2016, bajeti na taarifa za serikali kuwa wazi.

Sheria ya Upatikanaji wa habari inatumika lakini utekelezaji wake umekuwa ni mwiba kwa vyombo vya habari ikizingatiwa uhuru wa kutoa maoni na kupata habari bado uko kitanzini.

Wachambuzi mbalimbali wa masuala ya habari wanabainisha kwamba vyombo vya habari vinabanwa, vinatishwa na baadhi ya wanahabari wanatiwa nguvuni kutokana na kazi wanayofanya. 

Hali hiyo imetajwa kuwa ni mkakati wa watawala kuminya uhuru wa kujieleza na kupata taarifa ambapo magazeti ya Tanzania Daima, Raia Mwema, Mawio na MwanaHalisi yalifungiwa kwa tuhuma za uchochezi huku baadhi ya vituo vya runinga na redio vikionywa na kupigwa faini kwa kutangaza maudhui yanayodaiwa kuwa na mlengo tofauti na serikali.

Kulingana na Utafiti wa Twaweza (2016) unaeleza kuwa  “Uhuru wa kujieleza umekuwa ukikabiliwa na vitisho vikali ambapo polisi wamekamata watu 358 kwa mwaka 2015 na watu 911 2016 kwa kosa la kutumia lugha mbaya”.

Nazo Asasi za Kiraia haziko salama katika kutekeleza majukumu ya kuboresha maisha ya jamii. Kutokana na hali hiyo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu  (LHRC) na Baraza la Habari Tanzania (MCT) wanakusudia kwenda mahakamani kupata tafsiri ya neno ‘Uchochezi’ ambalo limekuwa likitumia kuviadhibu vyombo vya habari vinapotekeleza majukumu ya kuhabarisha umma

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC  wa wakati huo, Dkt. Hellen Kijo Bishimba alisema, “Tunaungana na wadau ambao wapo tayari kwenda Mahakamani kuomba tafsiri ya neno Uchochezi na pia tafsiri ya kifungu cha kanuni ya maudhui hususani kifungu cha 8 katika mazingira ya utawala wa serikali dhidi ya raia”.

Hata hivyo, Serikali inashauriwa kuhimiza uhuru wa kujieleza, vyombo vya habari na asasi za kiraia. Pia inapaswa kupunguza vikwazo kwa tasnia ya habari ili kuwawesha waandishi kufanya kazi zao bila hofu na vitisho ili kuruhusu uwajibikaji na uwazi katika jamii.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *