SAMAKI na dagaa kutoka Ziwa Nyasa wameadimika. Kuwala imekua kama anasa, kwani, licha kutopatikana kirahisi, wamekuwa bei aghali.
Inashangaza kwamba bei ya mazao hayo ya Ziwa Nyasa, “haishikiki” hata wanapouzwa mwaloni.
Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, ugumu huo wa kupatikana kwa samaki na dagaa, umeongezeka maradufu katika kipindi hiki cha masika, kiasi kwamba hata wakazi wa Mbamba Bay katika Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma, ambao wako kwenye mwambao wa ziwa hilo, wanakosa kitoweo ama kukipata kwa bei aghali.
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Isabela Chilumba, akiwa anaangalia dagaa waliokaushwa katika mwambao wa Ziwa Nyasa eneo la Mbamba Bay.
“Ulaji wa samaki wa ziwa hili umekuwa kama anasa kwa sasa, hususan kipindi hiki cha masika kutokana na maji mengi ya mito kutiririka ziwani na kuwasogeza samaki mbali,” anasema James Komba, mkazi wa Mbamba Bay.
Komba anaeleza kwamba, uhaba wa samaki umekuwa ukiongezeka siku hadi siku ingawa hawajui sababu kubwa ni nini.
Katika miji ya Mbinga na Songea, samaki wa Ziwa Nyasa wameonekana kuwa anasa zaidi kutokana na kuuzwa kwa bei ya juu.
FikraPevu imebaini kwamba, samaki mmoja aina ya Mbufu mwenye wastani wa nusu kilo, amekuwa akiuzwa kwa kati ya Sh. 10,000 na Sh. 20,000 wakati dagaa wamekuwa wakiuzwa kwa Sh. 35,000 hadi Sh. 50,000 kwa debe moja la ujazo wa lita kumi.
Wafanyabishara katika mwalo wa Mbamba Bay wanasema wanalazimika kugombea samaki kidogo wanaopatikana, hali inayopandisha bei kwa kuwa mahitaji ni makubwa kuliko bidhaa.
“Tunanyang’anyana samaki hapa kwa sababu hata kama wavuvi mia moja watakwenda ziwani, lakini wengi wao huwa hawarudi na samaki na wanaobahatika wanakuja nao kidogo sana,” anasema Melina Mhagama, mfanyabiashara wa eneo hilo la mwaloni.
Melina ameiambia FikraPevu kwamba, bei ya dagaa nayo haikamatiki kwani kiplasitiki kidogo cha lita tatu ambacho miezi mitano iliyopita kilikuwa kikiuzwa kwa Sh. 2,000, hivi sasa kinauzwa kwa Sh. 10,000 hadi 15,000.
“Vichanja vyote havina dagaa kama unavyoona, mvuvi anaweza kuzama huko ziwani usiku mzima lakini akarudi na lita kumi tu, ni shida,” anaongeza Melina.
Eneo la Mwalo wa Mbamba Bay.
Hata hivyo, Meshack Moyo, mkazi wa Kilosa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbamba Bay, anasema kwamba, miundombinu mibovu nayo imechangia kuadimika kwa samaki katika mji huo pamoja na maeneo mengine yakiwemo Mbinga na Songea.
Moyo anasema kwamba, vipo baadhi ya vijiji ambako wavuvi wanapata samaki lakini wafanyabiashara wanashindwa kwenda kutokana na changamoto ya ukosefu wa usafiri unaosababishwa na ubovu wa barabara.
“Ukienda Liuli, Mkili, Nindai, Ndumbi hadi Lituhi kuna wavuvi wengi, ingawa hawapati samaki wa kutosha, lakini kama samaki wale wangekuwa wanasafirishwa kuja hapa Mbamba Bay na maeneo mengine, pengine wangeweza kupunguza huu uhaba uliopo na hatimaye kushusha bei kuliko ilivyo sasa,” anasema Moyo.
Eneo la Bandari ya Mbamba Bay
FikraPevu imeelezwa kwamba, usafiri pekee unaotegemewa ni wa pikipiki tu ambazo hata hivyo zinaongeza gharama kwa mfanyabiashara.
“Kukodi pikipiki kutoka hapa mpaka Chiwindi (takriban kilometa 50 kutoka Mbamba Bay) inaweza kugharimu hadi Shs. 30,000, sasa kwa mfanyabiashara fedha hizo ni nyingi na biashara inakuwa ngumu,” anaeleza Mariana Hyera, mfanyabiashara katika soko la Mbamba Bay.
Mariana anasema kwamba, wengi wao wana mitaji midogo na hawakopesheki kwa sababu biashara zao ni ndogo, hivyo kuamua kubaki hapo hapo Mbamba Bay na kunyang’anyana samaki na dagaa wachache wanaopatikana.
“Kama miundombinu ingekuwa mizuri na usafiri ungekuwepo, ingeweza kusaidia kwa sababu hata wavuvi wa vijijini wangeweza kuleta wenyewe samaki,” anasema.
Tunachokijua
FikraPevu inatambua kwamba, samaki na dagaa katika Ziwa Nyasa hupatikana kwa msimu, ambapo samaki wanapatikana kwa wingi kati ya mwezi Februari hadi Juni na dagaa ni mwezi Juni hadi Septemba.
Aidha, samaki wanaopatikana kwa mwezi Oktoba hadi Januari, mara nyingi ni wale wadogo maarufu kama vitui.
Samaki aina ya Kambare waliovuliwa katika Ziwa Nyasa.
Kupungua kwa samaki katika ziwa hilo kunaelezwa kwamba kunatokana na sababu za kisayansi kwamba sehemu kubwa ya ziwa hilo liko kwenye kina kirefu kinachozidi meta 250 ambako hewa safi ya oksijeni ni kidogo na hivyo kufanya samaki kushindwa kuzaliana vya kutosha.
Ziwa Nyasa limezungukwa na nchi tatu ambazo ni Tanzania, Malawi na Msumbuji na lipo kwenye usawa wa meta 500 kutoka usawa wa bahari ambapo kina chake ni meta 750, wakati urefu wake ni karibu kilometa 1,000.
FikraPevu inatambua kwamba, utafiti ambao ulifanywa katika ziwa hilo na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kushirikiana na nchi ya Uingereza kati ya mwaka 1991 hadi 1994 na mwaka 1996 hadi 2000, ulionyesha kuwa ziwa hilo lina tani 165,000 za samaki na kati ya kiasi hicho, tani 35,000 ni jamii ya samaki wa maji ya juu ambao wanaweza kuvuliwa bila kuathiri uvuvi kila mwaka.
Aidha, ziwa hilo lina aina 503 za samaki wa mapambo ambao hawapatikani mahali popote ulimwenguni na tangu mwaka 1993 kampuni za kigeni zinauza samaki wa mapambo wanaovuliwa kutoka eneo la Liuli katika nchi za Ujerumani, Ufaransa na Norway.
Inaelezwa kwamba, samaki mmoja wa mapambo huuzwa kati ya dola 450 hadi dola 500.